TAEC yafanya kikao na wadau kujadili Rasimu ya Mpango wa Miradi ya Teknolojia ya Nyuklia Nchini

NA MWANDISHI MAALUM

TUME ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) jana Aprili 14,2022 imekutana na wadau jijini Dodoma ili kujadili Rasimu ya Mpango wa Ushirikiano kati ya Tanzania na Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani (IAEA).
Hatua hiyo inalenga utekelezaji wa miradi ya teknolojia ya nyuklia, Country Programme Framework (CPF) kupitia Sekta za Afya, Maji, Lishe, Chakula, Kilimo, Nishati, Viwanda, Rasimali Watu na usalama wa matumizi ya mionzi na matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia unaotarajiwa kutekelezwa katika kipindi cha mwaka 2023-2027.
Kikao hicho kimefanyika katika Chuo cha VETA jijini Dodoma kilifunguliwa rasmi na Profesa Maulilio Kipanyula, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Jumla ya wadau 40 kutoka katika taasisi na wizara mbalimbali wameudhuria ikiwemo Wizara ya Afya Zanzibar (MOH.ZNZ), Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (MOEST), Wizara ya Mifugo, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Maji, Mamlaka ya Chakula na Dawa Zanzibar, Hospitali ya KCMC, Chuo cha Kilimo cha Sokoine.

Wengine ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC), Taasisi ya Taifa ya Uhimilisha wa Mifugo (NAIC), Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), Wakala wa Uchunguzi wa Magonjwa ya Mifugo (TVLA), Hospitali ya Bugando (BMC).

Sambamba na Taasisi ya Utafiti wa Chai (TRIT), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Taasisi ya Chuo Kikuu cha Nelson Mandela (NM-AIST) Taasisi ya Utafiti wa Viwanda na Maendeleo (TIRDO) na Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu (TPHRA-TPRI).

Akifungua kikao hicho rasmi, Prof. Kipanyula alimshukuru Profesa Busagala, Mkurugenzi Mkuu wa TAEC kwa kukutanisha wadau ili kufanya mkutano huo wa mapitio ya mpango/programu ya (CPF) katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo baina ya Tanzania na Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani.
CPF ni Mpango wa Ushirikiano wa Kiufundi Kati ya Tanzania na Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki Duniani ambao unahakisi mahitaji na vipaumbele vya maendeleo ya nchi mwanachama kwa upande mmoja na upatikanaji wa rasilimali za utekelezaji wa vipaumbele hivyo kwa upande mwingine. 

Aidha, vipaumbele hivi ni muhimu kwa ajili ya kuahinisha maeneo yote ambayo teknoljia ya nyuklia inaweza kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

"Ifahamike kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inashiriki katika programu za kudhibiti na kuhamasisha matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia hapa nchini zinazofadhiliwa na Shirika la Nguvu za Atomu Duniani.

"Sambamba na programu za kanda ya Afrika kupitia Foramu ya AFRA. Kupitia programu hizo, Tanzania imeendelea kunufaika na miradi mbalimbali ambayo imesaidia kuboresha sekta za kilimo, afya, mifugo, maji, rasilimali watu, na lishe," alisema Profesa Kipanyula.

Profesa Kipanyula aliendela kusema kwamba katika mpango unayomaliza muda wake mwaka huu, Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani (IAEA) imetekeleza miradi ya kitaifa ambayo imeendelea kuboresha Sekta za Kilimo, Afya, Mifugo, halikadhalika kujenga uwezo wa rasilimali watu, rasilimali za maji na lishe. Na utekelezaji wa miradi hii unaratibiwa na Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC).

Miradi yote ya Kitaifa inayotumia teknolojiaa ya nyukliaa hapa nchini inatekelezwa kwa makubaliano na Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani na miradi hii imetoa matokea makubwa kwa maendeleo ya nchi yetu kwenye sekta mbalimbali ni kama ifuatavyo:

Katika sekta ya Kilimo, Mpunga, Mahindi na Mtama ni miongoni mwa mazao matatu muhimu ya nafaka nchini Tanzania ambayo uzalishaji wake umekuwa ukikumbwa na changamoto mbalimbali ikiwemo magonjwa pamoja na ukame. Mojawapo ya magonjwa ambayo yameathiri kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa mpunga nchini ni ugonjwa unaojulikana kama Yellow Mottle Virus (RYMV).

"Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani kwa kushirikiana na Taasisi ya utafiti wa kilimo Zanzibar (ZARI) pamoja na chuo Kikuu cha kilimo Sokoine (SUA) zinatekeleza mradi unaotumia teknolojia ya nyuklia, ambapo kupitia mradi huo taasisi hizo zilipata mbegu bora aina ya SUPA BC inayotumika (Zanzibar) na TASIRI ilipatikana (Tanzania Bara) ambapo kwa ujumla wake mbegu hizi zinahimili maradhi mbalimbali ikiwemo magonjwa ya “Yellow Mottle Virus” (RYMV) pamoja na ukame," alisema Profesa Kipanyula.

