Rais Dkt.Mwinyi aibua shangwe kwa wafanyakazi, mishahara ijayo 2022/23 mambo ni safi

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kwa mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali itaongeza mshahara kwa kutumia utaratibu wa kuwapanga watumishi katika madaraja na vyeo kwa mujibu wa miundo ya utumishi kwa kuzingatia elimu zao pamoja na uzoefu wa kazi.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo huko katika viwanja vya Maisara kwenye hotuba yake aliyoitoa ya kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), ambapo kwa Zanzibar sherehe hizi zimefanyika leo, hii ni kufuatia kuwapa wananchi wa Zanzibar muda wa matayarisho ya Sikukuu ya Idd el Fitr.

Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa, ana imani kwamba ongezeko la mishahara litakalofanywa litakuwa na mchango katika kuimarisha uwezo wa watumishi wa umma kujikimu kimaisha pamoja na kuondoa kilio cha muda mrefu kwa watumishi wa umma ambapo elimu na uzoefu wao wa kazi haukuwa ukijitokeza wazi wazi katika marekebisho ya mshahara yaliyofanywa vipindi vilivyopita.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwasili katika viwanja vya Maisara Suleiman kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani iliyofanyika leo 8-5-2022.(Picha na Ikulu).

Hivyo, Rais Dk. Mwinyi amesema kuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetenga shilingi bilioni 12.7 kwa mwezi sawa na shilingi bilioni 153 kwa mwaka kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa zoezi hilo katika mwaka wa fedha wa 2022/2023.

Amesema kuwa, kutokana na utaratibu huo mshahara wa kima cha chini kwa mtumishi aliyeajiriwa mwaka 2019 utapanda kutoka 300,000 hadi kufikia 347,000 ikiwa ni ongezeko la asilimia 15.6.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza katika maadhimisho Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliofanyika katika viwanja vya Maisara Suleiman Unguja Jijini Zanzibar leo 8-5-2022.(Picha na Ikulu).

Ameongeza kuwa vile vile kwa mtumishi wa elimu ya ngazi ya cheti kwa masomo ya sanaa aliyeajiriwa katika mwaka huo huo mshahara wake utapanda kutoka sh. 321,000 hadi kufikia sh. 382,000 ikiwa ni ongezeko la asilimia 19.

Kwa maana hiyo, Rais Dkt. Miwnyi amesema kwamba kila mfanyakazi atapata nyongeza ya mshahara kutegemea na elimu yake pamoja na muda aliofanya kazi ambapo mfano huo ni kwa mfanyakazi mpya hivyo hata ambaye hana cheti lakini amefanya kazi muda mrefu mshahara wake utaongezeka kwa kadri ya muda aliofanyakazi.

Vile vile, Rais Dkt.Mwinyi amesema kuwa katika kuhakikisha kwamba wafanyakazi wanaendelea kuwa na kipato hata wanapopata changamoto ya kupoteza ajira au kupata ajali wakiwa kazini, Serikali kupitia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) imeanzisha Fao la Upotevu wa Ajira na Fao la Kuumia Kazini.

Rais Dkt.Mwinyi amesema kuwa, mafao hayo yataanza kutolewa kuanzia mwaka wa fedha ujao ambapo hivi sasa kazi ya kukamilisha taratibu za kisera na kisheria zinaendelea vizuri na ziko katika hatua za mwinsho kukamilika.

“Kwa mara nyingine nawanahisi watumishi wa umma kwamba, Serikali itaendelea kuimarisha maslahi ya watumishi wa umma kadri ya hali ya uchumi itakavyoruhusu,”amesema Rais Dkt.Mwinyi.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akimkabidhi zawadi Mfanyakazi Bora wa Benki ya Watu wa Zanzibar Bw.Kombo Hamad Kombo.(Picha na Ikulu)

Aidha, Rais Dkt.Mwinyi amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejipanga kuanzisha Bima ya Afya katika mwaka ujao wa fedha ambapo itaanza kwa wafanyakazi wa Serikali kisha yataingizwa makundi mengine lengo ni kuwa na Bima ya Afya kwa wananchi wote wa Zanzibar.

Kwa mujibu wa maelezo ya Rais Dkt. Mwinyi tayari Serikali imelipa jumla ya shilingi Bilioni 1.8 kwa madeni ya wafanyakazi wa Serikali ikiwa ni pamoja na shilingi Bilioni 4.9 za wazabuni.

Rais Dkt. Mwinyi alieleza kwamba katika mwaka wa fedha ujao Serikali itaajiri Watumishi wapya 5,639 katika sekta mbalimbali za Utumishi wa Umma ikiwemo Afya, elimu pamoja na sekta nyingine ili kuweza kutekeleza azma hiyo Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 24.6 katika bajeti ya mwaka ujao kwa ajili ya kugharamia ajira hizo mpya.

