Mamlaka za Serikali za mitaa kuepuka hoja za ukaguzi

NA ASILA TWAHA, OR-TAMISEMI 

KATIBU Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI),Prof. Riziki Shemdoe amezitaka halmashauri zote 184 nchini kuhakikisha zinatekeleza na kusimamia miradi yote inayopelekwa katika halmashauri ili kuepuka hoja za ukaguzi zinazotokea pindi miradi hiyo inaposhindwa kutekelezwa kwa wakati. 
Akizungumza na Wakurugenzi na Maafisa manunuzi wote wa Mamlaka za Serikali za Mitaa hivi karibuni jijini Dodoma, Katibu Mkuu amesema, hoja za ukaguzi zinazotokea katika halmashauri zinaepukika na inawezekana kutokuwepo kwa hoja kabisa kwa watendaji kusimamia, kutekeleza majukumu yao na kufuata sheria na taritibu za utekelezaji wa miradi yote ya maendeleo inayopelekwa katika maeneo yao. 

Akiendelea kufafanua kuhusu mpango wa utekelezaji unaowekwa na halmashauri husika katika utekelezaji wa miradi kisha Halmashauri kutokutekeleza au kubadilisha matumizi ya malengo yaliyowekwa na kutofuata sheria ni miongoni mwa chanzo kikubwa cha hoja za ukaguzi. 

"Pesa za ruzuku zinazopelekwa Halmashauri kubadilisha matumizi kwa kutokuomba kibali vinachangia hoja hizi.

“Watendaji wenzangu tufuateni sheria kuepuka hoja tufuate taratibu za kazi sisi kama viongozi na niwatendaji tushirikianeni ili tumalize hoja hizi,"alisisitiza Prof. Shemdoe. 

Aidha, aliwaelekeza Wakurugenzi wote kuisimamia miradi inayopelekwa kwenye maeneoe yao kwa ubora na wahakikishe thamani ya fedha inaonekana. 

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Wakurugenzi, Bw. Kiomoni Kibamba ameishukuru Serikali kwa kuendelea kupeleka miradi ya maendeleo na kuahidi wataendelea kuisimamia kwa kuzingatia maelekezo wanayopatiwa. 

“Kupitia kikao hiki cha tathmini ya utendaji wa miradi ya maendeleo tutaendelea kufanya kazi kwa uadilifu na ubora unaotakiwa ili wananchi wapate huduma bora,” alisema Bw.Kibamba. 

Kikao hicho cha siku moja kilikuwa na lengo la kujadili tathmini ya utekekelezaji wa miradi ya UVIKO-19 na miradi mingine yote inayotekelezwa kwenye halmashauri.

Post a Comment

0 Comments