Aidha, utafiti wa kuboresha vinasaba vya mbegu hizo kwa ajili ya kuboresha ladha, kuongeza wingi wa mazao pamoja na kuhimili maeneo yenye chumvi kali bado unaendelea huku mbegu hizo zikiongeza huzalisha katika wastani wa tani tatu zaidi kuliko ile ya kwanza yaani tani saba (7) badala ya tani nne (4) kwa hekta kama ilivyokuwa awali.

Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani kwa kushirikiana na TAEC inaendelea na utafiti kuboresha mbegu za mahindi na shairi katika Taasisi ya utafiti wa Kilimo Seliani Arusha kwa kutumia teknolojia ya nyuklia, ambapo mradi huo unategemewa kusaidia kupatikana kwa mbegu bora za mahindi na shairi ambazo zitastahimili magonjwa mbalimbali ikiwemo ukame hatimaye kutoa mavuno mengi zaidi.

Profesa Kipanyula katika taarifa yake pia amebainisha ya kwamba katika sekta ya mifugo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejikita katika kuboresha uzalishaji wa sekta ya mifugo ikiwemo kuongeza upatikanaji wa maziwa na nyama bora, hivyo Tanzania kwa ushirikiano na Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani pamoja na Kituo cha Uhamilishaji wa mifugo Arusha (NAIC).

Kupitia uratibu wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania pamoja na Wakala wa Maabara za Mifugo (TVLA) nchi inaendelea kuzalisha mbegu bora za ng’ombe wanaotoa maziwa mengi na nyama nyingi ambapo mpaka sasa maisha ya wafugaji Tanzania bara na Visiwani yameboreka kupitia programu hii, kwani mbegu hizo zimekuwa zikitawanywa kwa wafugaji katika maeneo mbalimbali nchini, ambapo ngo’mbe wengi wameendelea kupandishwa kwa njia ya Uhimilishaji Bandia (Artificial Insemination).

Profesa Kipanyula amebainisha kuwa Teknolojia ya nyuklia hutumika kubaini ng’ombe ambao hawajashika mimba na hatimae kupandishwa tena ndani ya siku 14 ambapo njia hii njio njia pekee ambayo husaidia kugundua kwa haraka kama ngombe hajashika mimba na hivyo kupunguza muda wa huduma za upandishaji.

Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani kupitia TAEC inaendelea kuboresha maabara za mifugo huko Zanzibar ambapo kwa sasa mtambo wa kuzalishia gesi ya hewa baridi “Liquid Nitrogen Gas” umeboreshwa na sasa utasaidia kuhifadhi na kusafirisha mbegu za madume ya ng’ombe na kuwafikia wafugaji zingali hai katika maeneo mbalimbali ya wafugaji na kupandishwa kwa majike ya ng’ombe kwa njia ya uhimilishaji (AI) zimesaidia kuongeza ufanisi wa uzalishaji na upatikanaji wa maziwa mengi.

Profesa Kipanyula alihitimisha kwa kusema kuwa matumizi ya teknolojia ya nyuklia yalifanikiwa kwa kiasi kikubwa kutokomeza kabisa wadudu aina ya mbung’o ambao walikuwa na athari kubwa kwa sekta ya mifugo visiwani Zanzibar, hivyo kwa kutumia Teknolojia hiyo madume ya wadudu hao yalihasiwa na hatimaye kufanikiwa kuwatokomeza mbungo katika visiawa vya Zanzibar hivyo kufanikiwa kupunguza kiwango kikubwa cha ugonjwa wa ‘‘nagana’’ kutoka asilimia 19 hadi sifuri (0). Kutokomezwa kwa mbung’o visiwani Zanzibar kumeleta mafanikio makubwa kwa kuboresha sekta ya mifugo na kuinua hali ya maisha ya wafugaji visiwani humo.

Mkurugenzi Mkuu wa TAEC, Profesa Busagala katika taarifa yake aliyeitoa kwa wadau amesema kuwa katika sekta ya afya kwa muda wa kipindi cha miaka mitano kuanzia (2017-2022), Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani kwa kushirikiana na TAEC imefanya juhudi kubwa katika kuhakikisha mashine za tiba ya saratani kwa njia ya mionzi na mashine za kupangilia mfumo wa tiba (Treatment Planning System) katika Hospitali ya Bugando zinapatikana, ili kusaidia kutoa huduma ya tiba ya saratani kwa wananchi wa kanda ya ziwa ambao wamekuwa wakihangaika kwa muda mrefu kuyafuata matibabu ya aina hiyo katika Taasisi ya Saratani Ocean Road jijini Dar es salaam.

