WABUNGE KUELIMISHWA KUHUSU PURA, WIKI YA NISHATI

NA DIRAMAKINI

WABUNGE na Viongozi mbalimbali wa Serikali wanatarajiwa kuelimishwa kuhusu Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) na shughuli inazozitekeleza kwenye Maonesho ya Majukumu ya Wizara ya Nishati na taasisi zake.
Spika wa Bunge Dkt. Tulia Akson (kushoto) na Waziri wa Nishati January Makamba (kulia) walipotembelea banda la PURA kwenye Maonesho ya Majukumu ya Wizara na Taasisi Zake, yanayoendelea kwenye viwanja vya Bunge, jijini Dar es Salaam.

Maonesho hayo yaliyoanza rasmi Mei 23, 2022 katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma yanaongozwa na kaulimbiu isemayo ‘Nishati kwa Maendeleo Endelevu’ na yatafikia tamati Mei 26, 2022.

Kwa mujibu wa Waziri wa Nishati January Makamba, maonesho hayo yanalenga kujibu maswali ya wabunge juu ya masuala mbalimbali ya sekta ya nishati na kutatua changamoto mbalimbali zinazohusiana na sekta.

Wataalamu wa PURA wamejipanga kuongeza uelewa kwa wabunge hao kwa maeneo mbalimbali ikiwemo ya mradi wa kubadili gesi asilia kuwa kimiminika (LNG), ushiriki wa wazawa kwenye miradi mbalimbali ya sekta ndogo ya mafuta na gesi asilia pamoja na fursa mbalimbali zinazopatikana kwenye utekelezaji wa miradi ya mkondo wa juu wa petroli.
Wajiolojia wa PURA, Ebeneza Mollel (kulia) na Wangese Matiko (katikati) wakitoa elimu kuhusu sekta ya mafuta na gesi asilia kwa moja ya washiriki waliotembelea banda la PURA kwenye Maonesho ya Majukumu ya Wizara na Taasisi Zake, yanayoendelea kwenye viwanja vya Bunge, jijini Dar es Salaam.

Mjiolojia Ebeneza Mollel ameeleza kuwa maonesho haya ni jukwaa muhimu kwa PURA kuwafikia wananchi kupitia viongozi wao kwa kuwaongezea uelewa na namna bora ya kutumia fursa zinazopatikana katika utekelezwaji wa miradi mbalimbali ya mafuta na gesi asilia.

“Viongozi hawa ni kundi muhimu kufahamu fursa hizi kwani wanaweza kufikia wananchi kwa urahisi zaidi ikiwa ni pamoja na kuwasaidia na kuwajengea uwezo wa jinsi ya kuchangamkia fursa hizi,” alieleza.

Naye Mjiolojia Wangese Matiko amebainisha kuwa wabunge watakaotembelea banda la PURA pia watapata fursa ya kujifunza masuala ya kiufundi kama ya mnyororo wa thamani wa mafuta na gesi asilia, shughuli za utafutaji na uzalishaji zinazoendelea nchini na mengineyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news