NDOO KICHWANI ZINUNE: Missenyi kumekucha, makubwa yendafanyika,Ni tisa Juni, mradi unafunguka

NA LWAGA MWAMBANDE (KiMPAB)

JUNI 9, mwaka huu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua Mradi wa Maji wa Bilioni 15.7 wa Kyaka-Bunazi wilayani Missenyi Mkoa wa Kagera.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akifungulia maji kama ishara ya uzinduzi wa mradi wa maji utakaohudumia Mji wa Misungwi na maeneo ya pembezoni Juni 14, 2021. (Picha na Ikulu).

Mradi huo ambao unatarajiwa kuwanufaisha zaidi ya wananchi 65,000 unatajwa kuwa wa kwanza wa aina yake kutumia chanzo cha maji cha Mto Kagera.

Huu ni mto ambao una historia ndefu ambao pia ndiyo chimbuko la jina la Mkoa wa Kagera, ambao hutiririsha maji yake kutoka Rwanda kupitia Kaskazini na kumwaga maji yake katika Ziwa Victoria.

Mshairi wa kisasa, Bw.Lwaga Mwambande kwa kuendelea kutambua juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita za kuhakikisha inamtua mwanamke ndoo kichwani, kwa kuhakikisha inatekeleza miradi mbalimbali ya maji, kupitia kalamu yake ana jambo la kukushirikisha kuhusu mradi huu, ungana naye kujifunza hapa;

1:Ni Missenyi kumekucha, makubwa yendafanyika,
Hata ninaacha bucha, na mimi niweze fika,
Anayekuja ni kocha, kazi ni kuwajibika,
Maelfu maelfu, maji watanufaika.

2:Ni tarehe tisa Juni, mradi unafunguka,
Na Rais wa nchini, kazi hiyo atashika,
Furaha hadi moyoni, adha yazidi punguka,
Maelfu maelfu, maji wanufaika.

3:Huu mradi wa maji, ni mkubwa kwa hakika,
Waenda tibu hitaji, la maji ya kutumika,
Kyaka na Bunazi maji, yanakwenda tiririka,
Maelfu maelfu, maji watanufaika.

4:Ni mwanzo Mto Kagera, maji kuweza tegeka,
Hii yatimiza sera, ndoo kuacha kutwika,
Maji salama na bora, nyumbani kumiminika,
Maelfu maelfu, maji watanufaika.

5:Awamu hii ya sita, serikali kwa hakika,
Lengo lake kuifuta, shida maji kusikika,
Pesa nyingi inapata, miradi inafunguka,
Maelfu maelfu, maji watanufaika.

6:Rais Samia heko, kazi inayofanyika,
Twatoka kwenye uloko, ukisasa unafika,
Kupika madikodiko, shida maji yatoweka,
Maelfu maelfu, maji watanufaika.

7:Sitinatano elfu, watu watafaidika,
Maji wawe ni nadhifu, afya zikiimarika,
Ni usafi si uchafu, ndio utaongezeka,
Maelfu maelfu, maji watanufaika.

8:Hiyo nakwambia moja, miradi yaongezeka,
Pesa trilioni moja, zinakwenda kutumika,
Ni miradi ya pamoja, nchi nzima yafanyika,
Maelfu maelfu, maji watanufaika.

9:Miji ishirina nane, inakwenda nufaika,
Watu wengi si wanne, maji yatakakofika,
Ndoo kichwani zinune, kwenye vichwa zafutika,
Maelfu maelfu, maji watanufaika.

10:Wanawake Tanzania, wengi ndio hupigika,
Maji ili kufikia, nyumbani ya kutumika,
Miradi ikiwajia, kwa kweli wanakomboka,
Maelfu maelfu, maji watanufaika.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Post a Comment

0 Comments