Rais Dkt.Mwinyi atuma salamu za rambirambi kifo cha Mwai Kibaki

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ametuma salamu za rambirambi kwa Rais wa Jamhuri ya Kenya, Uhuru Kenyata kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Taifa hilo, Mwai Kibaki.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi.

Katika salamu hizo, Rais Dkt. Mwinyi alieleza jinsi alivyopokea kwa mshituko na huzuni kubwa kifo cha Rais Mwai Kibaki ambaye alikuwa Rais wa tatu wa Jamhuri ya Kenya tangu mwaka 2002 hadi 2013.

Salamu hizo za rambirambi zilieleza kuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wananchi wake wote wanaungana na ndugu zao wa Kenya katika kipindi hichi cha msiba na kumuombea kwa Mwenyezi Mungu amlaze marehemu Kibaki mahala pema peponi. Amin.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi alimsihi Rais Uhuru Kenyata pamoja na wananchi wote wa Kenya kuendelea kuwa na subira katika kipindi hichi kigumu cha msiba.

Rais Dkt. Mwinyi alisema kuwa Rais Mwai Kibaki atakumbukwa kwa juhudi zake kubwa alizozichukua katika kuuimarisha uchumi pamoja na demokrasia ya Kenya.

Rais Uhuru Kenyata alitangaza kwamba, Rais Kibaki (90) amefariki dunia usiku wa siku ya Alhamisi ya Aprili 21,2022.

Post a Comment

0 Comments