BARABARA YA MVUMI KUWEKWA LAMI KILOMITA TATU

NA ASILA TWAHA, OR-TAMISEMI

NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. David Silinde amesema, Serikali inaendelea kutafuta rasilimali ili barabara ya Mvumi wilayani Chamwino mkoani Dodoma ijengwe kwa kiwango cha lami kwa urefu wa kilomita tatu.
Mhe. Silinde ameyasema hayo Mei 25, 2022 wakati wa ziara yake ya kukagua barabara iliyojengwa kwa kiwango cha lami kilomita moja kuanzia eneo la Makaburini hadi Bilia Kata ya Mvumi Mission Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino jijini Dodoma.

Wakati wa ziara hiyo Mbunge wa Jimbo la Mvumi, Mhe. Livingstone Lusinde aliwasilisha ombi la wananchi wake kutaka kuongezewa barabara ya lami ili kuongeza hadhi ya kata hiyo na kurahisisha shughuli za usafirishaji.
Mhe. Silinde amesema suala hilo litafanyiwa kazi na atahakikisha anasimamia utekelezaji kwa vitendo ili barabara hiyo ipate lami ya kutosha kuipa hadhi Mvumi kuwa mji mdogo.

“Tuendelee kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na kumuunga mkono ili aweze kufanya mambo makubwa zaidi kama mnavyoona kwenye utekelezaji wa miradi na sisi wasimamizi wake tutaendelea kuisimamia kwa vitendo niwahakikishie Mvumi mtaongezewa lami zaidi ya kilomita mbili,"amesema.
Aidha, Mhe. Silinde amesema ameridhishwa na ukaguzi aliofanya katika barabara hiyo kwa kuwa asilimia kubwa umekamilika na amemuelekeza Meneja Wakala wa Barabara za Mjini na Vjijini (TARURA) kuandaa bajeti ya uwekaji wa taa za kwenye barabara hiyo.

“Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa ametuagiza sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI tunapojenga barabara tuweke na taa za barabarani niwaelekeze TARURA hili tutalisimamia,” amesema Mhe. Silinde.
Naye Mbunge wa Jimbo la Mvumi, Mhe. Livingstone Lusinde, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa kuhakikisha wanaisimamia TARURA kwa kutekeleza miradi ya ujenzi wa barabara na ameishukuru Serikali kuridhia ombi la wananchi kuongezewa kilomita za lami.

“Sisi wananchi wa mvumi pamoja na maendeleo tunayo yaona Serikali inayofanya lakini pia tumejiandaa kwa ajili ya zoezi la sensa kuhesabiwa linalotegemewa kuanza nchi nzima mwezi Agosti,2022 na niombe Serikali iendelee kutuunga mkono kuleta maendeleo hapa Mvumi,” amesema Mhe. Lusinde.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news