Serikali yadhamiria kuimarisha Pato la Taifa kupitia Uchumi wa Buluu

NA MWANDISHI WETU

SERIKALI imesema itaendelea kuwekeza kwenye rasilimali mafunzo kupitia Chuo cha Bandari Dar es Salaam (DMI) ili kuhakikisha dhamira ya kuongeza pato la Taifa kwa kutumia Uchumi wa Buluu inatekelezwa kikamilifu.
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete akimsikiliza Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Bandari Dar es Salaam (DMI), Mhandisi Ernest Mihayo kabla ya kufungua Mkutano wa kwanza wa kitaifa wa Uchumi wa Buluu uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa kwanza wa Kitaifa kuhusu Uchumi wa Buluu jijini Dar es Salaaam, Naibu Waziri wa Uchukuzi Atupele Mwakibete, amesema utekelezaji wa mikakati hiyo inakwenda sanjari na uzalishaji wa watalaam na utekelezaji wa miradi mikubwa ya meli ikiwemo ujenzi wa Meli kubwa ya MV. Mwanza na ukarabati wa meli katika Ziwa Tanganyika, Nyasa na Viktoria.

"Kama Serikali tumejipanga kikamilifu kupitia wataalam wanaozalishwa hapa DMI sababu Uchumi wa buluu unahitaji sana wataalm hawa katika maeneo mbalimbali hata viwandani,” amesema Naibu Waziri Mwakibete.

Naibu Waziri Mwakibete amesema ni wakati muafaka kwa wataalam kuangalia nyanja zote za uchumi huo wa buluu ikiwemo viumbe vilivyopo baharini kama miti ya mikoko, mwani na vingine ili kuwa na uwanda mpana wa namna wanavyoweza kuishauri Serikali kuanzia kwenye sera na utekelezaji.

Kwa upande wake Balozi wa Heshima wa Visiwa vya Shelisheli, Maryvonne Pool, amesema kama nchi wameweka mikakati madhubuti kuhakikisha kupitia bahari nchi inapata mapato hali inayofanya nchi hiyo kuwa na kiwanda kikubwa cha tatu duniani kinachouza samaki katika nchi za ulaya na maeneo mengine.

“Sisi tulishaanza kuitumia fursa ya uchumi wa buluu na mikakati tuliyojiwekea imeanza kuzaa matunda kwani Bahari imekuwa ikichangia sehemu kubwa ya pato la nchi yetu na kwenye hili tunalisimamia kwa karibu sababu tumeweka kanuni ambazo kwa mtu anayebainika anafanya uvuvi haramu faini ni kuanzia dola milioni moja", amefafanua Balozi Maryvonne Pool.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya DMI, Nahodha Ernest Mihayo, ameiomba Serikali kukitazama chuo hicho kwa uzito mkubwa kwani ni chuo pekee kinachozalisha wataalam watakaoweza kutimiza lengo la Serikali katika Uchumi wa Buluu.

Mkutano huo wa kitaifa wa Uchumi wa Buluu umewakutanisha wadau mbalimbali wa usafirishaji kwa siku mbili ambapo pamoja na mambo mengine utajadili na kuangalia fursa zilizopo Bahari ya Hindi na Maziwa Nchini na namna ya kuzitumia kwa manufaa ya Taifa.

Post a Comment

0 Comments