Wanafunzi 70 Shule ya Sekondari Mkuza wanusurika kifo katika ajali ya moto

NA DIRAMAKINI

ZAIDI ya wanafunzi 70 wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Mkuza iliyopo Kibaha Picha ya Ndege mkoani Pwani wamenusurika kifo.

Shule ya Sekondari ya Wasichana Mkuza inamilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani (DMP).

Tukio hilo linatokana na ajali ya moto iliyotokea usiku huu katika bweni la shule hiyo na kuteketeza mali za wanafunzi hao ikiwemo nguo, madaftari, vitabu na vinginevyo.
Mmoja wa mashuhuda katika eneo hilo, ameieleza DIRAMAKINI BLOG kuwa, ajali hiyo imetokea wakati wanafunzi wakiwa katika ibada.

"Ukimtumainia Mungu, hakuna lisilowezekana, hakuna mwanafunzi aliyepata ajali ukizingatia moto ulikuwa mkali sana, kwa sababu walikuwa ibadani, ni jambo la kumshukuru Mungu sana,"amesema shuhuda huyo.

Mheshimiwa Abubakar Kunenge ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani amefika shuleni hapa.

Kunenge amewataka wazazi kuwa na amani kwani, hakuna mtoto aliyedhurika na wote wapo salama.

Naye Kamanda wa Zimamoto mkoani hapa, Jenipher Shirima amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Kamanda Shirima amewaomba wananchi kuendelea kuwa mstari wa mbele kutoa taarifa kuhusu ajali za moto ili iwe rahisi kuudhibiti kabla ya kuleta madhara.

Kwa upande wake, Dkt. Alex Malasusa ameushukuru uongozi wa Mkoa wa Pwani pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kwa ushirikiano wao.

Shule hiyo inaendeshwa chini ya dawati la wanawake wa dayosisi hiyo ambao ndio hasa wanaoisimamia tangu kuanzishwa kwake zaidi ya miaka 10 iliyopita.

Aidha, pamoja na kuwa shule hiyo ni ya pekee ya wasichana katika dayosisi hiyo imekuwa ikifanya vizuri mwaka hadi mwaka na kuweka historia ya kutokuwa na daraja sifuri.

Kwa sasa timu MAALUM inaendelea na uchunguzi Ili kuweza kufahamu chanzo cha ajali hiyo ya moto.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news