Rais Dkt.Mwinyi: Asanteni, tuendelee kujitoa kwa ajili ya wote wasiojiweza

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewashukuru wananchi wenye uwezo mbao wamejitolea kuwasaidia wananchi maskini na wale wanaoishi katika mazingira magumu katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt.Hussein Ali Mwinyi akijumuika na Wananchi wa Mkoa wa Kusini Unguja (hawapo pichani) katika futari maalum aliyowaandalia katika ukumbi wa Dkt.Ali Mohamed Shein Tunguu (SUZA) na (kushoto kwa Rais) ni Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja , Mhe.Rashid Hadidi na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt.Abdalla Juma Mabodi na (kulia kwa Rais) ni Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kaabi.(Picha na Ikulu).

Alhaj Dkt. Mwinyi ametoa shukurani hizo kwa wananchi wa Mkoa wa Kusini Unguja, ambapo kwa nyakati tofauti alikabidhi sadaka za chakula kwa wananchi wa makundi tofauti hao katika eneo la TC Dunga Wilaya Kati pamoja na Unguja Ukuu kwa wanachi wa Wilaya ya Kusini Unguja.

Amesema ni jambo jema kwa wananchi hao kuwasaidia watu wengine wenye uwezo duni, huku akiwataka wananchi hao kumshukuru Mwenyezi Mungu na kuwaombea dua.

Alhaj Dkt. Mwinyi aliwataka wananchi hao kulitumia vyema kumi la mwisho wa mwezi wa Ramadhani, kwa kuzidisha kufanya ibada na kumdhukuru Mwenyezi Mungu, ikiwa pamoja na kuitafuta Lailatul Kadr.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Hadidi Rashid Hadidi alimueleza Alhaj Dk. Mwinyi kuwa wananchi wa Mkoa huo wamefarijika sana na sadaka hiyo.
Miongoni mwa sadaka hizo zilizokabidhiwa kwa jamii ya watu wenye ulemavu, yatima pamoja na wale wanaoishi katika mazingira magumu ni pamoja na mchele, sukari, unga, ngano, mafuta ya kupikia pamoja na tende.

Katika hatua nyengine, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Mwiyi alishiriki katika hafla ya Futari aliiyoiandaa kwa ajili ya wananchi wa Mkoa huo iliofanyika katika Ukumbi wa Dk. Ali Mohammed SheinTunguu, Mkoa Kusini Unguja.

Katika salamu zake, Alhaj Dkt. Mwinyi aliahidi kuendeleza utamaduni wa kufutarisha kila mwaka kama alivyorithi kutoka kwa watangulizi wake.
Naye, Mkuu wa Mkoa huo Hadidi Rashid Hadidi alimshukuru Alhaj Dkt. Mwinyi kwa maandalizi ya futari hiyo na kusema wananchi wa Mkoa huo wamefarijika sana.

Post a Comment

0 Comments