Rais Samia na uchumi wa gesi, tupo njia sahihi

NA DAVID KAFULILA

JUNI 11, 2022, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameshuhudia makubaliano ya awali ya uwekezaji wa dola za Kimarekani Bilioni 30 kati ya Serikali yake na kampuni kubwa tano za kimataifa ambazo ni Equinor, Shell, ExxonMobil, Medco Energy na Pavilion.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akishuhudia utiaji saini Mkataba wa Awali wa Mradi wa kuchakata na kusindika Gesi Asilia (Liquefied Natural Gas – LNG Project) kwenye Hafla iliyofanyika Juni 11, 2022 Ikulu, Chamwino jijini Dodoma.

Hii ni hatua muhimu sana kuelekea makubaliano ya msingi kuhusu utekelezaji na uendeshaji wa mradi (Host Government Agreement) ambayo yanatarajiwa kufikiwa Desemba 2022 na hatimaye maamuzi ya mwisho wa uwekezaji yanayotarajiwa kufikiwa mwaka 2025.

Huu ni uwekezaji mkubwa sana Mashariki na Kusini ya Afrika. Prof.Benno Ndulu mwaka 2016 alisema uwekezaji wa awali tu (initial investment) ingeongeza asilimia mbili ya pato la Taifa..

Uwekezaji wa dola bilioni 30 ni nusu ya uchumi wa Tanzania kwa sasa ( $64bn), ni karibu sawa na uchumi wa Uganda kwa sasa($34bn), ni karibu mara tatu ya uchumi wa Rwanda kwa sasa ($11bn)na ni karibu sawa na theluthi moja ya uchumi wa Kenya kwa sasa($99bn). 

Kama mwenendo wa uchumi utaenda kama ulivyo (ceteris peribus),biashara hii itaifanya Tanzania kinara wa uchumi Afrika Mashariki.

Huu ni mradi mkubwa unaohusisha weledi katika maeneo mengi ya Nishati, Biashara na Uchumi wa kitaifa na kimataifa, sheria za kitaifa na kimataifa, mazingira na taaluma nyingi zinazohitaji weledi na uzoefu mkubwa. 

Ndio maana nilipata kuandika kwenye gazeti la Raia Mwema siku ya Mei 5, 2021 kwamba tulihitaji mshauri eneo hilo kumudu meza ya majadiliano. 

Ndio sababu niliposoma Januari 25, 2022 kuwa Serikali imepata mshauri mwelekezi kampuni yenye uzoefu ya Boots Barker kutoka Uingereza. Nilipongeza nikiamini ilikuwa hatua muhimu sana kutanzua mkwamo wa mradi huu ambao ulifika mahala kuzua maswali tunakwama wapi hasa ikizingatiwa nchi kama Msumbiji ilikuwa imepiga hatua mbele.

Nikweli nchi yetu ina wasomi na vyuo vingi, lakini ni ukweli usiopingika kuwa hatuna hazina yenye weledi na uzoefu wa kutosha kwenda mezani mwanzo mwisho kwenye mradi mkubwa kiwango hiki bila kujengeana uwezo wa ziada.. 

Na kwa dunia ya leo sio aibu kununua au kukodi utalaamu usiokuwa nao kufanikisha jambo kubwa kama hili. Nakumbuka Uingereza baada ya mgogoro wa kiuchumi walimteua Mark J. Carney ambaye alipata kuwa Gavana wa Canada kuwa Gavana wa Bank Kuu Uingereza (NewYork Times Nov26, 2012). https://www.nytimes.com/2012/11/27/business/global/canadian-to-lead-bank-of-england.html#:~:text=LONDON%20%E2%80%94%20In%20a%20surprising%20departure,Britain's%20most%20prominent%20public%20officials

Au mwaka wakati Uingereza inafanya maamuzi ya kujitoa Umoja wa Ulaya, walimteua mshauri mwelekezi kutoka News land kuwa mshauri mwelekezi kwenye mikataba mipya ambayo Uingereza ilipaswa kuingia upya kama Taifa na mataifa mengine.

