DCEA:Tupeni taarifa sahihi kuhusu dawa za kulevya, tutawatunzia siri

NA GODFREY NNKO

KAMISHNA Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA), Bw. Gerald Musabila Kusaya amesema kuwa, mtu yeyote ambaye ana taarifa sahihi kuhusu mtu, kikundi kinachojihusisha na uhalifu wowote ikiwemo dawa za kulevya awasiliane na mamlaka, kwani mbali ya kumtunzia siri pia watampa zawadi. 
Ametoa rai hiyo leo Juni 30,2022 wakati akitoa ufafanuzi kuhusu dawa za kulevya, hali ya matumizi ya dawa za kulevya kupitia Kipindi cha Clouds360 kinachorushwa na runinga ya Clouds jijini Dar es Salaam. 

Kusaya amesema, hawawezi kufanya kazi peke yao badala yake wananchi ndio wanawapatia taarifa na ameomba waendelee kufanya hivyo ili kuiweka Tanzania salama bila dawa za kulevya na uhalifu.

"Nawaambia wananchi waendelee kutupatia taarifa na sio tu za dawa za kulevya za uhalifu wowote na taarifa zitabaki kuwa siri.Kama hawana imani na watu wengine waje kwangu (Kamishna Jenerali Kusaya) moja kwa moja na hata kama yupo nje ya mkoa aje nitamlipia nauli, lakini aje na taarifa sahihi na kuna zawadi tutampatia. 

"Aje na taarifa ya kweli sio ya majungu au amesikia anatembea na mke wake amsingizie anauza dawa za kulevya hapana, tutakugeuka. Mwenye taarifa ya ukweli apige namba 119 (bure)."amesema Kamishna Jenerali Kusaya.

Jela inakuhusu

Wakati huo huo,Kamishna Jenerali Kusaya amesema kuwa, ukikamatwa na dawa za kulevya nchini ujue jela maisha inakuhusu.

"Mwanzoni tulikuwa na Tume ya Dawa za Kulevya haikuwa na meno ilikuwa ikiratibu zaidi, lakini baada ya kuundwa kwa mamlaka kamili ya udhibiti wa dawa za kulevya sasa tuna mamlaka ya kukamata. 

"Pia adhabu zimeongezeka na kuna uzito ukifika sehemu hukumu yake lazima ianzie miaka 20 hadi 30 na kifungo cha maisha jela. Yote hii imekusudia ili kukomesha dawa hizi za kulevya nchini,"amesema Kamishna Jenerali Kusaya.

Doria popote

Kamishna Jenerali Kusaya amesema kuwa, wao kama mamlaka kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama wanafanya operesheni na doria mbalimbali kuanzia nchi kavu hadi majini.

"Kuna njia kuu mbili za kuingiza dawa za kulevya nchini,kwa kutumia viwanja vya ndege pamoja na bahari. Kwa upande wa viwanja vya ndege tupo vizuri kabisa kwa sababu tunatumia vifaa na watu wapo, eneo la pili ambalo tuna changamoto kubwa ni njia ya bahari kwa sababu,ukanda wa bahari ni mkubwa sana, lakini kote huko tunafanya kazi ili kuhakikisha dawa za kulevya haziingii nchini,"amesema.

Amesema, dawa za kulevya zikiendelea kutumika nchini hata kizazi kitapotea ndio maana wanakuwa wakali zaidi. 

"Na sisi tunataka kizazi kiendelee inafika sehemu mtu alivyoathirika na dawa za kulevya hawezi kubeba hata mkate anasema ni mzito. Hiyo ni hatari, kama hawezi kubeba mkate ataweza kubeba SMG kwenda vitani?," amehoji Kamishna Jenerali Kusaya.

Kuhusu DCEA

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ilianzishwa chini ya kifungu cha 3 cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015. Sheria hii iliifuta Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya. Kuanzishwa kwa Mamlaka Kulitokana na mapungufu yaliyokuwepo katika mfumo wa udhibiti wa dawa za kulevya.

Mapungufu hayo yalikuwa ni pamoja na Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya iliyoanzishwa na Sheria ya ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Namba 9 ya mwaka 1995 kukosa nguvu ya kisheria ya kupeleleza, kufanya uchunguzi na kukamata wahalifu wa dawa za kulevya.

