SERIKALI ITAANZA UCHAPISHAJI WA VITABU NCHINI-WAZIRI PROF.MKENDA

NA MATHIAS CANAL

SERIKALI imeitaka Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kuweka mkakati wa ndani ya mwaka mmoja kuhakikisha inapata mashine kubwa ya kuchapa na kutafuta tenda nafuu ya malighafi ya karatasi.
Agizo hilo linakuja wakati ambapo matumizi ya Serikali kwa ajili ya kuchapisha vitabu vya nukta nundu vinavyotumiwa na wanafunzi wasioona na wenye uoni hafifu ikiwa ni Bilioni 15 kwa mwaka.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe Prof. Adolf Mkenda ametoa rai hiyo alipofanya ziara ya kutembelea vituo vya kuchapisha vitabu cha Press A Magogoni na Press B kilichopo shule ya Uhuru Mchanganyiko jijini Dar es Salaam tarehe 15 Mei 2022 na kusisitiza kuwa kiasi hicho kinatokana na malighafi ya karatasi inayotumika kuchapa kununuliwa Dubai na Marekani.
“Dubai ni Jangwani, hakuna miti wakati hawazalishi karatasi, sisi tunaenda kuchapa huko kwa fedha nyingi, nataka na sisi tukanunue malighafi huko wanakonunua wao tuchapishe wenyewe.

“Wafadhili wanaotupatia fedha kwa sasa masharti ni lazima tenda ya kuchapa itangazwe kimataifa, sasa badala sisi tutangaze tenda ya kuchapiwa bora tutangaze tenda ya kupata mashine kubwa ya kisasa hii itapunguza gharama,”amesema. 
Prof.Mkenda amesema kuwa mashine kubwa zaidi ya uchapaji huuzwa shilingi Bilioni 30, hivyo mazungumzo yanapaswa kufanyika na wafadhili ili waweze kufanikisha hilo, kwani wanatekeleza manunuzi ya kimataifa ikiwa ni moja ya sharti la wafadhili hao.

Waziri Mkenda ameongeza kuwa serikali imedhamiria kuimarisha uchapishaji kwa kuiwezesha TET kupata karatasi kwa bei nafuu, umeme wa uhakika na mashine kubwa ya kisasa ya uchapaji kwani kupitia fedha za Mapambano dhidi ya UVICO 19 zilizotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan imewezesha TET kuchapa vitabu vya nukta nundu vyote vya kidato cha kwanza hadi cha sita.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dkt. Aneth Komba amesema taasisi yake imepokea maelekezo ya serikali na inaanza kuyafanyia kazi kwa haraka.

Akielezea sababu za vitabu kutochapishwa nchini ni kutokana na gharama kubwa ya karatasi, kutokuwepo kwa umeme wa uhakika na wa bei nafuu na mitambo ya kutosha kumudu uchapaji kulingana na mahitaji.
Amesema Kiwanda cha uchapaji cha Press A Magogoni ni moja kati ya viwanda saba vya taasisi hiyo na walikabidhiwa na wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia tangu mwaka 2019.

“Kiwanda hiki kinatumika kuchapa muongozo wa walimu darasa la awali hadi la saba na kwa mwaka huchapa vitabu milioni tatu ukihusisha na vya wenye uoni hafifu ambapo hata hivyo mahitaji ya vitabu hivyo yanakidhi ambapo kwa wanafunzi wenye uoni hafifu wanatumia wastani wa vitabu vitatu kwa mwanafunzi mmoja.

Katika kuimarisha ujifunzaji na ufundishaji kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu serikali imeandika na kuchapa nakala 57,756 za vitabu vya Kiada, Kidato cha 1 - 4 vya maandishi yaliyokuzwa kwa masomo ya Biology, Physics, Chemistry, Mathematics, Agriculture, Home Econonics, Kiswahili, Civics, Information and Computer Studies, Geography, History na English.
Aidha, imeandika, kuchapa na kusambaza vitabu vya nuktanundu nakala 9,178 kwa masomo hayo ya sekondari kwa ajili ya wanafunzi 353 wasioona.

Post a Comment

0 Comments