RC Hapi ateta na watu wenye ulemavu

NA DIRAMAKINI

MKUU wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi amekutana na watu wenye ulemavu wa Mkoa wa Mara katika ukumbi wa Chuo cha Utatibu Musoma na kupokea baadhi ya changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu katika Mkoa wa Mara.

Akizungumza katika kikao hicho, Mheshimiwa Hapi amewataka Maafisa Ustawi wa Jamii kuwasaidia watu wenye ulemavu ikiwa ni pamoja na kuwaombea ufadhili kwa wadau ;na kuwasaidia kuomba mikopo ya Halmashauri na kuifuatilia mikopo hiyo kwa niaba ya watu wenye ulemavu.

“Ninataka Maafisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri muwajibike katika kuwasaidia watu wenye ulemavu, kuwaombea ufadhili katika masuala mbalimbali kwa wafadhili na kufuatilia mikopo yao wanayoomba Halmashauri,"amesema Mheshimiwa Hapi.

Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa kazi ya Afisa Ustawi wa Jamii ni pamoja na kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu masuala yao yanapewa kipaumbele na Halmashauri zao na wanasikilizwa wanapokuwa na shida katika ofisi za Halmashauri.

Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa amewaagiza Wakuu wa Wilaya zote za Mkoa wa Mara kuzindua Kamati za watu wenye ulemavu katika ngazi za Wilaya, Kata, Vijiji na Mitaa katika wilaya zao kwa mujibu wa miongozo ya Serikali.

Mheshimiwa Hapi amemtaka Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Buhare kukarabati ofisi na vyoo vinavyotumiwa na Shirikisho la Watu Wenye Ulemavu Mkoa wa Mara wakati anapofanya ukarabati majengo ya chuo hicho.

Mkuu wa Mkoa ameagiza Waganga Wakuu wa Halmashauri kuhakikisha dawa zote zinazotumiwa na watu wenye ulemavu wa akili na matatizo ya kisaikolojia zinapatikana wakati wote ili kuwaondolea changamoto za ukosefu wa dawa hizo wanazodai kuzipata.

Amewataka wazazi wa Watoto wenye ulemavu kuwapeleka Watoto hao shule ili waweze kupata elimu itakayowasaidia kuweza kuyamudu maisha yao ya baadaye.

Aidha Mkuu wa Mkoa ameahidi kuwasaidia kupata ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zinazowakabili watu wenye ulemavu katika Mkoa wa Mara zilizopo ndani ya mamlaka yake.

Mheshimiwa Hapi amechukua fursa hiyo kuwahamasisha watu wenye ulemavu kushiriki katika Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika hapa nchini tarehe 23 Agosti, 2022.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirikisho wa Watu Wenye Ulemavu Mkoa wa Mara Bwana Iddi Hamis Mtani amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kukutana na watu wenye ulemavu kwa mara ya pili baada ya kula nao futari wakati wa Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Akisoma risala ya watu wenye ulemavu ameeleza kuwa wanakabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo ughali wa vifaa saidizi vinavyotumiwa na walemavu, ukosefu wa takwimu sahihi za watu wenye ulemavu, taasisi za fedha kukataa kutoa mikopo kwa walemavu waioona kutokana na kukosa utaalamu wa kuandika na kusoma maandishi ya nukta nundu na uchakavu wa majengo na miundombinu ya Kituo cha Watu wenye Ulemavu Nyabange.

Bwana Mtani amezitaja changamoto nyingine kuwa ni baadhi ya walemavu kutokunufaika na TASAF, halmashauri kutokutenga bajeti za kutosha kuhudumia watu wenye ulemavu na milolongo mirefu ya kupata mikopo ya Walemavu inayotolewa na Halmashauri.

Katika risala hiyo, Shirikisho la Watu Wenye Ulemavu wamemuomba Mkuu wa Mkoa kuwasaidia kupata kiwanja ambacho wamepatiwa na Manispaa ya Musoma ambacho wameshindwa kukilipia gharama za kulipa fidia inayokadiriwa shilingi 21,200,000.

Mkoa wa Mara kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi unajumla ya watu wenye ulemavu mbalimbali 13,650 ikiwa ni miungoni mwa mikoa yenye watu wengi wenye ulemavu.

Kikao cha Mkuu wa Mkoa na watu wenye ulemavu kimehudhuriwa na Afisa Usalama wa Mkoa, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa, Mwakilishi wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, viongozi wa taasisi zinazotoa huduma katika Mkoa wa Mara na baadhi ya watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.

Post a Comment

0 Comments