EPUKENI KUFANYA KAZI KWA MAZOEA-JAJI MAMBI

NA INNOCENT KANSHA-Mahakama

JAJI wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma Mhe. Dkt. Adam Mambi amewataka Wahasibu na Wakaguzi wa Ndani kutumia mafunzo waliyoyapata kuongeza kasi ya uwajibikaji na kuepuka kufanya kazi kwa mazoea ikiwa ni pamoja na kupunguza urasimu usio wa lazima katika kutoa huduma kwa wananchi na watumishi.
Sehemu ya washiriki wa mafunzo hayo wakifuatilia hotuba ya Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma Mhe. Dkt. Adam Mambi (hayupo pichani) wakati wa ufungaji mafunzo hayo.

Akifunga mafunzo ya kundi la tatu la washiriki hao yaliyofanyika kwa siku tano tarehe 17 Juni, 2022 katika Ukumbi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki jijini Dodoma, Mhe. Dkt. Mambi alisema, Mahakama inategemea kupitia mafunzo hayo yatawaongezea ufanisi na weledi katika ukusanyaji wa maduhuli, kufanya malipo kupitia mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), kusimamia matumizi bora ya fedha na rasilimali za Serikali kwa ujumla.

“Tukatumie mafunzo haya kwa kuwa waadilifu, kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza utumishi wetu na pengine mkawe watoa elimu hii kwa watumishi wengine kila fursa ya kufanya hivyo inapopatikana”, alisisitiza Jaji Mambi.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma Mhe. Dkt. Adam Mambi (aliyesimama) akifunga mafunzo ya Wahasibu na Wakaguzi wa Ndani kundi la tatu (hawapo pichani) yaliyofanyika kwa siku tano tarehe 17 Juni, 2022 katika Ukumbi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki jijini Dodoma. Wengine ni Naibu Msajili Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Bernard Mpepo (kulia) na Afisa Utumishi Mahakama ya Tanzania, Kitengo cha Mafunzo Bw. Rajabu Singana.

Hivyo kwenu, ni wajibu na dhamana mliyokabidhiwa kufanya kazi mlizojifunza kwa nidhamu ili kutatua changamoto zilizopo na kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu na kutumia mfumo wa TEHAMA katika kazi, kuzingatia uadilifu, kulinda usalama wa fedha na matumizi sahihi ya mitandao.

“Washiriki wa mafunzo mkiwa kama wasaidizi wa Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika kusimamia matumizi bora ya fedha, naamini mafunzo haya yatawasaidia sana katika kutekeleza majukumu yenu na kurahisisha kazi ya Ofisi ya CAG”, Jaji Mambi aliongeza.
Sehemu ya washiriki wa mafunzo hayo wakifuatilia kwa makini hotuba ya Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma Mhe. Dkt. Adam Mambi (hayupo pichani) wakati wa ufungaji mafunzo hayo.

Dkt. Mambi akawakumbusha washiriki hao mambo ya msingi ya kuyazingatia ambayo ni uadilifu, weledi na kuongeza bidii katika kazi ikiwa ni pamoja na kutumia vipawa vyao kubuni njia sahihi za kutatua changamoto. Ushirikianao kama timu na nidhamu ya dhati katika utekelezaji wa majukumu wakiongozwa na uzalendo na uchamungu.

Jaji Mambi alisema, mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa sheria ya miamala ya kielektroniki ya mwaka 2015 pamoja na sheria ya Serikali mtandaoya 2019. Sheria zote mbili zinaruhusu malipo kufanyika kupitia mtandao (e-payment) na usimamizi wa fedha kupitia mtandao (e-auditing).
Sehemu ya washiriki wa mafunzo hayo wakifuatilia hotuba ya Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma Mhe. Dkt. Adam Mambi (hayupo pichani) wakati wa ufungaji mafunzo hayo.

Sheria hizi zinatoa mamlaka ya kufanya malipo na kusimamia fedha kwa kutumia mfumo wa TEHAMA. Mathalani vifungu vya 13, 14, na 15 vya sheria inayosimamia miamala ya kielektroniki ya mwaka 2015, vinaruhusu malipo ya fedha kufanyika kwa njia ya mtandao kama sehemu ya utekelezaji wa Serikali mtandao. Vilevile vifungu vya 31, 35, na 64 vinatambua na kuruhusu malipo na usimamizi wa fedha kufanyika kwa njia ya kielektroniki au mtandao, aliongeza Jaji Mambi.
Sehemu ya washiriki wa mafunzo hayo wakifuatilia hotuba ya Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma Mhe. Dkt. Adam Mambi (hayupo pichani) wakati wa ufungaji mafunzo hayo.(Picha na Innocent Kansha-Mahakama).

Aidha, Dkt. Mambi alisema mafunzo hayo yalijikita katika kuongeza uzoefu wa namna bora ya kutumia TEHAMA katika masuala mazima ya fedha kama vile kufanya malipo, kupokea au kukusanya fedha kwa njia ya mtandao na kufanya ukaguzi kwa kwa njia hiyo.

Kwa upande wa Mpango Mkakati wa Mahakama awamu ya pili, Jaji Mambi aliwakumbusha washiriki kuwa mafunzo hayo yameutafsiri mpango huo kwa vitendo katika kuhakikisha usimamizi na utoaji wa huduma ya haki inayomlenga mwananchi anayehudumiwa inaendelea kwa kasi na yenye kufuata misingi ya uadilifu, uwajibikaji, weledi bila kusahau uzalendo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news