Mjadala wa saa mbili na nusu wajibu hoja na maswali yote kuhusu Loliondo na Ngorongoro

NA DIRAMAKINI

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Balozi Dkt. Pindi Chana amesema jumla ya vigingi 422 vimewekwa kutenga eneo la kilomita 1,500 za mraba ambazo ni Pori Tengefu la Loliondo lililopo Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha.
Mheshimiwa Balozi Dkt.Chana ameyasema hayo leo Juni 22,2022 kupitia mjadala maalum kupitia mtandao wa Zoom.

Mjadala huo umeratibiwa na Watch Tanzania kwa udhamini wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania na Airtel Tanzania.

Mada kuu iliangazia juu ya Zoezi la Uwekaji Alama za Mipaka Tarafa ya Loliondo na Maendeleo ya Zoezi la Uhamaji wa Hiari kwa Wakazi wa Ngorongoro

Mheshimiwa Waziri amesema, hatua hiyo imechukuliwa ili kutunza eneo hilo muhimu ambalo ni mazalia ya wanyamapori na chanzo muhimu cha maji. 

“Kabla ya hapo eneo hili lote lilikuwa pori tengefu kilomita za mraba 4,000, lakini sasa Serikali ikasema hizi 2,500 tuwaachie wananachi, hili eneo la kilomita 1500 la hifadhi tulitunze.

“Kwa hiyo kwa tangazo la Serikali namba 421 la tarehe 17 Juni 2022 sasa linatangazwa kuwa Pori Tengefu la Poloreti na eneo hili ndipo mapito ya nyumbu, wanapita eneo hilo, wanazaliana eneo hilo, kuna vyanzo vya maji na maji haya ndiyo yanasaidia hata upande wa Serengeti,” amesema Waziri Dkt.Chana. 

Uwekaji wa alama za mipaka unatokana na uamuzi wa Serikali hususani Baraza la Mawaziri liloketi mwaka 2019 wa kuhakikisha alama zote za mipaka katika eneo hilo zinazoonekana zinawekwa katika maeneo yote ya hifadhi ili kuepusha wananchi kuvamia na kuzuia migogoro isiyo ya lazima.

“Unaposema hii ni hifadhi lazima kuwe na kigingi pamoja na majina nukta yake kwa hiyo hili ni zoezi la kawaida kabisa,” amesisitiza Waziri Balozi Chana.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mheshimiwa John Mongela amesema uwekezaji wa alama za mipaka Loliondo ulikuwa na umuhimu mkubwa ili kudhibiti watu kuvamia maeneo ya pori tengefu lilipo katika tarafa hiyo.

Amesema, wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo haki za binadamu zimezingatiwa na limekamilika vizuri, licha ya kuwepo kwa madai ya baadhi ya Wamasai kujeruhiwa.

Mheshimiwa Mongella amekanusha madai ya baadhi ya watu wanaosema kuwa eneo hilo limeuzwa kwa mwekezaji.

“Pori la Loliondo halijawahi kumilikiwa na mtu binafsi ni mali ya umma chini ya usimamizi wa Serikali,mimi nataka ushahidi wa mtu ambaye atasema pori hili ni mali ya mtu.

“Mimi kama mkuu wa mkoa sijapata huo ushahidi na usimamizi wake uko chini ya mamlaka za mfumo wa Serikali ambazo wanasimamia maeneo mengine mengi nchini,” amesema Mheshimiwa Mongella.

Kwa upande wake,Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa katika ofisi ya Geneva nchini Uswisi, Balozi Hoyce Temu amesema, jumuiya ya kimataifa zinapaswa kuelewa kuwa zoezi la kuweka alama ni la kawaida katika shughuli uhifadhi na wananchi hawajaondolewa katika eneo la Loliondo.

“Wamerudi katika kanuni za malengo endelevu ambazo ni kuheshimu sayari, kujali jamii, kujenga jamii ya kidemokrasia na kutoacha mtu myuma ndiyo kilichotokea kuonekana kwamba sisi Tanzania tunafanya kwa ajili ya wananchi wetu,” amesema Balozi Temu.

Wakati huo huo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa amesema Serikali imetenga na kupeleka shilingi milioni 503.4 kufanya matengenezo ya barabara Kwenjugo-Mbagwi-Msomera yenye kilomita 32.6.

Ni barabara kuu kutoka makao makuu ya Wilaya ya Handeni hadi eneo la Msomera wanapohamia wakazi kutoka eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ili barabara ziweze kupitika wakati wote bila shida.

Pia, Serikali imetenga shilingi Milioni 716 kwa ajili ya matengenezo ya barabara za mizunguko ndani ya eneo la Msomera yenye kilomita 50 ambapo zitafunguliwa barabara mpya, matengenezo, kujengwa vivuko na kalavati ili kurahisha huduma ya kuingia na kutoka kwa wananchi inayoenda sambamba na utengenezaji wa barabara inayounganisha Kijiji cha Msomera na Wilaya ya Korogwe yenye urefu wa kilomita 22.8.

Bashungwa amesema, tayari ujenzi wa shule ya msingi mpya umekamilika na shule ya sekondari mpya ambayo vyumba saba vya madarasa vimekamilika, ujenzi wa bweni unaendelea kwa ajili ya wanafunzi wenye uhitaji wa kukaa shuleni, ujenzi vyoo vipya vya kutosha na ofisi za walimu na mahabara kwa ajili ya wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi.

Aidha, ameeleza inakadiriwa jumla ya wanafunzi 765 watahamia eneo la Msomera ambapo wanafunzi 415 wa awali na msingi na wanafunzi 350 wa sekondari, hivyo idadi ya wanafunzi hao itakuwa sambamba na kupeleka walimu katika shule hizo.

Vile vile, Bashungwa amesema tayari Serikali imetoa shilingi milioni 500 kuanza ujenzi wa kituo cha afya kipya na shilingi Milioni 50 kwa ajili ya kupanua na kuboresha huduma za afya katika zahanati ya Kijiji cha Msomera na kujenga jengo la wazazi, kuongeza watumishi na wataalam wapya katika sekta ya afya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news