TUZO YA GHANA NI USHAHIDI WA MAMBO MAKUBWA ANAYOFANYA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN

NA MWALIMU MEIJO LAIZER

NI dhahiri sasa kuwa vyombo vya habari Duniani vinahitaja Tanzania kama sehemu salama katika uendeshaji wa shughuli za kiuchumi na uwekezaji, kisiasa, kijamii na kadhalika.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akionesha Tuzo ya Babacar Ndiaye kwa mwaka 2022 (Babacar Ndiaye Trophy 2022) kutokana na mafanikio kwenye Ujenzi wa Barabara, mara baada ya kukabidhiwa Tuzo hiyo na Makamu wa Rais wa Sekta Binafsi, Miundombinu na Viwanda katika Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Solomon Quaynor tarehe 25 Mei 20220 Accra nchini Ghana. (Picha na Ikulu).

Nchi yetu imepata heshima nyingine kubwa kimataifa kwa Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan kupatiwa tuzo ya heshima kwa uzalendo, uwajibikaji na utendaji wake katika uongozi wa awamu yake ya sita ya serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania. Sisi sote ni mashahidi katika yote yanayofanyika katika Serikali yake.

Suala la ujenzi wa madarasa ya UVIKO 19 ni jambo jema na ni dhamira njema vilevile ya Rais, Uboreshaji wa huduma za afya nchi nzima, utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu ambayo imeboreshwa zaidi kwa kuwepo ongezeko kubwa la wanufaika maradufu, sekta ya maji kwa maeneo ya vijijini na mijini tumeshuhudia ikifanyiwa kazi zaidi kuhakikisha sasa huduma hiyo haipatikani kutoka umbali mrefu hii ni kazi nzuri inayofanywa katika Taifa letu na Mheshimiwa Rais Samia Sluhu Hassan.

Wanasema mnyonge mnyongeni lakini haki yake apewe, waziri mwenye dhamana ndugu Juma Awesso ameifanya kazi hii kikamilifu akimsaidia Mheshimiwa Rais kwa weledi mkubwa ili kuhakikisha anamtua mwanamke ndoo kichwani, jambo ambalo litasaidia kufanya shughuli za kiuchumi zaidi badala ya kuhangaika na kutafuta maji tena, kwani ilibidi watumie muda mwingi zaidi kuyatafuta maji badala ya kwenda shambani na shughuli nyingine za uzalishaji.

Hivyo tuzo aliyopewa Mheshimiwa Rais wetu huko nchini Ghana hakika anastahili na kwamba hajabebwa kwasababu ushahidi wa mambo makubwa anayofanya tunao hapa nchini na tuzo hiyo imekua zawadi kubwa kwetu watanzania kama nchi, tuna kila sababu ya kumuunga mkono kiongozi wetu na mkuu wa nchi ili afanye zaidi ya haya aliyofanya kwa muda huu mfupi, ni wakupewa moyo badala ya kumkatisha tamaa.

Eneo la uboreshaji wa masilahi ya watumishi wa umma aliyoufanya ni ushahidi mwingine sote tunaona, watumishi wa umma wanaostahili kupandishwa madaraja wamepanda, malipo ya malimbikizo ya mshahara inaendelea kulipwa, na nyongeza ya mshahara kwa watumishi wa umma tayari RAIS wetu ameridhia ongezeko la 23.3% hii ni hatua kubwa na upendo kwa watu wake haya yote yanathibitisha kwamba kupewa tuzo huko nchini Ghana hawajabahatisha na anastahili tuzo kubwa zaidi.

Ukusanyaji wa mapato kwa Sasa umevuka malengo ukilinganisha na hapo awali, suala la utoaji wa kodi kwa wananchi wetu limekua na hamasa kubwa na uzalendo zaidi kwani kila mtanzania amejua umuhimu wa kulipa kodi kwa nchi yake bila shuruti kwakuwa wanatambua kuwa wao ni sehemu ya maendeleo ya Taifa lao.

Kodi hizo zimesaidia katika ujenzi wa miundo mbinu iliyopelekea pamoja na mambo mengine kumfanya rais wetu atunukiwe tuzo huko Ghana, kwahiyo tuna kila sababu ya kutembea kifua mbele, kwamba tuzo ya rais ni yetu pia na tukifanya zaidi tutaendelea kumuheshimisha rais na nchi yetu kwa ujumla katika anga za kimataifa na hivyo Tanzania itaendelea kung’ara.

Suala la kujenga maridhiano na vyama vya siasa nchini pia limejenga heshima kubwa kwa Rais wetu na kwa nchi yetu kwani imeonyesha dhamira njema ya kiongozi wetu kuwa nchi hi itajengwa na watanzania wote bila kujali utofauti za vyama vyao, rangi, jinsia wala kabila.

Kudumisha umoja, mshikamano, amani na utulivu ndani ya nchi ndiko kutaleta maendeleo ya kweli hongera Mheshimiwa Rais kwa utashi huo.

Haya yanaendelea kuthibitisha kwamba tuzo ya Ghana imebeba ujumbe mkubwa kwa watanzania kujua na kutambua kazi zinazofanywa na Mheshimiwa Rais wetu.

Suala la Diplomasia ya kiuchumi nalo Mheshimiwa Rais hajaliacha nyuma na hii ni kwasababu Tanzania siyo kisiwa lazima tukubali kushurikiana na wenzeu huko duniani, ameendelea kujenga mahusiano ya kimataifa kila uchao kuhakikisha nchi na vilivyomo kama vivutio vya utalii vinajulikana zaidi na kuleta fedha za kigeni.

Funga kazi katika yote ni “FILAMU YA ROYAL TOUR” Kiukweli Mheshimiwa Rais ameupiga mwingi kama wasemavyo watanzanai wenzangu, katika suala zima la ukuaji na ukuzaji wa sekta ya utalii ambayo inachangia pakubwa katika pato la taifa.

Sote kama watanzania tukubali kuwa Tuzo ya Mheshimiwa Rais wetu ni zawadi kwetu kama Taifa na ni heshima kwa Rais, imeonyesha dhahiri kuwa uzalendo wake na upendo wake kwa nchi yetu imetujengea heshima sisi sote kama taifa hongera sana rais wetu Samia Suluhu Hassan.

Mwalimu Meijo Laizer ni;
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa mstaafu
Wilaya ya Siha
Mkoani Kilimanjaro
0755898037

Post a Comment

0 Comments