BASHUNGWA AUNGANA NA MAWAZIRI KUPOKEA KAYA ZILIZOWASILI MSOMERA KUTOKEA HIFADHI YA NGORONGORO

NA OR-TAMISEMI 

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa ameungana na Waziri wa Maliasili na Utalii na Utalii, Mhe. Balozi Dkt Pindi Chana, Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Ridhiwan Kikwete kupokea jumla ya kaya 20 kati ya 290 zilizowasili Msomera, Wilaya ya Handeni Mkoa wa Tanga zilizoamua kuondoka kwa hiyari katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro mkoani Arusha.
Kaya hizo zimewasili leo Juni 16,2022 kwa kusafirishwa na Serikali ikiwa ni awamu ya kwanza na kuanza makazi mapya katika eneo la Msomera ili kupisha shughuli za uhifadhi katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.

Waziri Bashungwa amesema, tayari Serikali imeweka mazingira mazuri kwa ajili yao ambapo Serikali ilileta shilingi Milioni 400 kujenga shule mpya za msingi na sekondari na bweni moja katika Kata ya Misima ndani ya Kijiji cha Msomera ambazo zimekamilika ili wanafunzi wasitembee mwendo mrefu kupata masomo ya elimu ya msingi na sekondari.
Amesema, tayari Serikali imetoa shilingi Milioni 500 kuanza ujenzi wa kituo cha afya Msomera ambao unaendelea na shilingi Milioni 50 kwa ajili ya kupanua na kuboresha huduma za afya katika zahanati ya Kijiji cha Msomera katika kata ya Misima Wilaya ya Handeni Mkoa wa Tanga kinachotoa huduma kwa wananchi wasiopungua 10,000.

Amesema, Serikali kupitia Ofisi ya Rais - TAMISEMI itaongeza watumishi ambao ni wauguzi, wataalam wa maabara na madawa ili ukarabati unaofanyika katika zahanati ya Msomera uendane na huduma nzuri zinazoendelea kutolewa hapo.

Vile vile, amesema TARURA wanaendelea wa barabara inayotoka Handeni Mjini hadi Kata ya Misima kwa kujenga makalavati na boksi kalvati katika maeneo korofi.

Pia, amemuagiza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais - TAMISEMI kuleta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa madarasa ya wanafunzi wa awali ili yaweze kuwahudumia watoto wadogo walio katika eneo la Msomera.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news