MAMA SAMIA KATUHESHIMISHA:Ni ujenzi uso' shaka, Kwa mipango 'lopangika

NA DKT.MOHAMED OMARY MAGUO

MEI 25,2022 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amepokea tuzo ya Babacar Ndiaye (2022) kwa mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji.
Tuzo hiyo alipokea katika Mkutano wa 57 wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ambayo hupewa viongozi wa Afrika walio mstari wa mbele katika kuendeleza miundombinu.

Katika hafla hiyo, Rais Samia alitoa wito kwa nchi za Afrika kuungana, kuzijenga na kuziwezesha jumuiya za kiuchumi za kikanda na bara zima kwa ujumla.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akionesha Tuzo ya Babacar Ndiaye kwa mwaka 2022 (Babacar Ndiaye Trophy 2022) kutokana na mafanikio kwenye Ujenzi wa Barabara, mara baada ya kukabidhiwa Tuzo hiyo na Makamu wa Rais wa Sekta Binafsi, Miundombinu na Viwanda katika Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Solomon Quaynor tarehe 25 Mei 20220 Accra nchini Ghana. (Picha na Ikulu).

Mshairi wa Kisasa, Mhadhiri na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Masoko Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dkt. Mohamed Omary Maguo ameandaa utenzi wa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kupata Tuzo ya Mjenzi Bora Afrika ya Babacar Ndiaye kwa mwaka wa 2022. 

Bw.Maguo anasema, tuzo hii ni heshima kubwa kwa Watanzania kwa umahiri wao katika kuchapakazi na kufanikisha maendeleo makubwa katika ujenzi wa taifa ulioifanya nchi yetu kupata tuzo hiyo kubwa barani Afrika. Karibu;

1

Tuzo hiyo Afrika
Samia uliyoshika
Siyo siri ni hakika
Mama 'metuheshimisha

2

Mandeleo tulo'fika
Ni ujenzi uso' shaka
Kwa mipango 'lopangika
Na tuzo ni dhihirisho

3

Duniani kutajika
Ni mtaji 'sopimika
Wekezaji tamiminika
Faida Watanzania


4

Watalii tatiririka
Vivutio kufurika
Wananchi kufaidika
Kwa zao la hiyo tuzo

5

Nyoyo zetu burudika
Nchi yetu kusikika
Ujenzi bora Afrika
Hongera Mama Samia

6

Uchumi kuimarika
Na Corona ingalika
Ni kwako kuchakarika
Samia Rais wetu

7

Nchi yetu kufunguka
Mitaji taongezeka
Ajira zitaoneka
Tuzo iwe chachu kubwa

8

Daima hatutachoka
Kujituma kuwajibika
Nchi yetu kujengeka
Kazi ya Watanzania

9

Hongera sana Samia
Hongera Watanzania
Tuzo hiyo mardhia
Ni heshima kwa taifa

Post a Comment

0 Comments