Mama Kevela: Hongera Mheshimiwa Rais Samia kwa Tuzo ya Babacar Ndiaye 2022

NA DIRAMAKINI

MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake (UWT) Mkoa wa Njombe Scholastika Kevela amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupewa Tuzo ya 'Babacar Ndiaye 2022' iliyotokana na mchango wake katika ujenzi wa miundombinu.
Akizungumza leo, Mwenyekiti huyo amesema hatua ya Rais Samia kupewa tuzo hiyo ni muendelezo wa jitihada zake katika kuhakikisha anailetea maendeleo Tanzania suala lililopo ndani ya ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hata hivyo akipokea tuzo hiyo Rais Samia amebainisha kuwa kama kuna mtu aliyestahili tuzo hiyo basi ni Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli akisisitiza kuwa kupatikana kwa tuzo hakutokani na jitihada zake mwenyewe binafsi, bali pia viongozi wengine wa serikali zilizopita hususani Rais Magufuli tangu akiwa Waziri wa Ujenzi hadi
alipokuwa Rais.

Rais Samia alikabidhiwa tuzo hiyo jana jijini Accra nchini Ghana,Tuzo ambayo hutolewa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa kushirikiana na Jarida la Actual Root ikiwa na jina la Babacar Ndiaye ambaye ni Rais wa zamani wa AfDB aliyekuwa kitovu wa masuala ya ujenzi wa miundombinu kuanzia mwaka 1985 hadi 1995.

Aidha, akizungumzia hatua hiyo ya Rais Samia kupokea tuzo hiyo, Mwenyekiti huyo wa UWT Mkoa wa Njombe amesema kuwa suala hilo siyo fahari kwake peke yake bali kwa watanzania wote kwa kuwa wananchi wote wapo nyuma yake kusaidia jitihada zake za ujenzi wa miundombinu na maendeleo kwa ujumla.

"Ukweli Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan anazidi kutuheshimisha, anafanya mambo mengi na makubwa kwa vitendo, tuzo hii ni matokeo ya juhudi hizo katika eneo la ujenzi wa miindombinu, anastahili pongezi zetu za dhati katika hili,"alisema Mama Kevela.

Alisema kwa niaba ya wanawake wote wa Mkoa wa Njombe na watanzania kwa ujumla suala hilo ni faraja kubwa kwao wakiamini kuwa ataendeleza jitihada zake hizo katika kuhakikisha maendeleo ya Tanzania yanazidi kukua kwa Kasi.

Alisema msimamo wao kama UWT Mkoa wa Njombe ni kuwa wataendelea kusimama naye wakati wote wakiamini kuwa hata njia yake kurejea madarakani baada ya uchaguzi wa Mwaka 2025 ni rahisi kwa kuwa ameshawahakikishia watanzania uwezo mkubwa alionao.

Awali akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Rais Samia Suluhu alisema kuwa ni faraja kwake kupatiwa tuzo hiyo ambayo alieleza kuwa Tanzania haikuwahi kuota kuipokea.

Aidha, alizungumzia dhana ya umuhimu wa kuwa na mtangamano wa kiuchumi Afrika hususani kupitia eneo huru la biashara Afrika,akisema anaamini muunganiko wa nchi za Afrika kupitia miundombinu ni chachu ya kulikomboa bara kiuchumi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news