RC Kunenge afungua msikiti mpya Kibaha, atoa maelekezo na onyo

NA ROTARY HAULE

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge ameufungua Msikiti wa Masjd Mariya uliopo Kata ya Visiga katika Halmashauri ya Kibaha Mjini huku akiwataka viongozi wa Msikiti huo kuhakikisha unatumika kwa malengo ya kufundisha dini na sio kuweka kambi za kihalifu.
Kunenge amefungua Msikiti huo jana kwa kushiriki Swala ya Adhuhuri akiambatana na Shehe Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Hamis Mtupa pamoja na waumini mbalimbali waliopo katika eneo hilo.

Akizungumza mara baada ya kufungua msikiti huo, Kunenge amesema kuwa kazi ya nyumba za ibada ni kuhubiri amani na kutoa mafundisho ya dini kwa jamii kwa hiyo ni vyema viongozi wakawa wasimamizi wazuri.

Amesema kuwa, Serikali haina dini lakini wananchi wake wana dini mbalimbali na ndio maana imetoa haki ya kuabudu kwa kuwa inaamini ibada hizo zinasaidia kujenga amani ya nchi, lakini isitokee Msikiti unafanya kinyume na kuhubiri dini.

Aidha,amesema ikitokea msikiti huo unatumika visivyo halali ikiwemo ya kuweka kambi ya kihalifu ni wazi kuwa Serikali haitavumilia na hatua kali za kisheria zitachukuliwa maramoja.

"Leo nimekuja hapa kufungua Msikiti huu lakini lazima mtambue mimi ni Mkuu wa Mkoa na mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama kwahiyo nikigundua kuna mambo ya tofauti yanafanyika hapa hatutosita kuchukua hatua,"amesema Kunenge

Kunenge, ameishukuru taasisi ya Miraji Islamic Centre chini ya mwenyekiti wake Shehe Arif Surya kwa jitihada zake za kufanikisha ujenzi wa Msikiti huo kwani hiyo ni hatua kubwa ya kuwaleta waumini pamoja hususani katika suala la kuhubiri amani.
Kunenge,pamoja na mambo yote lakini amewasisitiza waumini wa Msikiti huo kufanya maombi ya kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan dhidi ya kumuepushia na shari,kuwa na afya bora,kumzidishia hekima pamoja na ujasiri wa kuendelea kuwatumikia Watanzania.

"Nawaomba pia tutumie Msikiti huu kumuombea kwa mwenyezi Mungu Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ili haweze kuwa imara Katika kuwatumikia Watanzania na kuleta maendeleo ya nchi yetu kwakuwa tunaona kazi kubwa anayofanya,"amesema Kunenge.

Kunenge akiwa Msikitini hapo alitumia nafasi hiyo kugawa msaada wa vyakula kwa ajili ya futari kwa waumini zaidi ya 300 msaada ambao ulitolewa na taasisi hiyo huku akikemea wafanyabiashara kuacha kutumia Mwezi wa Ramadhani kupandisha bei ya vyakula.

"Nitoe wito wa wafanyabiashara kuwa waache kupandisha bei ya vyakula kiholela kwakuwa huu sio Mwezi wa kufanya hivyo kwakuwa bei ya vyakula inapangwa na Serikali kwa utaratibu wake maalum,"amesema Kunenge
Naye Shehe Mkuu wa Mkoa wa Pwani Hamis Mtupa,amesisitiza viongozi kuendelea kuhubiri amani kwakuwa wananafasi ya kupita maeneo mbalimbali kwa ajili ya kukutana na waumini.

Mtupa amesema kuwa bila amani hakuna maisha huku akisema mtu wa amani ndiye mwenye kupasa kuingia katika nyumba za ibada na kamwe wasimkaribishe mtu wa wasiwasi kuingia nyumba ya ibada.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Miraji Islamic Centre Arif Surya,amesema kuwa Taasisi hiyo imekuwa ikisaidia jamii mbalimbali hapa nchini kwa kujenga misikiti na kutoa huduma za vyakula kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Hata hivyo,Surya amemshukuru Kunenge kwa kushiriki katika ufunguzi wa mkutano huo huku akiahidi kutumia Msikiti huo kwa kazi ya kuhubiri dini na kustawisha amani kama ambavyo Serikali inaelekeza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news