Msajili Mahakama Kuu atoa maelekezo kwa wamiliki wa maeneo ya kimkakati ndani ya Mhimili

NA TIGANYA VINCENT-Mahakama

MSAJILI wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt amewataka Wamiliki wa maeneo ya kimkakati ndani ya Mhimili (SO-Owners) kuhakikisha wanatumia mafunzo waliyopata ya usimamizi wa miradi kuhakikisha miradi inayoendelea inasimamiwa kwa weledi na kuongeza huduma ya utaoji haki kwa wananchi. 
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya namna bora ya kusimamia Miradi (Project Management) kutoka Mahakama ya Tanzania wakifuatilia hotuba ya ufungaji wakati wa kuhitimisha mafunzo mjini Mombasa. 

Mhe. Sarwatt ameyasema hayo jana tarehe 10 Juni, 2022 mjini Mombasa alipokuwa akifunga mafunzo ya siku 14 ya namna bora ya kusimamia Miradi (Project Management) kwa kundi la pili ambayo yaliyoanza tarehe 30 Mei mwaka huu. 

Alisema mafanikio ya Mahakama yanategemea jitihada za watumishi wote na hivyo ni vema wahakikishe elimu waliyopata wanaipeleka kwa watumishi wengine ambao hawakupata fursa ya kushiriki mafunzo hayo. 

“Mafunzo mliyopata kwa siku zote yanapaswa kusaidia katika kusimamia vizuri miradi ya Mahakama ili ikamilike kwa ubora na kiwango kinachokusudiwa, na elimu hiyo mliyopata msikae nayo nyinyi pekee yenu nendeni mkawafundishe watumishi walio chini ya Idara na Vitengo mnavyovioongoza ili kuleta mafanikio makubwa kwa Mahakama yetu ya Tanzania” alisisitiza. 
Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt (kulia) akifunga mafunzo ya namna bora ya kusimamia Miradi (Project Management) kwa kundi la pili la Watumishi wa Mahakama ya Tanzania. Amefunga mafunzo hayo jana tarehe 10 Juni, 2022 jijini Mombasa . Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Maboresho cha Mahakama ya Tanzania (JDU), Mhe.Dkt.Angelo Rumisha.

Aidha, aliwataka Wahitimu wa Mafunzo hayo kuhakikisha wanatumia ujuzi walioupata kuleta matokeo mazuri ili Viongozi wa Mahakama ya Tanzania wakiongozwa na Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma waone kuwa hawakukosea kuwatafutia mafunzo ya usimamizi wa miradi watumishi wao. 

Msajili huyo aliongeza kuwa, hatua hiyo itaonekana kuwa na tija ikiwa kutakuwa na matokeo chanya katika utekelezaji wa miradi inayoendelea na ile inayokusudiwa kuanza hapo baadae. 

Mafunzo hayo ya siku 14 yametolewa na wakufunzi kutoka Taasisi ya Mafunzo ya Uongozi na Utawala katika Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika (ESAMI) ambapo jumla ya watumishi 31 wamepata mafunzo hayo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news