Polisi: Ni marufuku magari ya mizigo (IT) kupakia abiria

*DC Jokate asisitiza usalama barabarani ni jukumu la kila mwananchi na wote wanatakiwa kufuata sheria bila shuruti

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

JESHI la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani limepiga marufuku magari yote ya mizigo pamoja na magari yanayokwenda nje maarufu kama IT kubeba abiria huku likitoa anyo kwa wamiliki ambao wanaingiza magari mabovu barabarani na kusababisha ajali.
Mkurugenzi wa Shirika la Amend, Simon Kalolo (kulia) akimkabidhi zawadi ya picha Kamanda wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Wilbroad Mutafungwa (wa pili kushoto) wakati wa kutamatisha Programu Maalum ya Mahakama ya Watoto iiyokuwa ikitoa elimu ya usalama barabarani kwa wanafunzi wa shule za msingi za Serikali jijini Dar es Salaam. Hafla hiyo ilifanyika katika shule ya msingi Kongowe iliyopo Mzinga jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Jokate Mwegelo (kushoto) na Kamanda wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Wilbroad Mutafungwa (kulia) wakifurahia jambo kutoka kwa wanafunzi waliokuwa wakiimba wimbo maalum wa usalama barabarani katika hafla maalum ya kufunga rasmi programu hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa kufunga programu maalum ya kutoa elimu ya Usalama Barabarani iliyopewa jina la Mahakama ya Watoto iliyofanyika katika Shule za msingi tisa za Serikali mkoani Dar es Salaam,Kamanda wa jeshi hilo ACP Wilbroad Mutafungwa amesema, marufuku hiyo inaanza mara moja sambamba na ukaguzi wa magari ambayo hayakuwekwa stika ya nenda kwa usalama barabarani.

Akifafanua kuhusu magari ya mizigo kubeba abiria amesema, kumekuwepo na tabia ya baadhi ya abiria au wamiliki wa magari hayo kubeba abiria na matokeo yake yamekuwa yakisababisha ajali, na kwamba jambo hilo ameshalikataza na katika operesheni iliyoanzishwa na Kikosi hicho watakamata magari yatakayobainika kubeba abiria wakati ni maalum kwa kubeba mizigo.
Dereva wa daladala akitia saini kiapo cha kukiri makosa yake mara baada ya kusomewa makosa yake na kuyakubali.

"Tukibaini gari ya mizigo (lori) limebeba abiria tutalikamata gari pamoja na dereva na wamiliki wa magari hayo,lakini hata magari yanayobeba abiria nayo ni marufuku kubeba mizigo.Tunataka watumiaji vyombo vya moto waheshimu sheria za usalama barabarani ili kwa pamoja tushirikiane kupunguza ajali ambzo zinakatisha maisha ya wananchi na wengine kubakia na ulemavu wa kudumu,"amesema.
Meneja Programu wa Shirika la Amend ambalo limejikita katika kutoa mafunzo ya elimu ya usalama barabarani Neema Swai akifafanua jambo wakati wa tukio la kufungwa kwa programu ya Mahakama ya Watoto.

"Kuhusu magari ya IT yanayosafirishwa kwenda nje za nje ya Tanzania nayo ni marufuku kubeba abiria na sheria inawataka kubeba abiria mmoja tu na si vinginevyo na hii haishii kwenye magari ya mizigo na IT tu bali hata magari yanayobeba magazeti nayo ni marufuku kubeba abiria.Katika hili hatutakuwa na utani, dereva na wamiliki lazima wafuate sheria za usalama barabarani,"amesema Kamanda Mutafungwa.

Amesema, iwapo abiria anataka kusafiri anatakiwa kwenda kwenye vituo vya mabasi ya abiria ili kupata usafiri wa uhakika na unaotambulika kwa mujibu wa sheria."Nasisitiza ni marufuku abiria kupanda gari ya mizigo,tutashukua hatua Kali.Tunakumbuka ajali ya gari iliyotokea Tanga watu watano walipoteza maisha na walikuwa wanasafiri na gari ya mizigo aina ya Fuso."