Vilevile kwa kipindi hicho, jumla ya vifaa tiba vyenye thamani ya TZS 33.4 billioni vilinunuliwa pamoja na wataalamu tisa kutoka sekta hiyo walihudhuria mafunzo (Fellowship) ya muda mrefu ambapo kiasi cha TZS 23.8 billioni kilitumika kulipia mafunzo hayo. Mradi umetumia jumla ya TZS 52.95 bilioni kwa kipindi cha miaka 5 alisema Profesa Busagala.

Pia Profesa Busagala amebainisha kuwa Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani kwa kushirikiana na TAEC, Wizara ya Afya pamoja na Taasisi ya Chakula na Lishe katika lishe ya binadamju linaendelea na utafiti unaotumia teknolojia ya nyukilia kuchunguza matatizo ya lishe kwa watoto wadogo, kwani teknolojia hii inatoa taarifa sahihi ya kiuchunguzi ukilinganisha na matumizi ya njia zingine.

Kwa muda wa miaka mitano kuanzia 2017 mpaka 2021, jumla ya gharama ya vifaa vilivyo nunuliwa kwa ajili ya kuboresha lishe ya bindamu ni kiasi cha TZS 1.2 billioni. Mafunzo mbalimbali yalitolewa kama vile kuhudhuria mikutano pamoja na semina mbali mbali ndani na nje ya nchi ambapo gharama ya TZS 211.7 million zilitumika. Jumla ya TZS 1.4 billioni kwa kipindi cha miaka 5 zilitumika kwenye mradi huu uliofadhiliwa na Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani, alisema Profesa Busagala.

Profesa Busagala aliongeza kuwa katika sekta ya maendeleo ya rasilimali watu wafanyakazi kutoka sekta mbalimbali wamepatiwa mafunzo kupitia mradi wa Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani katika maeneo tofauti tofauti ikiwemo pamoja na Mifugo, Afya ya Binadamu, Kilimo, usimamizi wa rasilimali za Maji, Lishe, Nishati na Viwanda. Mafunzo yaliyotolewa yalikua ya muda mfupi katika kipindi cha wiki moja hadi tatu na yale ya muda mrefu kuanzia miezi sita hadi miaka mitatu, hivyo kwa muda wa miaka mitano (2017 – 2022), jumla ya TZS 3.2 Trillion Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani ilitumia fedha hizo kugharamia mafunzo pamoja na vifaa vya utafiti kwa wanafunzi kutoka katika Wizara na Taasisi mbambali hapa nchini.

Katika Sekta ya usimamizi wa rasilimali za maji kwa muda wa miaka mitano iliyopita (2017 – 2021) jumla ya thamani ya vifaa vilivyo nunuliwa na Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani kwenye Usimamizi wa Rasilimali za Maji ni TZS 218.5 millioni, zikijumuisha mafunzo mbalimbali yalitolewa ikiwemo mafunzo ya muda mrefu pamoja na ziara za kisayansi ambazo zilighalimu kiasi cha TZS 251.9 millioni hivyo jumla ya TZS 470.4 millioni zimetumika kwa kipindi hicho alibainisha Profesa Busagala.

Profesa Busagala aliongeza kwa kusema mafanikio yote haya yametokana na vipaombele vya Mpango wa Ushirikiano wa Kiufundi Kati ya Tanzania na Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki Duniani unaomaliza muda wake ambapo uhamisho wa nyuklia na rasilimali za ushirikiano wa kiufundi ulielekezwa ili kusaidia malengo ya maendeleo ya kitaifa.
Katika taarifa yake Profesa Kipanyula aliwaelekeza wadau kuwa mpango mwingine wa (CPF) unaoandaliwa wa kipindi cha miaka mitano (5) yaani 2023 – 2027 uzingatie na kujikita katika vipaumbele vya kitaifa ili kuinua na kukuza uchumi wa Viwanda, Kilimo, Afya, Elimu, Mifugo, Rasilimali za Maji, Madini, Nishati pamoja na uchumi wa bluu hapa nchini

Na katika kuwezesha mchango wa teknolojia hii kuwafikia wananchi, wizara yangu itafanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa mipango ya programu inatekelezwa bila vikwazo vya aina yeyote na hii itahusisha pia kuahakikisha kunakuwa na misamaha ya kodi ya vifaa vinavyopokelewa kupitia miradi hii inatolewa ili kuondoa vizuizi vya utekelezaji wake na kufikia malengo tuliyojiwekea, alieleza Profesa Kipanyula.
Profesa alimaliza kwa kuwaambia wadau waweze pia kuahinisha maeneo mapya ambayo yanahitaji kuzingatiwa katika Mpango wa sasa na kuainisha ipasavyo vipaumbele vya jumla vinavyolenga mahitaji ya kitaifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news