RC Telack:Matumizi sahihi ya mbolea yana tija kubwa katika kilimo Lindi

NA NURU MWASAMPETA-TFRA

MKUU wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack amesema uhamasishaji wa matumizi sahihi ya mbolea kwa wakulima wa mkoa wake kutapunguza kilimo cha kuhamahama kwa wananchi wa mkoa huo.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bi. Zainab Telack akivuna muhindi katika moja ya shamba lililopandwa kwa mbolea ili kudhibitisha tija iliyotokana na kupanda kwa kutumia mbolea katika eneo la Chimbila B Wilaya ya Luangwa mkoani Lindi leo Aprili 11, 2022

Amesema, wananchi wake wamekuwa wakihamahama kutokana na kuamini kwamba pindi shamba likilimwa linapoteza rutuba na hivyo kupelekea wananchi hao kuhamia eneo lingine wakiamini kuwa eneo hilo linakuwa na rutuba ya kutosha kustawisha mazao.

Ametoa kauli hiyo leo Aprili 11, 2022 alipokuwa akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Lindi ikiwa ni maadhimisho ya Siku ya Mkulima iliyoandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA).
Wananchi mbalimbali walioshiriki katika maadhimisho ya siku ya mkulima yaliyofanyika leo katika kijiji cha Chimbila B wilayani Ruangwa mkoani Lindi.

"Kwa hili la uhamasishaji wa matumizi ya mbolea mlilolileta naaamini wananchi wetu watakuwa na makazi ya kudumu. Sasa tuwape uhakika kwamba kwenye ardhi hiyohiyo wakilima kwa kutumia mbolea watavuna mazao ya kutosha,"Telack ameongeza.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bi. Zainab Telack (kushoto) akifuatilia maelezo kutoka kwa Kaimu Meneja wa Ukaguzi kutoka TFRA, Dkt. Asheri Kalala alipokuwa akikagua mashamba darasa yaliyolimwa kwa kutumia mbolea na yale ambayo hayajatumia mbolea leo.

Maadhimisho hayo ni kilele cha uhamasishaji wa matumizi sahihi ya mbolea kwa wakulima wa mkoa wa Lindi yaliyoanza mwezi Mei, 2021 kufuatia mkoa huo kuwa na matumizi hafifu ya mbolea ukilinganisha na maeneo mengine ya nchi kama vile Iringa, Mbeya, Mwanza na maeneo mengine.

Akizungumzia sababu zinazopelekea uwepo wa matumizi hafifu ya mbolea kwa wananchi wa Mkoa wa Lindi, Telack alisema ni kutokuwepo kwa wauzaji wa mbolea katika mikoa ya kusini na kuyataka makampuni yanayojihusisha na biashara ya mbolea kufungua matawi ili kuwawezesha wakulima wa maeneo hayo kupata huduma hiyo.

"Tunahitaji elimu tunahitaji kusaidiwa na ili mtusaidie kwa uharaka leteni tawi karibu, tuwasaidie wakulima naomba tuwasaidie wakulima," Telack amesisitiza.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bi. Zainab Telack akifuatilia maelezo ya aina za mbolea kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Stephan Ngailo.

Kwa upande wa huduma ya upimaji wa afya ya udongo inayoweza kuwasaidia wakulima kujua aina ya udongo na mazao yanayoweza kustawi Telack amelitaka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) kufungua tawi katika mkoa huo ili kuwezesha wananchi kupata huduma hiyo.

Aidha, Mkuu wa Mkoa Telack aliwaelekeza wakurugenzi wa halmashauri kuwekeza kwa wakulima na kuhakikisha mazao wanayolima yanawekwa mbolea ili waongeze tija.

Akinukuu kauli ya Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) amesema, Wewe umesema kuona ni kuamini na mimi nasema kuona ni kujifunza na sisi tumejifunza na kuwataka wakulima waliopata elimu hiyo kufikisha elimu hiyo kwa.wakulima wengine ili na wao wapate uelewa huo.

Akihitimisha hotuba yake, Bi. Telack amesema, kwa sababu Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amewekeza na sisi tuwekeze, naomba sasa tuwekeze kwa wakulima ili mhe. Rais aone tija inayotokana na uwekezaji alioufanya kwenye Sekta ya Kilimo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa TFRA, Dkt. Ngailo amesema mamlaka iliamua kufanya uhamasishaji wa matumizi sahihi ya mbolea katika mikoa ya Lindi na Mtwara kutokana na maeneo haya kutojihusisha na matumizi ya mbolea kwenye shughuli zao za kilimo.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Stephan Ngailo akitoa taarifa fupi ya uhamasishaji wa matumizi sahihi ya mbolea kwa wakulima wa Mkoa wa Lindi yaliyofanyika katika Kijiji cha Chimbila B wilayani Ruangwa leo.

Amesema, hiyo ni hatua ya awali katika uhamasishaji wa matumizi sahihi ya mbolea itakayopelekea wadau na wafanyabiashara wa mbolea kufungua biashara ya mbolea katika mikoa ya Kusini yaani Lindi na Mtwara.

Amesema, kufuatia uwepo wa bandari ya Mtwara itarahisisha usafirishaji wa mbolea kutoka nje ya nchi ya kushishwa moja kwa moja kwenye bandari hiyo na kuwapunguzia wakulima adha ya upatikanaji wa mbolea.

"Tumeona kuanzishwa mashamba darasa ni njia sahihi ya kuwahamasisha wakulima kutumia mbolea katika kilimo kwani vikundi vya wakulima vilishiriki mwanzo mpaka mwisho katika kuhudumia mashamba darasa hayo" Dkt. Ngailo alisisitiza
Mkuu wa mkoa wa Lindi, Bi. Zainab Telack akimsikiliza mwanakikundi wa Jitegemee Bi. Samia Ngajua akitoa shuhuda wa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea waliyoipata kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) walipokuwa wakitoa elimu hiyo kupitia mashamba darasa yaliyoanzishwa kwa madhumuni hayo.

Kwa upande wa vikundi vya wakulima kupitia risala yao walieleza manufaa waliyoyapata kufuatia elimu ya matumizi sahihi ya mbolea na namna walivyohusika katika maandalizi mpaka mavuno ya mazao hayo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news