Alipoulizwa Waziri Mkuu wa Uingereza kwa nini amefanya maamuzi ya kuteua mtaalamu kutoka nchi nyingine kuongoza timu ya wataalamu wake katika kushauri serikali kuhusu mikataba kati ya nchi yake na nchi zingine, alijibu kuwa kwa muda Uingereza imekaa Umoja wa Ulaya imepoteza uzoefu wake katika kuingia mikataba hiyo kwa kuwa miaka yote mikataba hiyo ilifanyiwa kazi Brussels.

Sasa kama Taifa kubwa lenye vyuo bora dunaini kuna mahala linakubali kupungukiwa na kukodi au kuazima utaalamu toka nje, sioni tatizo kwa nchi yetu. Muhimu ni tunajua tunachokitaka na hivyo mshauri anatusaidia namna ya kukifikia.

Lakini pia miradi kama hii inahitaji uelewa na uvumilivu kwa sababu ni mradi unaokwenda kubadilisha kabisa uchumi wa Tanzania, lakini unachukua muda (game changer). 

Ndio unaona mpango wa kufikia maamuzi ya uwekezaji unapangwa kufikiwa mwaka 2025 (investment decision), na mwanzo wa ujenzi mpaka kukamilisha itachukua miaka kadhaa pia. 

Na hii ni kawaida, nchi kama Canada iliwachukua miaka saba kufikia maamuzi ya uwekezaji (Investment Decision) na kampuni hizi za Kimataifa kwenye mradi kama huu wa Kitimat wenye thamani $31bn.soma gazeti la CITIZEN- November8, 2018 hapa https://www.thecitizen.co.tz/tanzania/magazines/canada-offers-lessons-on-lng-project-for-tanzania-2661110

Kwenye Dunia ambayo nishati ni mwamuzi wa uchumi duniani, makubaliano yake yanachagizwa na misukumo mingi ikiwemo ujasusi mkubwa kwani mafanikio ya nchi yoyote kuingia soko la LNG yanabeba tafsiri pia kwa nchi washindani ambao wana sura tofauti ama za kama kampuni za kimataifa zinazoshindana au nchi wahusika zinazoshindana. 

Ndio sababu sio ajabu tena mbinu kama ugaidi kuweza kuwa sehemu ya mkakati katika kukabiliana kibiashara tofauti na dhana ya zamani kuhusu misingi ya ugaidi. 

Ni katika msingi huo uwekezaji mkubwa kama huu unachukuliwa tahadhari zote. Wote tunakumbuka kilichotokea Msumbiji baada ya kuonekana wanaweza kuingia mapema kwenye soko la LNG wakiwa na LNG ya bei nafuu sana kutokana na mazingira ya gesi yao asilia.

Msumbiji wana bahati kubwa ya gesi asilia karibu futi za ujazo trilioni 100 karibu mara mbili ya Tanzania ambapo gesi iliyokwishanguliwa inafikia futi za ujazo trilioni 57. 

Zaidi gesi ya Msumbiji karibu asilimia 85 inapatikana kwenye eneo la kina kifupi (shallow water) kulinganisha na Tanzania ambao karibu asilimia 90 ya gesi ipo bahari ya kina kirefu ( deep sea). 

Niliwahi kugusia hili kama sababu ya Msumbiji kututangulia wakati bei ya gesi asilia dunia imeanguka kiasi ambacho ilihitajika kuzalisha kwa unafuu ili kuweza kuwa biashara. 

Tafiti zinaonesha kwamba gharama za kuchimba kisima cha gesi kwenye kina kirefu  (deapsea) ni karibu mara mbili ya kuchimba kina kifupi. 

Kwa takwimu za mwaka 2015 ni kati ya $50m- mpaka $70m kulinganisha na kisima kirefu (deap sea) ambacho ni kati ya $ 100m mpaka $120m. https://www.sciencedirect.com/topics/engineering/drilling-cost

Naam, changamoto ni nyingi lakini tupo kwenye mstari sahihi. Tunahitaji kujenga mjadala wa uelewa ili kurahisisha mijadala kwenye masuala makubwa yenye maslahi mapana kwa Taifa letu leo na kesho. Tulipoamua kujenga uchumi wa gesi Tanzania, kwa kiasi kikubwa tulitazama mradi huu wa gesi asili (LNG).

Post a Comment

0 Comments