Benki ya NBC yawashukuru Watanzania kwa kuunga mkono Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara

NA THEOBALD SABI

WAKATI Ligi Kuu ya NBC ikikaribia ukingoni, napenda kutoa shukrani za dhati kwa kila mtu aliyewezesha kufanikiwa kwa ligi hii maarufu Afrika na duniani kwa ujumla. 

Mafanikio ya kifedha na yasiyo ya kifedha ambayo ligi kwa pamoja imeyaleta kwenye jamii yetu, hasa kwa wale walio katika mnyororo wa thamani ya soka, yamezidi matarajio yetu ya awali.

Kile kilichoanza kama uamuzi wa kibiashara, kimepelekea kuzaliwa kwa jukwaa la uwezeshaji kwa sekta mtambuka, ambalo limefanikiwa kugusa na kuboresha maisha yetu sote. Leo, tunasimama kifua mbele kujivunia kufanikiwa kwa lengo letu kuu katika uwekezaji huu: Kufungua fursa za maisha.

Kwa niaba ya Bodi na Wafanyakazi wa Benki ya NBC, napenda kutoa shukrani za pekee kwa Serikali ya Tanzania chini ya Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan, kwa kuunga mkono sekta ya mabenki na hivyo kutupa fursa ya kufanya uwekezaji huu, mashabiki kwa shauku yao isiyoyumba, na kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kutuamini na kutukubali kuwa washirika wao. Asanteni sana.
Tunajivunia pia kwa ya hivi karibuni kuongeza thamani katika uwekezaji huo kwa kuongeza kipengele cha utoaji wa bima za afya na maisha kwa wachezaji wa ligi hiyo. Shukrani kwa TFF na washirika wetu wa kampuni za Bima za Sanlam na Britam kwa kuwezesha utoaji wa Bima hizo ambazo pia zitahusisha wafanyakazi wa klabu, na familia zao. 

Ligi Kuu ya NBC ni zaidi ya Soka

Ligi ya NBC sasa imeimarika kutoka mchezo wa dakika tisini na kuwa jukwaa la uwezeshaji wa kijamii na kiuchumi kupitia upatikanaji wa ajira, kuzalisha mapato ya Serikali kupitia kodi, kuendesha ajenda za kitaifa za ujumuishaji wa kiuchumi, na kuongeza miamala na uzalishaji katika mnyororo wa uchumi wa taifa.

Timu 16 zinazoshiriki katika Ligi Kuu ya NBC, zina jukumu muhimu katika maendeleo na ustawi wa jamii zao kiuchumi na kijamii. Biashara mbalimbali katika miji yenye timu hizi huneemeka sana kwa uwepo wa mechi katika miji yao na hivyo kuasaidia sana kuongeza vipato vya familia.

Ligi hii yenye jumla ya michezo 240 iliyoenea nchini kote kuanzia Dar mpaka Geita hadi Mpanda, imekuwa ni msaada mkubwa katika mapato na hivyo kusaidia kwa kiasi kikubwa katika mapambano dhidi ya umaskini.

Ripoti ya hivi karibuni alionyesha kuwa moja ya mechi kubwa kabisa nchini, miaka michache iliyopita iliyohudhiriwa na zaidi ya watu 59,000, iliingiza mapato ya kiasi cha shilingi 545,422,000 na hivyo kuingiza kodi kubwa kwenye kapu la Serikali.

Huu ni mchango mkubwa kwa maendeleo ya Taifa. Pia kuna zaidi ya ajira 3,000 za moja kwa moja kwa wachezaji, waamuzi, wauguzi, na walimu. Ikiwa ukubwa wa wastani wa kaya nchini watu wa tano au zaidi kwa kaya, ligi ya NBC inasimama kama chombo cha kupunguza umaskini, kuboresha ustawi wa kaya, na kuboresha viwango vya maisha.

Mamilioni ya ajira zingine zisizo za moja kwa moja zinaundwa katika minyororo ya uchumi kupitia bidhaa kama chakula, mavazi, malazi, utangazaji, wachuuzi na mengineyo.

Benki ya NBC pia inajivunia kutumia jukwaa hili katika kuunga mkono juhudi za Serikali kusukuma ajenda ya ujumuishaji wananchi katika sekta rasmi ya fedha. Kupitia mechi za ligi hii, tumefanikiwa kukutana na wanachi wengi zaidi kuliko hapo awali. Mpira wa miguu unasimama kama jukwaa muhimu sana katika kuwafikia ambao walikuwa hawajafikiwa na elimu rasmi juu ya masuala ya fedha na uwekezaji.

Ligi Kuu ya NBC pia inajumuisha mchanganyiko wa nyota wa kimataifa na vipaji vya nyumbani. Shirikisho la Soka Afrika (CAF) linaitaja ligi hii kwa kuashika nafasi ya nane bora barani Afrika. Wakati huo huo, klabu za Yanga na Simba zinaongoza kwa kuwa na amshabiki wengi zaidi zaidi Afrika Mashariki na Kati.

Ni wakati wa muafaka sasa kuanza kubadili umaarafu huu nchi za jirani kuwa chanzo cha fedha za kigen na mapato kwa taifa kupitia utalii wa michezo. Ligi Kuu ya Uingereza ilipata dola milioni 602 kutoka kwa mashabiki wa kimataifa wanaosafiri kwenda kwenye michezo.

Uwepo wa majina makubwa ya nyota wa kigeni wanaocheza katika ligi yetu ya NBC, Umaarufu wa ligi yetu kimataifa, ikijumuishwa na mazingira bora ya usafiri na amani nchini, vinaweza kuwa vivutio tosha kuleta watalii wa michezo nchini kutazama mechi zetu kubwa na baadaye kutembelea vivutio vyetu vya utalii.

Theobald Sabi
Mkurugenzi Mtendaji - Benki ya NBC

Post a Comment

0 Comments