Kamati ya Bunge yatoa ushauri kwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

NA MWANDISHI WETU

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeishauri Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi katika ujenzi wa kushirikisha wadau kutoa vipaumbele kwa miradi ya barabara za kiuchumi kwa Taifa na ile ya kimkakati ili kufanikisha malengo makuu ya Serikali. 
Kazi za ushindiliaji wa zege katika barabara ya Lusitu – Mawengi (km 50) zikiendelea mkoani Njombe. Ujenzi wa barabara hiyo unatarajiwa kukamilika ifikapo Agosti mwaka huu. (PICHA NA WUU).

Hayo yamesemwa mkoani Njombe na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Selemani Kakoso wakati Kamati hiyo ilipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Itoni – Ludewa – Manda (km 211.4), sehemu ya Lusitu – Mawengi (km 50), inayojengwa kwa kiwango cha zege na kuridhishwa na hatua zilizofikiwa za ujenzi huo. 

“Kamati inaangalia miradi ya kimkakati hivyo Wizara katika mipango yenu hakikisheni mnazingatia barabara zitakazokuza uchumi wa Taifa na kurudisha gharama kwa haraka,”amesema Mwenyekiti huyo. 
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mhe. Selemani Kakoso, akifafanua jambo kwa wajumbe wa Kamati na uongozi wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi wakati kamati hiyo ilipokagua ujenzi wa barabara yaLusitu – Mawengi (km 50), kwa kiwango cha zege, mkoani Njombe.

Mhe. Kakoso ameeleza kuwa ukamilikaji wa barabara hiyo utaenda sambamba na ongezeko la mizigo katika Bandari nchini kwa kuwa katika Mkoa wa Njombe ndipo kwenye uzalishaji mwingi wa mazao ya misitu, makaa ya mawe ya Mchuchuma na madini ya chuma cha Liganga na hivyo kutaongeza zaidi mapato kwa Serikali. 

“Mkoa wa Njombe ni mkoa tajiri sana kwani una rasilimali kubwa ambazo zinaweza zikatengeneza pato kubwa la Taifa na GDP ya kwetu kupanda kwa kiwango kikubwa,”amefafanua Mwenyekiti wa Kamati. 

Aidha, Kamati imempongeza Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutoa fedha za ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja kwa wakati na kufungua uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na kuchochea biashara kati ya mikoa kwa mikoa na nchi kwa nchi. 

“Tumeelezwa kuwa tayari mkandarasi wa sehemu ya kwanza ya barabara hii kuanzia Itoni – Lusitu (km 50), ameshakabidhiwa eneo kwa ajili ya kuanza ujenzi hii ina maana kubwa kuwa Serikali ipo kazini na inaendelea kuifungua barabara hii,” amesema Mhe. Kakoso. 

Vilevile, Kamati imeishauri Serikali kutafuta fedha kwa ajili ya kuunganisha mkoa wa Njombe na Morogoro kwa barabara za kiwango cha lami kuanzia Kibena – Lupembe – Madeke – Mlimba – Ifakara – Mikumi kwa kuwa ni barabara ya kiuchumi. 
Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, akisisitiza jambo kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu katika ziara yao ya ukaguzi wa ujenzi wa barabara ya Lusitu – Mawengi (km 50), kwa kiwango cha zege, mkoani Njombe.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, ameishukuru Kamati hiyo kwa kukagua na kujionea kazi zinavyoendelea za uwekaji zege katika barabara hiyo ambayo ujenzi wake unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Agosti, mwaka huu. 

Kasekenya ameieleza Kamati hiyo kuwa Serikali iko mbioni kuanza kuijenga upya barabara ya Njombe hadi Songea ambayo imekuwa finyu na ilijengwa toka miaka 1980 na tayari Benki ya Dunia imekwishatoa fedha kwa ajili ya uboreshaji mkubwa wa barabara hiyo. 

Awali akitoa taarifa ya mradi, Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Njombe Eng. Ruth Shalua, ameeleza kuwa mpaka sasa ujenzi umefikia asilimia 88 ambapo kilometa 47.3 zimekwishakamilika kujengwa kwa kiwango cha zege na kazi zinaendelea vizuri na wanauhakika mradi utakamilika kwa muda uliopangwa na viwango vya ubora. 

Nao Wabunge kutoka jimbo la Njombe Mjini, Mhe. Deo Mwanyika na Mbunge wa Jimbo la Ludewa Mhe. Joseph Kamonga, wameishukuru Serikali kwa kuendelea kufungua mkoa huo kwa barabara zenye viwango na kuahidi kuendelea kuisimamia miradi yote inayoendelea kwa karibu. 

Takribani magari 10,000 yanatarajiwa kupita kwa siku katika barabara ya Itoni – Ludewa – Manda (km 211.4) pindi barabara hiyo itapokamilika kujengwa na hivyo kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji na kupunguza muda na gharama za usafiri.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news