Rais Dkt.Mwinyi, Mwenyekiti wa ACT Wazalendo wateta, wasisitiza ushirikiano

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameeleza kwamba ushirikiano wa pamoja unahitajika katika kuiendeleza na kuiimarisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa maslahi ya Wazanzibari wote.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo Aprili 25,2022 Ikulu jijini Zanzibar wakati alipokutana na Mwenyekiti mpya wa Chama Cha ACT – Wazalendo, Juma Duni Haji ambaye alifika Ikulu kwa ajili ya kujitambulisha rasmi.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi alieleza kwamba ujio wa kujitambulisha pamoja na kufanya mazungumzo na kiongozi huyo ni mwelekeo mzuri wa kuiimarisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa pamoja na mustakbali mpana wa kuiiendeleza Zanzibar.

Rais Dkt. Mwinyi alitumia fursa hiyo kumpongeza Mwenyekiti huyo mpya wa ACT- Wazalendo Taifa kwa kuchaguliwa na chama chake kushika wadhifa huo.

Nae Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Taifa Juma Duni Haji kwa upande wake alitoa shukurani kwa Rais Dk. Mwinyi kwa kupata fursa ya kuja kujitambulisha kwa Rais pamoja na kujadili masuala mbali mbali juu ya mustakbali wa Zanzibar.

Katika maelezo yake Mwenyekiti huyo mpya wa ACT-Wazalendo alieleza kuwa mbali ya mazungumzo hayo pia, amepokea wito wa Rais Dkt. Mwinyi wa kutaka kukaa pamoja na kujadili masuala yenye mustakbali wa wananchi wa Zanzibar.

Alisema kuwa Rais Dkt. Mwinyi mara nyingi amekuwa akisisitiza umuhimu wa kukaa pamoja na kuzungumza badala ya kubishana kwenye majukwaa na kutupiana maneno.

Hivyo, alieleza jinsi alivyovutiwa na wito huo wa Rais Dkt.Mwinyi ambao una umuhimu mkubwa juu ya mustakabali wa Zanzibar.

Mwenyekiti huyo mpya wa ACT-Wazalendo alitumia fursa hiyo kumpongza Rais Dkt. Mwinyi kutokana na ukaribisho wake sanjari na mazungumzo yao ambayo yalikuwa mazuri huku akiahidi kuwaeleza wanachama wake juu ya suala zima la maridhiano linavyoendelezwa kama vile ilivyokusudiwa.

“Mimi Mwenyekiti wao nimehakikishiwa na Mheshimiwa Rais kwamba hakuna tatizo juu ya yale yote waliyokubaliana na Marehemu Maalim Seif kwani sote tuna nia ya kuijenga nchi yetu,”alisema Mwenyekiti huyo mpya wa ACT- Wazalendo.

Sambamba na hayo, Mwenyekiti huyo mpya wa ACT-Wazalendo alitumia fursa hiyo kuwasihi wanachama wa chama hicho kuendeleza siasa zenye tija na kuepuka vijembe majukwani, kwani hatua zilizokusudiwa katika kuiendeleza Zanzibar zinakwenda vizuri.

Juma Duni Haji alishinda nafasi ya Mwenyekiti wa Chama Cha ACT- Wazalendo Taifa kufuatia uchaguzi uliofanyika kwenye Mkutano Mkuu Maalum wa chama hicho mnamo Januari 29, 2022.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news