'WIZARA, BRELA, BPRA LINDENI KAZI ZA WABUNIFU'

NA MWANDISHI WETU

MAKAMU wa Kwanza wa Rais–Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman ametoa Wito kwa Wizara zinazosimamia masuala ya ubunifu pamoja na taasisi zikiwemo Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) na Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali (BPRA) ya Zanzibar, kuhakikisha kuwa zina andaa mikakati maalumu ya kulinda kazi mbalimbali za wabunifu.
Mhe Othman ametoa agizo hilo tarehe 16 Mei, 2022 wakati wa ufunguzi wa Wiki ya Kitaifa ya Ubunifu (MAKISATU) inayoambatana na maonesho ya Wabunifu, katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.

Amesema kuwa, nchi mbalimbali zimepata maendeleo makubwa kwasababu ya kuwa na mikakati madhubuti ya kulinda kazi za wabunifu, kwa hivyo ni vema kuwasaidia wabunifu na lazima kuwa na mikakati ya kuwasaidia, kujua ni namna gani na hatua gani za kulinda kazi hizo.
“Siku hizi vitu vingi vinafanyika kwa udanganyifu na ujanja mkubwa umekuwa ni wa kuchukua kazi za wengine, hivyo tunapaswa kuwa na mikakati ya kulinda kazi za wabunifu,” amefafanua Mhe. Othman.

Mhe. Othman amefafanua kuwa, kazi za ubunifu zisipolindwa zitakuwa hazina maana, na hii itawafanya wavuje jasho lakini bila kuwa na tija inayotokana na jasho lao, hivyo kuna haja ya kutilia mkazo suala hili kwa kuweka mikakati madhubiti.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Miliki Bunifu Bw. Seka Kasera ameeleza kuwa, kama kaulimbiu inavyo sema, “Ubunifu kwa Maendeleo Endelevu,”amewataka wabunifu waliosajiliwa kuendeleza bunifu zao kwa kuziboresha kulingana na mahitaji ya jamii.

“Katika maonesho haya nimetembelea mabanda ya wabunifu na kuziona bunifu nyingi ambazo zinahitaji kuendelezwa kwa kuziboresha zaidi badala ya kuziacha kama zilivyo,” alifafanua Bw. Kasera.

Akirejea kauli ya Mgeni rasmi kuwa tangu mwaka 2019 China ndio nchi inayoongoza kwa kutoa bunifu nyingi na inaongoza kwa kutoa bunifu endelevu kwakuwa wamekuwa wakiziongezea ubora mara kwa mara kulingana na mahitaji ya jamii.

Bw. Seka amewashauri wabunifu ambao bunifu zao bado hazijapata ulinzi lakini zina sifa ya kupata ulinzi, kuwasiliana na BRELA kwa ajili ya kupata ulinzi juu ya uvumbuzi walioufanya. .

BRELA imekuwa ikitoa elimu ya namna ya kuboresha bunifu zile ambazo zimesajiliwa na kuziendeleza na kuangalia jinsi ya kushirikiana na taasisi nyingine za kikanda na kimataifa kuwasaidia kuzipatia masoko.

Maonesho haya ya wiki ya MAKISATU yaliyoanza tarehe 15 Mei, 2022 yatahitimishwa tarehe 20 Mei, 2022.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news