Mabalozi:Royal Tour imebeba biashara, utalii na uwekezaji

NA GODFREY NNKO

BALOZI wa Tanzania nchini India, Mhe.Anisa Mbega amesema, wapo katika mazugumzo na watu mashuhuri, wenye ushawishi na maarufu nchini India ili kushiriki kikamilifu kuitangaza filamu ya utalii ya Tanzania The Royal Tour nchini humo.
Mheshimiwa Mbega ameyasema hayo leo Mei 21, 2022 katika Mjadala wa Kitaifa uliorushwa kwa njia ya mtandao wa Zoom chini ya uratibu wa Taasisi ya Watch Tanzania kwa udhamini wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) na mtandao wa simu za mkononi Airtel.

Mjadala huo wa saa mbili na nusu uliangazia mchango wa Filamu ya Tanzania The Royal Tour katika kukuza Diplomasia ya Uchumi.

Balozi Mbega amesema kuwa, wamefikia hatua hiyo, baada ya kubaini kwamba watu wengi wanapenda kuona na kusikiliza kwanza ndio washawishike, hivyo wanatarajia mpango huo ukifanikiwa itakuwa njia moja wapo ya kuwavutia zaidi wawekezaji kutoka nchini humo kuja Tanzania.

"Wengi wanapenda kuona na kusikiliza kwanza ndio washawishike, hivyo kupitia filamu hii ya Royal Topur itakwenda kushawishi watu wengi zaidi, kwani wananchi wa India wanapenda sana kuangalia filamu zao kwenye majumba ya sinema,"amesema.

Pia ameongeza kuwa, wapo katika mkakati wa kuzungumza na viongozi wa majumba ya sinema ili wakati wa mapumziko waweze kuionesha filamu ya Tanzania The Royal Tour.

Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Dkt.Asha-Rose Mtengeti Migiro akizungumzia kuhusu diplomasia ya uchumi amesema, ni dhana ambayo inatutaka kutumia uhusiano wetu wa kidplomasia katika kuchangia na kuleta manufaa ya kiuchumi kwa taifa letu, na maeneo ambayo yatakuwa chachu katika nyanja nyingine za maendeleo.

"Nyenzo kuu tunazotumia hivi sasa ni biashara, utalii na uwekezaji, hiyo ndiyo imekaa katikati ya diplomasia ya uchumi.Lakini, pia tunatumia nyenzo wezeshi ambazo zina mchango mkubwa katika kustawisha diplomasia ya uchumi kwa mfano lugha yetu ya Taifa, sasa hivi yenyewe inatumika kwa kasi sana kuimarisha mahusiano na nchi nyingine na raia wa nchi nyingine.

"Shughuli nyingine za utamaduni, sanaa, michezo na elimu zinatumika kama njia ya kukuza mahusiano. Hizi zinatosheleshana, diplomasia ya uchumi ni pana,japo kila mmoja wetu ana wajibu wa kutumia nafasi yake kustawisha mahusiano ya nchi na nchi.

"Hali ni nzuri sana, tunafahamu katika Serikali zote tangu tumepata uhuru,diplomasia ya uchumi limekuwa eneo muhimu sana, kila awamu ina msisitizo wake na ina manufaa yake,kutokana na jitihada zilizofanywa na marais waliopita kuwa nzuri, awamu hii ya sita mahusiano yamekuwa mazuri zaidi na hii imetokana na ziara mbalimbalia ambazo Mheshimiwa Rais amekuwa akizifanya nje ya nchi zikiwemo nchi jirani,"amesema.

Dkt.Migiro amesema kuwa, filamu ya Tanzania The Royal Tour kwenye diplomasia ya uchumi ina upekee wake mosi ikiwa ni ushiriki wa Rais na pili ni kuona na kuamini kuhusu yaliyomo nchini.

Naye Balozi wa Tanzania nchini China, Mheshimiwa Mbelwa Kairuki amesema kuwa, diplomasia ya uchumi katika Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuimarika zaidi duniani.

Amesema, ndani ya miezi miwili ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alivyoingia madarakani alifanya mazungumzo na Rais wa China kwa nyakati tofauti ili kuimarisha mawasiliano katika biashara na kijamii.

"Hivyo, kutokana na mahusiano mazuri kati ya Tanzania na China, 2021 tuliuza bidhaa za Tanzania zaidi nchini China tofauti na mwaka 2020,"amesema.

Balozi Kairuki amesema kuwa, kupitia jitihada za Rais Samia, Tanzania imekuwa nchi ya kwanza ambayo itapata mikopo, mbegu, vifaa vya kulimia maharageya soya ktoka China na kuyauza nchini humo.

"Kwa sasa China ina fursa ya zao la maharage ya soya, maana wao ndio watumiaji zaidi duniani, wanatumia zaidi ya tani milioni 100 kwa mwaka huku wao wakizalisha tani milioni 15 tu,"amesema.
TAZAMA KWA KINA HAPA

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news