BAKWATA Mwanza yahitaji Bilioni 3.5/- kukamilisha vituo vya afya

NA SHEILA KATIKULA

BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) mkoani Mwanza limewaomba wananchi wa maeneo mbalimbali kuchangia ujenzi wa vituo vya afya saba vinavyoendelea kujengwa kwenye wilaya mbalimbali za mkoani huo ambavyo vitagharimu shilingi bilioni 3.5 hadi kukamilika.   Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kutoa taarifa juu ya zoezi la uchangiaji wa ujenzi wa vituo saba vya afya ulipofikia tangu kuanza kwa zoezi hilo Aprili 23, mwaka huu.

Amesema, zoezi la uchangiaji wa vituo hivyo ulianza tarehe hiyo na mpaka hivi kimepatikana kiasi cha sh.milioni 10 kilichotolewa na watu mbalimbali na fedha hizo zimepelekwa kwenye ujenzi wa vituo hivyo.

"Kila kituo cha afya kitagharimu shilingi milioni 180 hadi kikamilike ila kuna kituo kimoja ambacho kinajengwa kwa ghorofa kwenye Wilaya ya Nyamagana kitagharimu sh.bilioni 1.5 hadi kikamilike.

Naye Sheikh wa Wilaya ya Ilemela, Abdulwarith Abdallah amesema,kwenye eneo lake wamefanikiwa kujenga vyumba 21 na kwa sasa wamefikia katika lenta katika kituo cha afya.

Sheikh wa Wilaya ya Sengerema, Ahmad Jaha amesema, ujenzi wa kituo cha afya umefikia kwenye boma kwani wanatarajia kufanya harambee katika misikiti 107 wilayani humo ili waweze kupata fedha za kukamilisha ujenzi huo.

Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Abuu Jadawi inayojishughulisha na tiba za asili, Sheikh Abuu Jadawi amesema, atahakikisha anaandaa kongamano la tiba ili wananchi waweze kuchangia ujenzi huo.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Waislamu Tanzania (JUWAKITA),Amina Masenza amewaomba akina mama wa sehemu mbalimbali kujitokeza kwa wingi kuchangia ujenzi huo ili waweze kupata matibabu wakati wa kujifungua kwani huduma hiyo itakuwa inatolewa na daktari wa wanawake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news