Maagizo 10 ya Waziri Bashungwa kwa waajiri na waajiriwa wapya leo

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI),Innocent L. Bashungwa (Mb) ametoa maelekezo ya msingi mbalimbali yanayopaswa kuzingatiwa na waajiriwa na waajiri nchini.

Maelekezo hayo yanakuja baada ya kutangaza majina 16,676 ya watumishi wapya waliopangiwa vituo vya kazi katika Sekta ya Elimu na Afya nchini.

Orodha hiyo inatokana na waombaji wenye sifa waliokidhi vigezo baada ya Aprili, 2022 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kutoa kibali cha ajira kwa kada za Ualimu na Afya, kwa ajili ya kuajiri walimu 9,800 wa shule za msingi na sekondari na wataalam wa afya 7,612.

Mheshimiwa Innocent Bashungwa amesema, baada ya kupata kibali cha ajira, Ofisi ya Rais-TAMISEMI ilitoa tangazo kwa wahitimu mbalimbali wa Ualimu na Kada za Afya, kuwasilisha maombi ya kazi, kupitia mfumo wa kielektroniki wa kupokea na kuchakata maombi ya ajira, kuanzia Aprili 20 hadi Mei 8,2022.

Mheshimiwa Bashungwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo Juni 26, 2022 amesema, jumla ya maombi 165,948 yakiwemo ya wanawake 70,780 na wanaume 95,168 yaliyopokelewa kwenye mfumo, ambapo maombi ya kada za afya ni 42,558, na kada ya Ualimu ni 123,390.

Amesema, kwa upande wa kada za ualimu,waombaji wenye sifa waliokidhi vigezo na kupangiwa vituo vya kazi ni 9,800 ambapo jumla ya walimu 5,000 wamepangwa shule za msingi na walimu 4,800 Shule za sekondari, wakiwemo walimu wenye ulemavu wa shule za msingi na sekondari 261.

Waziri Bashungwa amesema, kwa upande wa kada za Afya,waombaji wenye sifa waliokidhi vigezo na kupangiwa vituo vya kazi ni 6,876 wanawake ni 3,217 sawa na asilimia 46.8 na wanaume ni 3,659 sawa na asilimia 53.2 wakiwemo wenye ulemavu 42 sawa na asilimia 0.61.

Maelekezo ya Waziri

a."Waajiriwa wapya wote wahakikishe wanaripoti kwa wakurugenzi wa halmashauri walizopangiwa wakiwa na Kitambulisho cha Taifa au namba ya utambulisho ya NIDA,cheti halisi cha kuzaliwa,vyeti halisi vyote vya Taaluma na Utaalamu wa Kazi vya mwajiriwa, ili vihakikiwe na mwajiri kabla ya kupewa barua ya ajira;

b:Waajiri wote wahakikishe wanapokea vyeti na kuviwasilisha baraza la mitihani kwa ajili ya uhakiki. Wizara ipewe taarifa mara moja kwa wale watakaokutwa na vyeti ambavyo ni vya kugushi ili hatua kali zichukuliwe;

c. Waajiri wote wahakikishe watumishi wapya waliopangwa kwenye halmashauri, wanapewa barua za ajira, na kuripoti kwenye vituo walivyopangiwa tu, na si vinginevyo;

d. Mwajiriwa mpya atakayechukua posho ya kujikimu, na baadaye asiripoti katika kituo chake cha kazi alichopangiwa, atachukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria;

e. Waajiriwa wapya ambao hawataripoti katika vituo walivyopangiwa ndani ya siku 14, kuanzia tarehe
ya tangazo hili, watakuwa wamepoteza nafasi zao ambazo zitajazwa na waombaji wengine wenye sifa, waliopo kwenye Kanzidata (Database) ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI;

f. Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa ambazo Waajiriwa wapya wamepangwa, wahakikishe wanawapokea Waajiriwa wapya na kuwawezesha kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma, na
baadaye kutoa taarifa ya kuripoti kwao.

Taarifa za kuripoti waajiriwa hao zijazwe kwenye mfumo wa kielektroniki (ajira.tamisemi.go.tz), baada ya kila
mtumishi kupokelewa na kukamilisha taratibu;

g. Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wanaelekezwa kukamilisha taratibu za ajira haraka, ili waajiriwa wapya waingizwe kwenye mfumo wa taarifa za kiutumishi na mishahara (HCMIS) mapema iwezekanavyo;

h. Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi wote wa Halmashauri, kuhakikisha wanatekeleza maagizo ya OR-TAMISEMI yaliyotolewa kwenu Mwezi Machi, 2022, ya kuhakikisha mnafanya msawazo wa IKAMA ya walimu wa Shule za Msingi na Sekondari, ndani ya Mkoa na Halmasgauri kabla au ifikapo tarehe 30 Juni, 2022.

Tekelezeni kwa bidii maelekezo hayo ili kuhakikisha shule zinakuwa na uwiano mzuri wa walimu, na taarifa
ya utekelezaji iwasilishwe kabla au ifikapo tarehe 15 Julai, 2022. OR-TAMISEMI haitasita kumchukulia hatua Mwajiri ambaye hatatekeleza maelekezo haya ya kufanya msawazo wa walimu katika kuleta uwiano wa mwalimu, na wanafunzi wa 1:60 ulioelekezwa.

i. Tunawaelekeza Wakuu wa Shule na Walimu Wakuu kushirikiana na Bodi zao za shule ili kufuata miongiozo ambayo Wizara imetoa kwa ajili ya michango ya wanafunzi wanaoendelea na masomo.

Hatua kali zitachukuliwa kwa Mkuu wa Shule au Mwalimu Mkuu yeyote ambaye ataenda kuinyume na miongozo iliyotolewa na Serikali; na

j. Walimu waliopo kazini na Waajiriwa wapya, kuhakikisha wanafundisha wanafunzi kwa weledi, na bidii ya hali ya juu kwa kuzingatia kalenda ya ufundishaji iliyopo.

Wakuu wa Shule, Waratibu Elimu Kata, Maafisa Elimu wa Halmashauri na Mikoa yote nchini kufuatilia ufundishaji wa kila siku darasani, na kujiridhisha kuwa wanafunzi wanapata umahiri unaotarajiwa kwenye ngazi mbalimbali za elimu ya Msingi na Sekondari.

Aidha, Watumishi wote wa kada za Afya nchini, wanaoendelea na utumishi, na walioajiriwa wapya, kuhakikisha wanawahudumia wananchi kwa weledi na upendo wa hali ya juu, kwa kuzingatia Sheria, kanuni na miongozo ya utoaji bora wa huduma za afya nchini,"amefafanua kwa kina Mheshimiwa Waziri Bashungwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news