Dkt. Mwinyi alikemea tabia ya baadhi ya viongozi ambao alisema wamefilisika kiuongozi kwa kutoa visingizio visivyo vya ukweli katika kuwapa wafanyakazi haki zao kwa kusingizia kwamba wamepewa maagizo na Rais na kusema kwamba kiongozi yeyote atakayetumia lugha hiyo atawajibishwa.

Nae Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji Mudrik Ramadhan Soraga alieleza ofisi yake shughuli zilizofanywa na ofisi yake ikiwa ni pamoja na kuunda Bodi, kutoa elimu na kufanya ukaguzi maalum wa kufuatilia ulipwaji wa kima cha chini cha mshahara kilichotangazwa na Serikali ambapo taasisi 213 zililipa ipasavyo mbapo taasisi 19 hazikutii sheria.

Akitoa salamu zake Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Kanda ya Afrika Mashariki,Bwana Werllingtoa Chibebe alitoa pongezi kwa Rais Dkt. Mwinyi kutokana na mafanikio ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni ambayo Serikali anayoiongoza inaendelea kuyatekeleza sambamba na juhudi zinazoendelea katika kupambana na Uviko-19.

Alisema kuwa ILO inathibitisha uungaji mkono na ushirikiano wake na Serikali, vyama vya wafanyakazi na waajiri pamoja na wadau wengine na kutoa wito kwa wadau wote na kusisitiza haja ya kuunganisha nguvu ili kujenga mazingira ya kazi yanayozingatia haki na utu. 

Mapema akisoma risala ya wafanyakazi kupitia Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Zanzibar (ZATUC), Katibu Mkuu wa Shirikisho hilo Khamis Mwinyi Mohammed aliipongeza Serikali na uongozi wa Awamu ya Nane kwa hamu iliyonayo ya kutaka kuona nchi inapata maendeleo.
KATIBU Mkuu wa Shirikisho la Wafanyakazi Zanzibar Bw.Khamis Mwinyi Mohammed akiwasilisa Salamu za Wafanyakazi wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliofanyika viwanja vya Maisara Suleiman Unguja Jijini Zanzibar leo 8-5-2022.(Picha na Ikulu).

Katika risala yake hiyo Katibu Mkuu huyo alieleza kuwa kima cha chini cha mshahara hivi sasa ni TZS 300,000 kiwango ambacho pia, kinakatwa Kodi na mikato mingine ya kisheria, hivyo basi kinachobaki mkononi hakimkidhi mfanyakazi hata kwa robo ya mwezi.

Hata hivyo, aliwaomba wasaidizi wa Rais kubadilika na wajali thamani ya mazungumzo katika kuhimiza wajibu na maslahi ya wafanyakazi kwa mujibu wa sheria zilizopo na kueleza changamoto wanazokumbana nazo kutoka kwa baadhi ya viongozi wa Serikali.

Alieleza jinsi maslahi ya baadhi ya wafanyakazi katika baadhi ya Wizara yanavyopata changamoto ikiwa ni pamoja na marekebisho yaliyovuruga Kikokotoo cha mafao ya uzeeni ambayo miongoni mwa changamoto zake ni kupungua kwa kiinua mgongo.

Sambamba na hayo, alieleza tabia iliyojengeka kwa watendaji kufanya mambo yasiyofaa kwa kisingizio cha ‘Rais kasema’ ambapo baadhi ya mambo hayo ni kutolipa haki na madai halali ya wafanyakazi pamoja na kuwadhalilisha.

Akitoa neno la ukaribisho Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa alieleza jinsi wananchi walivyofarajika na juhudi za Rais Dk. Mwinyi katika kuwaletea maendeleo endelevu.
MAANDAMANO ya Wafanyakazi kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliofanyika leo katika viwanja vya Maisara Suleiman na kupokelewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) (Picha na Ikulu).

Rais Dk. Mwinyi alitoa zawadi kwa wafanyakazi bora wa mwaka huu pamoja na kutoa vikombe kwa washindi wa mashindano ya mpira wa miguu yaliyofanyika ambapo mapema mara tu baada ya kufika viwanjani hapo aliyapokea maandamano ya wafanyakazi mbali mbali kutoa sekta ya umma na sekta binafsi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

1 Comments

  1. Vipi kwamashilika binafsi hasa yaujenzi watu wanaumiakazini nakisha wanaachishwakazi

    ReplyDelete
Previous Post Next Post

International news