RC Hapi awahimiza viongozi wa dini kuhubiri amani

NA DIRAMAKINI

MKUU wa Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Ally Salum Hapi amekutana na viongozi wa dini wa Mkoa wa Mara na kuwataka viongozi hao katika mahubiri yao kuhimiza umoja, amani na usalama.

“Ninawaomba viongozi wa dini mkemee watu kutembea na silaha kila wakati bila ya sababu za msingi na matokeo yake mtu amemkosea kidogo tu anamfanyia ukatili wa kutisha jambo ambalo halipendezi;

Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa hivi sasa kumekuwa na matukio mengi ya ukatili katika jamii ambayo yanaashiria kuna sehemu jamii imepotoka na inahitaji kujirekebisha katika masuala ya maadili na kumjua Mungu na kuwataka viongozi hao kuendelea kutoa mafundisho ya kukemea ukatili kwa waumini wao.

Amewahamasisha viongozi hao wa dini kutumia nafasi zao na kukemea masuala yote ambayo yanadhalilisha wanawake, watoto na makundi yenye mahitaji maalum katika jamii kwa kukemea vitendo vya ukeketaji, baadhi ya mila potofu na mahusiano mabaya katika jamii.

Mheshimiwa Hapi amewataka viongozi wa dini kuhimiza malezi bora ya watoto na msingi mzuri wa familia ili kuweza kuwalinda waumini wao dhidi ya watu wasio na maadili mema kutoa elimu kwa makundi mbalimbali na hatimaye kubomoa jamii.

Amewataka viongozi wa dini kuisaidia Serikali katika kulinda amani na utulivu wa nchi ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa pale ambapo wanahisi kunatatizo kwa vyombo vya usalama ili kuweza kulinda amani na utulivu uliopo nchini.

Mheshimiwa Hapi ameitaka Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Mara kutumia hekima katika kudai kodi ya ardhi ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na viongozi wa dini kabla ya kuwapelekea madai ya kodi ya ardhi au kukumbushia malipo ya kodi ya ardhi.

Amewaagiza Wakuu wa Wilaya kufuatilia Mamlaka ya Udhibiti ya Usafiri Ardhini (LATRA) kuhusiana na kupanda kwa nauli katika maeneo mbalimbali hapa mkoani kulingana na hali halisi ya bei za mafuta zilivyo kwa sasa.

Risala ya viongozi wa dini kwa Mkuu wa Mkoa pamoja na masuala mengine ilimuomba Mkuu wa Mkoa kuwasaidia katika masuala ya kodi ya ardhi na kuwaombea msamaha wa malimbikizo ya kodi ya ardhi ya miaka ya nyuma ambapo walipatiwa utaratibu wa kufuata ili kuweza kulishughulikia suala hilo.

Aidha viongozi hao wamelalamikia tozo wanazolipa wanapoomba vibali kwa ajili ya mihadhara ya kidini katika mamlaka mbalimbali za Serikali na mfumko wa bei ambapo kwa kiasi kikubwa unawatesa wananchi katika kupata mahitaji yao muhimu.

Viongozi hao wamemuomba Mkuu wa Mkoa kuelimishwa kuhusiana na masuala ya Sensa ya Watu na Makazi yam waka 2022 ili na wao wasaidie katika kutoa elimu kwa waumini wao na watu wanaowazunguka ambapo wameahidiwa kupatiwa elimu hiyo ili waendelea kusaidia kama walivyosaidia kwenye mazoezi mengine muhimu.

Kwa upande wao, Wakuu wa Wilaya wameshukuru kwa ushirikiano wanaoupata kutoka kwa viongozi wa dini na kuwaomba waendelee kutoa ushirikiano kwa viongozi wa serikali ili kuleta amani katika jamii.

Mkutano huo umehudhuriwa pia na Katibu Tawala wa Mkoa, Wakuu wa Wilaya, Kamati ya Usalama ya Mkoa, Wakurugenzi wa Halmashauri, wakuu wa baadhi ya taasisi za Serikali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news