DC Haule asisitiza umuhimu wa kudumisha ulinzi shirikishi Musoma, awaita vijana mafunzo ya mgambo

NA FRESHA KINASA

MKUU wa Wilaya ya Musoma mkoani Mara, Dkt. Halfan Haule amesema kuwa, kuna haja kubwa kwa Wenyeviti wa Mitaa, watendaji na Madiwani katika Manispaa ya Musoma kuendelea kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yao ili kudhibiti vitendo vya kihalifu ambavyo vimeanza kuibuka.
Dkt. Haule ameyasema hayo Mei 20, 2022 katika kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya tatu cha Manispaa ya Musoma ambapo pamoja na mambo mengine amesisitiza wenyeviti wa mitaa kushiriki kikamilifu katika maeneo yao kuimarisha usalama.

"Wapo baadhi ya vijana wadogo wameanza kujitokeza (panya road) wakifanya udokozi japo si wengi sana, lazima wadhibitiwe kuweka hali shwari katika maeneo yote ya Manispaa ya Musoma kuzidi kuwezesha hali ya usalama na utulivu,"amesema Dkt. Haule.

Aidha, amesema kuwa kutakuwa na mafunzo ya mgambo kwa vijana wa manispaa ya Musoma ambayo yatafanyika katika kata ya Kigera Manispaa ya Musoma,hivyo amewataka vijana kushiriki katika mafunzo hayo kwa ajili ya usalama wa nchi na pia ni fursa kwa vijana katika kujiunga na mafunzo ya vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama pale wanapohitajika wakiwa wamepitia mafunzo hayo.

"Mafunzo ya mgambo ni muhimu kwa ustawi wa nchi yetu, wapo baadhi wamekuwa wakiyapuuza mafunzo hayo lakini ukweli ni kwamba mafunzo hayo ni muhimu sana vijana waliomaliza darasa la saba, kidato cha nne na wengine wote wanakaribishwa sana kushiriki mafunzo haya muhimu ambayo pia yatawajengea uzalendo na ukakamavu,"amesema Dkt. Haule.

Aidha, amesema kuwa, katika Manispaa ya Musoma jumla ya nyumba 37,000. zimehesabiwa na kwamba zinazoendelea kujengwa pia zitahesabiwa. Na pia amewataka Madiwani kuendelea kusisitiza wananchi wajitokeze kushiriki kwa ufanisi katika zoezi la Sensa litakalofanyika mwezi Agosti, 2022.
Kwa upande wake Meya wa Manispaa ya Musoma, William Gumbo amewataka watendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma kuendelea kufanya kazi kwa bidii kuwatumikia wananchi.

Pia, amewahimiza Madiwani wa Manispaa ya Musoma kuhimiza suala la chanjo ya polio kusudi watoto wapate chanjo hiyo kama ambavyo Serikali imekusudia. Akabainisha kwamba watahakikisha wanafikia malengo kwa ufanisi katika ukusanyaji wa mapato kuelekea mwisho wa mwaka wa fedha.

"Kila mtumishi katika sehemu yake afanye kazi kwa bidii na kwa uhakika kuwatumikia wananchi lengo ni kuona wananchi wa manispaa yetu ya Musoma wanazidi kupata maendeleo,"amesema Gumbo.

Mathias Paul ni mkazi wa Kata ya Mukendo Manispaa ya Musoma ambapo amesema vijana wanaojihusisha na uhalifu wanapaswa kuachana na tabia hiyo, badala yake watafute kazi halali za kufanya ziwapatie kipato na waheshimu sheria za nchi.

Neema Amon mkazi wa Iringo amewashauri wazazi na walezi kuendelea kutilia mkazo maadili mema kwa watoto wao sambamba na kuwafundisha mafundisho ya kiroho.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news