WAZIRI MKUU: WANAOTOA ARDHI WALIPWE FIDIA

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ihakikishe Watanzania wanaotoa ardhi yao waliyomilikishwa kihalali kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kimaendeleo ikiwemo uwekezaji wanalipwa fidia zao kwa wakati.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akijibu maswali ya bungeni jijini Dodoma, Mei 26, 2022.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Amesema hayo leo (Alhamisi, Mei 26, 2022) wakati akijibu swali la Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu. Mbunge huyo alitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha wananchi ambao maeneo yao yamechukuliwa na wawekezaji wanalipwa fidia.

Amesema ni muhimu kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuendelea kusimamia ulipwaji wa fidia kwa wananchi waliotoa ardhi zao kwa shughuli za kimaendeleo. ”Nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama kuna madai yametolewa na hasa kama uthamini umefanyika basi thamani ya ile ardhi iliyochukuliwa kwa ajili ya kupisha shughuli nyingine ni lazima fidia ilipwe ili haki itendeke".

Akijibu Swali ya Mbunge wa Moshi Mjini, Priscus Tarimo aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kupima maeneo ya Miji, Manispaa na Jiji, Waziri Mkuu amesema kuwa mpango huo ni endelevu wenye lengo la kupima maeneo yote nchini ili kubainisha huduma zote zinazotakiwa kutumika katika ardhi hiyo.

Mheshimiwa Majaliwa ameongeza kuwa mpango huo utakwenda hadi maeneo ya vijijini ili kuwasiaidia kupata maeneo yaliyopimwa na kutambulika rasmi ili waweze kupata hati. “Tunataka watumie hati hizi kama mtaji wa kukopea kwenye taasisi zetu za fedha, lengo ni kila Mtanzania anufaike na ardhi iliyopo, hivyo Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi iendelee kukamilisha zoezi hili, hii itawasaidia hata wawekezaji kutambua maeneo ya uwekezaji”

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali imeendelea kuhamasisha wakulima wadogo wa chikichi waendelee kulima kwa wingi zao hilo lengo likiwa ni kuhakikisha nchi inazalisha kwa wingi mafuta ya kula.

Pia, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza kwenye kilimo hicho kwa kuwa nchi ina ardhi ya kutosha na yenye rutuba. “Ardhi tunayo, na tumeshatoa maagizo kwa wakuu wa mikoa wote kutenga ardhi kwa ajili ya uwekezaji”.

“Tunataka tuzalishe na tukamue mafuta yetu sisi wenyewe, tunaamini gharama itakuwa ndogo na zile fedha tunazotumia kuagiza mafuta nje hazitakwenda tena bali tutaziingiza kwenye shughuli nyingine za kimaendeleo, uwekezaji huu ni mkubwa na endelevu".

Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Kigoma Kaskazini Assa Makanika ambaye alitaka kujua mkakati wa Serikali wa kuwakaribisha wawezaji wakubwa ili kupunguza Nakisi ya kuagiza mafuta ya kula nchini.

Mheshimiwa Majaliwa aliongeza kuwa, Serikali imeweka mkakati wa kuhakikisha inaimarisha teknolojia inayotumika katika kukamua mafuta ya chikichi “Sasa tunakwenda kuimairisha viwanda vya ukamuaji ili tuweze kukamua asilimia 99 ya mafuta kwenye chikichi badala ya 70 ya sasa”.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news