TAWA:Tutaendelea kumuenzi Mwalimu Nyerere daima

NA FRESHA KINASA

MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyapori Tanzania (TAWA) imesema inathamini na kumuenzi kwa dhati Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kutokana na kuwa mstari wa mbele katika suala la uhifadhi na kusimamia kikamifu rasilimali za nchi kwa maendeleo endelevu ya Watanzania.
Kauli hiyo imetolewa Aprili 13, 2022 na Mkuu wa Kitengo cha Habari wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Twaha Twaibu wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Maadhimisho ya Kumbukizi ya Miaka 100 ya kuzaliwa kwa Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambayo kitaifa yamefanyika Wilaya ya Butiama Mkoa wa Mara.

Katika maadhimisho hayo, mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali, mashirika ya umma, binafsi, chama pamoja na wananchi.

Twaha amesema, Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi mahiri na muadilifu aliyesimama kidete kusimamia rasilimali za nchi na kuhakikisha zinawanufaisha Watanzania wote. 

Na kupitia tamko lake la Uhifadhi la mwaka 1961 alililolitoa limewezesha Sekta ya Utalii kukua kwa kiwango kikubwa na kuendelea kutoa mchango katika maendeleo ya uchumi wa nchi.

Pia, Twaha amesema katika Maadhimisho ya Miaka 100 ya Kumbukizi ya Kuzaliwa kwa Mwalimu Nyerere, mamlaka hiyo imeweza kutoa elimu kwa wananchi waliofika katika banda la TAWA. Ambapo wameweza kuelimishwa masuala mbalimbali ikiwemo majukumu ya mamlaka hiyo, umuhimu wa kuendelea kulinda wanyamapori kwa manufaa endelevu ya nchi.

Aidha, Twaha amewahimiza Watanzania kujitokeza kwa wingi kutembelea hifadhi mbalimbali hapa nchini na mapori tengefu kwa ajili ya kufanya utalii wa ndani.

Mathias Juma ni Mkazi wa Butiama ambapo akizungumza na DIRAMAKINI amesema kuwa, kitendo cha TAWA kutoa elimu kwa wananchi kinasaidia kwa ufanisi wananchi kutambua umuhimu wa wanyamapori katika kuchochea maendeleo ya nchi kupitia watalii ambao ulipa fedha na pia fedha hizo, huwarudia wananchi kwa njia ya maendeleo kutokana na miradi mbalimbali ya kijamii inayotekelezwa katika maeneo yao.

"Niwapongeze TAWA, wamefanya kazi kubwa ya kutoa elimu kwa wananchi kipindi hiki cha maadhimisho hapa uwanjani. Elimu niombe hii waipeleke hata shuleni ambako kuna kundi kubwa la wanafunzi ambao wakielimishwa katika umri mdogo watakuwa mabalozi wema wa kusimamia na kulinda rasilimali wanyamapori na kupunguza pia vitendo vya ujangili ambavyo kwa kiwango kikubwa hivi sasa vimepungua kutokana na juhudi zinazofanywa na Serikali na wadau wa utalii," amesema Juma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news