Mwijaku aelea na ndege angani uzinduzi wa Royal Tour Zanzibar

NA DIRAMAKINI

WAKATI Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akizindua filamu maalum ya kuutangaza utalii na fursa za uwekezaji Zanzibar na Tanzania kiujumla, msanii maarufu Mwijaku, ametia fora katika shamrashamra hizo baada ya kuruka na ndege hewani kisha kujiachia mpaka ardhini.
Mchezo huu maarufu kama "Sky dive" umeshuhudia msanii Mwijaku akitumia fursa hiyo kuutangaza utalii wa Zanzibar kama ambavyo malengo ya filamu ya Royal Tour yanaelezea na kufanya kuiona Zanzibar yote kutokea mawinguni.
Huu ni muendelezo wa Uzinduzi wa filamu hii na kila mara msanii Mwijaku amekua akitoa elimu kwa wananchi juu ya faida za filamu hii nyumba kwa nyumba, na hii leo wananchi walipigwa na butwaa kumuona akielea angani mithili ya tai akiielezea Royal Tour kwa nakshi za mavazi na bendera maalum ya filamu hiyo.

Rais azindua

Wakati huo huo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,  Dkt. Hussein Ali Mwinyi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan kwa kuja na wazo la kutayarisha Filamu ya ‘The Royal Tour’ yenye lengo la kuitangaza Tanzania kiutalii Duniani.

Dkt. Mwinyi ametoa shukurani hizo katika uzinduzi wa Filamu hiyo hapa Zanzibar, hafla iliofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip iliopo karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume.

Alisema, madhumuhi ya kutayarisha filamu hiyo ni kuitangaza Tanzania katika nyanja za Utalii, Uwekezaji pamoja na Utamaduni, huku akibainisha Tanznaia kuwa na utajiri mkubwa wa rasilimali ikiwemo maeneo ya fukwe, mbuga za wanyama, maeneo ya urithi (mji mkongwe) na mengineyo na hivyo kutoa fursa ya kuvutia Wawekezaji.

Aidha, aliwataka watendaji Serikalini na sekta binafsi, wadau wa Utalii pamoja na wananchi kwa ujumla kujipanga na kutoa huduma bora ili kukidhi mahitaji kutokana na wimbi kubwa la watalii linalotarajiwa kuzuru hapa nchini kutokana na utayarishaji wa filamu hiyo.

Nae, Mwenyekti wa Kamati ya Maandalizi ya Filamu hiyo, Dkt.Hassan Abass alisema filamu hiyo imeandaliwa na kusimamiwa na mabingwa katika usimamizi wa filamu Duniani.

Mapema, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Sharrif Ali Sharrif alisema utayarishaji wa filamu hiyo ni jambo linalotoa taswira ya kuimarika kwa Muungano wa Tanzania, huku akibainisha jinsi itakavyofanikiwa kuitangaza Tanzania.

Katika hafla hiyo iliohudhuriwa na Viongozi mbali mbali wa Serikali, akiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohamed Gharib Bilali, Makamo wa Pili wa Rais Hemed Sleiman Abdalla pamoja na viongozi mbali mbali, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi alikabidhiwa Tuzo ya uigizaji Bora wa Filamu Tanzania.

Post a Comment

0 Comments