Prof.Mkenda:Kufikia Desemba 2022 Rasimu ya Mitaala mipya na Rasimu ya Mapitio ya Sera itakamilika

NA MATHIAS CANAL-WEST

SERIKALI imesema kuwa ina mpango kabambe wa kukimbiza na kuyafanyia haraka mageuzi ya elimu ambapo kufikia mwezi Disemba 2022 rasimu ya mitaala mipya pamoja na rasimu ya mapitio ya sera itakuwa imekamilika.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof Adolf Mkenda ameyasema hayo leo Mei 18, 2022 ofisini kwake jijini Dodoma wakati alipokutana na kuzungumza na Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Zlatan Milišić.
Waziri Mkenda amemuhakikishia mgeni wake kuwa serikali ya Tanzania imejipanga vyema na kufikia mwezi Januari mwaka 2023 inatarajia kuanza mchakato wa kufanya maamuzi baada ya Rasimu hiyo kuwa imekamilika.

Waziri Mkenda ameeleza kuwa Umoja wa Taifa umeandaa mkutano maalumu unaotarajiwa kufanyika mwezi Septemba mwaka huu Mjini New York nchini Marekani kujadili mageuzi makubwa ya elimu Duniani.
Waziri Mkenda ameeleza kuwa Mkutano wa wakuu wa nchi utaanzisha mchakato katika nchi nyingi Duniani lakini wakati zinaanza mageuzi hayo ya elimu tayari Tanzania itakuwa imefikia hatua nzuri za maamuzi hivyo kwenda mbele kwa haraka zaidi.

Prof.Mkenda amesema kuwa, mchakato huo wa magezi hayo nchini Tanzania umetokana na maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan aliyotoa wakati akilihutubia Bunge la Tanzania tarehe 22 Aprili 2021 kuhusu mabadiliko ya Mitaala ya elimu na muelekeo mpya katika sekta ya elimu aitakayo.

“Na mimi niwahakikishie tu kuwa kupitia Umoja wa Mataifa ni rahisi kujua nchi zingine zinafanya nini kwenye sekta ya elimu ili kuweza kuboresha sekta yetu,”amesema Prof.Mkenda.
Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Zlatan Milišić amemuahidi Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda kuendeleza ushirikiano ili kuhakikisha kuwa malengo ya maboresho kwenye elimu yanatimia ili elimu itolewayo iendelee kuwa bora.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news