TRC yasitisha mkataba na Eurowagon, yafafanua kuhusu mabehewa

NA DIRAMAKINI

SHIRIKA la Reli Tanzania (TRC) limetoa ufafanuzi juu ya ununuzi wa injini na behewa za abiria na mizigo kwa matumizi ya reli ya kisasa - SGR kwenye mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa mikutano TRC jijini Dar es Salaam Juni 15, 2022.

Mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhusiano TRC, Bi. Jamila Mbarouk ameeleza kuwa, TRC inafanya manunuzi ya behewa za mizigo, behewa za abiria, seti za treni za kisasa pamoja na vichwa vya treni ya umeme kwa mgawanyo wa awamu mbili.

Bi. Jamila alisema kuwa, awamu ya kwanza ya ununuzi wa vifaa vya uendeshaji wa mtandao mzima wa awamu ya kwanza ya ujenzi wa SGR Dar es Salaam - Mwanza yenye urefu wa kilometa 1,219 ambapo muda wa manunuzi ni miezi 36 hadi 48, pia manunuzi ya pili ni ya vichwa na behewa kwaajili ya majaribio na endeshaji wa awali ambapo muda wa manunuzi ni miezi 9.

“Manunuzi yamefanyika kwa kuzingatia Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2011, pamoja na marekebisho ya mwaka 2016 na kanuni za mwaka 2013 na marekebisho ya kanuni ya mwaka 2016,” alisema Bi. Jamila.

Aidha, Bi. Jamila alieleza kuwa katika kuhakikisha uendeshaji wa awali unaanza mara baada ya majaribio, TRC ilisaini mkataba wa muda mfupi wa ununuzi wa vichwa vya treni ya umeme viwili na behewa 30 za abiria vitakavyofanyiwa ukarabati kutoka kampuni ya Eurowagon ya nchini Uturuki.
Hata hivyo Bi. Jamila aliongeza kuwa kampuni ya Eurowagon imeshindwa kutimiza matakwa ya mkataba huo ambao ulitakiwa kukamilika mnamo mwezi Novemba, 2021.

“Ujenzi kipande cha kwanza Dar es Salaam - Morogoro upo hatua ya mwisho, hivyo TRC iliamua kusitisha mkataba kwa barua mnamo tarehe 25, Februari , 2022,”alisema Bi. Jamila

Vilevile Bi. Jamila alisisitiza kuwa TRC inaendelea na jukumu la kumalizia ukarabati bila gharama na vifaa vinatarajiwa kukamilika mwezi Agosti 2022.

Naye Mkurugenzi wa Ujenzi na Miundombinu Mhandisi Machibya Masanja alisema kuwa TRC ilisaini mikataba ya manunuzi ya behewa mpya 1,430 za mizigo kutoka kampuni ya CRRC ya nchini China, behewa mpya za abiria 59 kutoka kampuni ya Sung Shin Rolling Stock Technology Limited kutoka nchini Korea ya kusini, seti 10 mpya za treni za kisasa zenye jumla ya behewa 80 na vichwa 17 vipya vinavyotumia nishati ya umeme kutoka kampuni ya Hyundai Rotem ya nchini Korea kusini kwaajili ya uendeshaji wa reli ya SGR.

“Gharama ya mikataba ni shilingi Trilioni 1.18 na ipo kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji “ alisema Mhandisi Machibya.

Mhandisi Machibya alieleza kuwa mikataba hiyo ya ununuzi imetolewa katika kampuni mbalimbali ambazo zilitaja bei nzuri ya manunuzi.

Pia Mhandisi Machibya alisema kuwa ujenzi wa SGR unajengwa kwa ufanisi na kuhakikisha usalama kwa wananchi kwa kujenga vivuko katika njia ya reli ikiwemo kivuko cha wanyama, binadamu na vyombo vya usafiri.

“Usanifu na ujenzi wa SGR tumezingatia mazingira halisi ya mtanzania“ alisema Mhandisi Machibya.

Ujenzi wa SGR kwa awamu ya kwanza Dar es Salaam - Mwanza unaendelea vema na mchakato wa manunuzi ya mkandarasi wa ujenzi wa awamu ya pili kwa kipande cha Tabora - Kigoma unaendelea.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news