RAIS WETU ASANTE: Tumeona umetenda, nyongeza hiyo asante,Miaka tuliyokonda, tutaisahau yote

NA LWAGA MWAMBANDE (KiMPAB)

HATIMAYE Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametimiza ahadi yake ya kuimarisha maslahi ya wafanyakazi nchini, ikiwa ni siku 13 zimepita tangu atoe ahadi hiyo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Makamu wa Rais Dkt. Philip Isdor Mpango, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Hussein Kattanga, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson, Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamhokya wakiimba wimbo wa mshikamano (solidarity).(Picha na Ikulu).

Ahadi hiyo aliitoa Mei 1, 2022 katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi (Mei Mosi) ambayo Kitaifa yalifanyika katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.

Mheshimiwa Rais siku hiyo, alisema tayari ameagiza kufanyika majadiliano ya kuimarisha maslahi ya wafanyakazi yanayoendelea kati ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA) na Serikali ili kujua kiwango cha maslahi yatakayohitajika.

"Ndugu zangu, jambo letu lipo si kwa kiwango kilichosemwa na TUCTA (Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi) kwa sababu mnajua hali ya uchumi wetu, na hali ya uchumi wa Dunia, hali si nzuri sana na uchumi wetu ulishuka chini sana, yale tuliyofanya mwaka huu, mambo mbalimbali ikiwemo kupunguza kodi, tutaendelea kuyafanya,"amesema Mheshimiwa Rais Samia.

Bw.Lwaga Mwambande ambaye ni mshairi wa kisasa nchini, kwa kuona namna ambavyo Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan anathamini na kuheshimu rasilimali watu kama nguvu kazi muhimu ya kusaidia kufanikisha maendeleo ya Taifa, hivyo kuwatimizia ahadi ya nyongeza ya mishahara anatumia kalamu yake kuwasilisha shairi maalum kwa Mheshimiwa kama ifuatavyo. Karibu;


a:Unasema unatenda, Rais wetu asante,
Tumeona umetenda, nyongeza hiyo asante,
Kima cha chini kupanda, ajira ya umma yote,
Kupandishwa mshahara, hii ni faraja kubwa.

b:Vile tulivyojipinda, kwenye utendaji wote,
Miaka iliyokwenda, bila nyongeza yoyote,
Umetenda tumependa, Mama Samia asante,
Kupandishwa mshahara, hii ni faraja kubwa.

c:Ari mpya umeunda, kwa wafanyakazi wote,
Tija yetu itapanda, katika sekta zote,
Tutafanya utapenda, kwa maendeleo yote,
Kupandishwa mshahara, hii ni faraja kubwa.

d:Lugha yako tunapenda, kumbukumbu zetu zote,
Mwaka jana tulipenda, kwa maneno yako yote,
Mshahara utapanda, mwaka ujao tupate,
Kupandishwa mshahara, hii ni faraja kubwa.

e:Mwaka huu tulipenda, kwa maneno yako yote,
Jambo letu limeshinda, tusherehekee wote,
Julai tunaipenda, ije haraka tupete,
Kupandishwa mshahara, hii ni faraja kubwa.

f:Miaka tuliyokonda, tutaisahau yote,
Mla jana amepinda, posho iliisha yote,
Mla leo ameshinda, salari mpya apate,
Kupandishwa mshahara, hii ni faraja kubwa.

g:La mafao tumependa, hata maagizo yote,
Watumishi watupenda, hayo maamuzi yote,
Na sisi hatutapinda, kuzifanya kazi zote,
Kupandishwa mshahara, hii ni faraja kubwa.

h:Wenye nyumba twawapenda, sisi familia zote,
Mshahara umepanda, ni kidogo siyo wote,
Kodi zisijekupanda, iliwe nyongeza yote,
Kupandishwa mshahara, hii ni faraja kubwa.

j:Watumishi tutapenda, bei zisipande zote,
Hata vita twaviponda, viletavyo shida zote,
Huko Russia tungependa, silaha washushe zote,
Kupandishwa mshahara, hii ni faraja kubwa.

k:Chifu Hangaya kashinda, fupa la miaka yote,
Asemayo twayapenda, kwa wafanyakazi wote,
Anasema anatenda, ni furaha kwetu sote,
Kupandishwa mshahara, hii ni faraja kubwa.

Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Post a Comment

0 Comments