Kuhusu makontena au mizigo ambayo haifungwi vizuri na kusababisha ajali amesema madereva na wahusika wanatakiwa kukahakikisha wanafunga mizigo ili kuwa salama wakati wote wa safari na kuongeza Jumatatu ya Aprili 4, mwaka huu yeye (Kamanda Mutafungwa) na maofisa wake watakutana na madereva waliopo Bandari ya Dar es Salaam kwa lengo la kuzungumza na kukumbushana wajibu wa kufuata Sheria za Usalama barabarani.

Akizungumza programu ya Usalama Barabarani iliyoandaliwa na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kwa kushirikiana na Shirika la Amend Kamanda Mutafungwa amesema programu hiyo ni muendelezo wa kufikisha elimu ya Usalama Barabarani na kupitia programu hiyo Kuna madereva ambao watakuwa mabalozi wa wengine katika kuhamasisha kuzingatiwa kwa sheria za barabarani.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke Jokate Mwegelo akizungumza alipokuwa akitoa hotuba yake ya kufunga Programu hiyo iliyofanyika katika shule la msingi ya Kongowe Jijini Dar es Salaam.

Kwa upande mgeni rasmi wakati wa kufunga programu hiyo,Mkuu wa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam, Jokate Mwegelo mbali ya kutoa shukrani kwa Shirika la Amend kwa kutoa mafunzo ya Usalama Barabarani kwa wanafunzi wa Shule za msingi amesema, suala la usalama barabarani ni jukumu la kila mwananchi na wote wanatakiwa kufuata sheria bila shuruti

Amesema, kwa mujibu wa takwimu za jeshi hilo zinaonesha kuwa kwa kipindi cha mwaka 2021 watu 1245 walipoteza maisha yao na wengine 2, 023 walijeruhiwa kutokana na ajali za barabarani.

"Kati ya takwimu hizo wanafunzi 56 walipoteza maisha na wengine 65 walijeruhiwa.Ni wazi kuwa jitihada zaidi zinahitajika katika kupunguza ajali na kundi ambalo liko hatarini ni wanafunzi ambao shule zao nyingi ziko barabarani,"amesema.
Wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia wakifuatilia kwa ukaribu matukio yanayoendelea katika hafla hiyo kutoka kwa mkalimani wao wa alama ya lugha (hayumo pichani) wakati wa kufunga rasmi programu hiyo jijini Dar es Salaam.

Aidha, ametumia nafasi hiyo kuliomba Jeshi la Polisi kuangalia namna ya kufanya kuhakikisha wanafunzi hawakai muda mrefu kwenye vituo vya daladala kwani madereva wengi wa daladala hawawapikii na hivyo wanafunzi kuchelewa kurudi majumbani.

"Angalieni namna ya kuweka utaratibu ili madereva wa daladala wasiache wanafunzi vituoni,"amesema.

Pia amewataka Wakala wa Barabara Tanzania ( TANROADS) na Wakala wa Barabara Vijijini ( TARURA) kuhakikisha barabara zinakuwa salama kwa watumiaji wote huku akisisitiza umuhimu wa kuwekwa kwa alama za barabarani yakiwemo maeneo ya shule.

Awali Mkurugenzi wa Shirika la Amend Tanzania Simon Kalolo akizungumzia programu ya Mahakama ya Watoto amesema lengo ni kuendelea kufikisha elimu ya Usalama barabarani kwa jamii ya Watanzani na wamekuwa wakitoa mafunzo hayo katika shule mbalimbali nchini.
Mkurugenzi wa Shirika la Amend Tanzania Simon Kalolo (aliyesimama) akizungumza kuhusu umuhimu wa programu za mafunzo ya elimu ya usalama barabarani ambazo wamekuwa wakizitoa maeneo mbalimbali nchini.

Aidha, amesema uchunguzi unaonesha kuwa maeneo ya mijini na yanayoendelea zaidi ya asilimia tatu ya Watoto wanajeruhiwa kwa ajali za barabarani kila mwaka na zaidi ya asilimia 90 ya Watoto wanaoathirika ni wanaotembea kwa miguu huku akisisitiza Shirika lao litaendelea kushirikiana na wadau wengine katika kuifikisha elimu ya usalama barabarani kwa Watanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news