Kutokana na mapungufu hayo, Baraza la Mawaziri katika kikao chake cha tarehe 8 Novemba, 2007 (Waraka Na 60/2007) liliagiza, kurekebisha au kufuta Sheria ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Namba 9 ya mwaka 1995, ili kukidhi matakwa na changamoto za udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya. 

Baraza la Mawaziri liliagiza kuundwa kwa chombo cha kupambana na dawa za kulevya chenye uwezo kiutendaji kwa kukipa mamlaka ya ukamataji, upekuzi na upelelezi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola ili kuongeza ufanisi wa udhibiti wa dawa za kulevya nchini.

Kufuatia agizo hilo, tarehe 24/03/2015 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga na kupitisha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015 na kuanza kutumika rasmi tarehe 15 Septemba, 2015 kupitia tangazo la Serikali namba 407 (GN NO.407/2015).

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ilianza kutekeleza majukumu yake kikamilifu Februari 17, 2017 baada Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kumteua Kamishna Jenerali.

Kuhusu bangi

Kamishna Jenerali Kusaya akizungumzia kuhusu bangi anasema kuwa, "Sisi ni Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya tunasimamia sheria yetu mama inayozuia kwamba bangi hairuhisiwi na ni zao haramu. 

"Kwa hiyo kwenye hizo nchi zingine zinazoruhusu bangi na sisi turuhusu sio kazi yetu. Sisi tunasubiri amri tu hii imekuwa sheria au sio sheria sisi tunaendelea. Wanasayansi wameshafanya utafiti kuhusu madhara ya dawa za kulevya leo uniambie bangi iruhusiwe kutumika siwezi kuruhusu hata mara moja, kwa sababu najua madhara ya dawa hizi. 

"Bangi ni mbaya inaharibu akili, inaleta kansa ya koo, ya mapafu inaharibu via vya uzazi.Dawa zinaingia zaidi jijini Dar es Salaam kuliko mikoa mingine vigezo ni vingi, sio tu dawa kuingia wengine wanaingia kwenye matumizi ya dawa hizi kwa ushawishi na ushawishi unafanyika zaidi kwa watu wa mjini,"amesema.

DCEA wanafanya nini

Majukumu ya Mamlaka ni kufafanua, kuhamasisha, kuratibu na kutekeleza hatua zote zinazoelekezwa katika udhibiti wa dawa za kulevya. Katika kutekeleza majukumu hayo Mamlaka inafanya kazi zifuatazo:

i.Kusimamia utekelezaji wa mikataba ya kimataifa, maazimio na makubaliano katika kudhibiti dawa za kulevya.

ii.Kuandaa na kutekeleza mpango wa Taifa wa kudhibiti dawa za kulevya.

iii.Kutengeneza miongozo inayoelezea tatizo la dawa za kulevya na madhara yake katika jamii;

iv.Kuboresha na kurekebisha sheria na kanuni za udhibiti wa dawa za kulevya;

v.Kuhamasisha udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya ikiwemo kutoa elimu juu ya madhara ya dawa za kulevya, kusambaza taarifa kwa umma na juhudi nyingine za udhibiti;

vi.Kuchukua hatua stahiki za kupambana na biashara ya dawa za kulevya zikiwemo kukamata, kupekua na uchunguzi wa masuala yanayohusiana na dawa za kulevya.

vii.Kuzuia, kupeleleza na kuchunguza uchepushaji wa dawa za tiba zenye madhara ya kulevya pamoja na kemikali zilizosajiliwa kutoka kwenye vyanzo halali wakati huo huo kuhakikisha dawa hizo zinapatikana kwa matumizi ya tiba, biashara na mahitaji ya kisayansi;

viii.Kuanzisha mfumo thabiti wa ukusanyaji taarifa na uchambuzi katika ngazi ya taifa kuhusu matumizi na biashara ya dawa za kulevya;

ix.Kuhamasisha, kuratibu na kuhakikisha jitihada za ushirikiano wa kimataifa katika kudhibiti wa dawa za kulevya zinaimarishwa;

x.Kufanya, kuwezesha na kuratibu tafiti zinazohusiana na dawa za kulevya;

xi.Kuratibu na kuwezesha wadau wanaojihusisha na udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya;

xii.Kuelimisha na kuhamasisha jamii kushiriki katika mapambano dhidi ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya;

xiii.Kutoa mafunzo kwa watendaji wanaojihusisha na udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya, fedha haramu na kemikali bashirifu.

xiv.Kufanya uchunguzi wa sayansi jinai

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news