Nafasi 736 za ajira kutangazwa upya baada ya kukosekana waombaji wenye sifa

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mheshimiwa Innocent Bashungwa amesema nafasi 736 kada za afya zimekosa waombaji wenye sifa.

Ameyasema hayo wakati akitangaza majina 16,676 ya watumishi wapya waliopangiwa vituo vya kazi katika Sekta ya Elimu na Afya nchini.

Orodha hiyo inatokana na waombaji wenye sifa waliokidhi vigezo baada ya Aprili, 2022 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kutoa kibali cha ajira kwa kada za Ualimu na Afya, kwa ajili ya kuajiri walimu 9,800 wa shule za msingi na sekondari na wataalam wa afya 7,612.

Mheshimiwa Innocent Bashungwa amesema, baada ya kupata kibali cha ajira, Ofisi ya Rais-TAMISEMI ilitoa tangazo kwa wahitimu mbalimbali wa Ualimu na Kada za Afya, kuwasilisha maombi ya kazi, kupitia mfumo wa kielektroniki wa kupokea na kuchakata maombi ya ajira, kuanzia Aprili 20 hadi Mei 8,2022.

Mheshimiwa Bashungwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo Juni 26, 2022 amesema, jumla ya maombi 165,948 yakiwemo ya wanawake 70,780 na wanaume 95,168 yaliyopokelewa kwenye mfumo, ambapo maombi ya kada za afya ni 42,558, na kada ya Ualimu ni 123,390.

Amesema,kada zilizokosa nafasi ni Daktari wa Meno (50), Tabibu Meno (43), Tabibu Msaidizi (244), Mteknolojia Mionzi (86) na Muuguzi ngazi ya cheti (313).

Mheshimiwa Waziri amesema, kada hizi zitarudiwa kutangazwa ili kupata waombaji wenye sifa watakaojaza nafasi.

Post a Comment

0 Comments