'Viongozi wa dini, mna waumini wengi, tumieni nafasi zenu kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa kuhesabiwa Agosti 23'

NA DIRAMAKINI

AKIZUNGUMZA kwa niaba ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati wa Kutabaruku Kanisa la Bikira Maria wa Fatima Geita tarehe 20,2022, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt.Angeline Mabula amesema, Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi ambazo bila ya kuwa na takwimu sahihi haitaweza kupanga mipango thabiti ya matumizi endelevu ya rasilimali hizo.
‘’Viongozi wa dini mnao waumini wengi tumieni fursa hiyo kuwaelimisha waumini wenu umuhimu wa kuhesabiwa,’’ ilieleza hotuba ya Waziri Mkuu.

Alisema, zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ni muhimu kwa kuwa linaipatia nchi takwimu za msingi zinazotumika kutunga sera, kupanga mipango na program za maendeleo pamoja na kufuatilia utekelezaji wake.

Kupitia hotuba hiyo, Dkt.Mabula alieleza kuwa, takwimu rasmi zitawezesha serikali na wadau wengine kufuatilia na kutathmini malengo yaliyofikiwa katika kutekeleza mipango ya maendeleo iliyokusudiwa sambamba na changamoto mbalimbali zitakazojitokeza katika sekta zote na hatimaye kuweka malengo na mikakati ya kukuza uchumi pamoja na kupunguza umasikini miongoni mwa watanzania

Post a Comment

0 Comments