Waziri Dkt.Tax mgeni rasmi Miaka 41 ya SUMAJKT

NA DIRAMAKINI

WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ,Dkt.Stergomena Tax anatarajia kuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya miaka 41 ya kuanzisha kwa Shirika la Uzalishaji mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMAJKT).
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Juni 25, 2022 Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMAJKT),Kanali Petro Ngata amesema, maadhimisho hayo yanatarajia kufanyika sambamba na maonesho ya 46 ya biashara ya Kimataifa Sabasaba katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere.

Amesema, shirika lao linajivunia kusherehekea miaka 41 tangu kuanzishwa kwake kwani limeweza kufanikiwa kutimiza malengo ya uanzishwaji wake ikiwemo kuchangia gharama za uendeshaji wa shughuli za JKT na kusaidia katika kujenga uchumi wa nchi.

''Maadhimisho haya tunatarajia kuanza Juni 29,mwaka huu na kilele chake kitakuwa Julai Mosi,2022 kipindi chote shirika limeweza kufanikiwa kutekeleza miradi mbalimbali ya kibiashara na ile ya huduma yenye maslahi ya kitaifa ikiwemo ujenzi wa ukuta kuzunguka mgodi wa madini ya Tanzanite Mirerani mkoani Manyara na kujenga mji wa Kiserikali jijini Dodoma,''amesema.

Amesema pia shirika lao limefanikiwa kuchangia pato la taifa kwa kutoa gawio Serikalini na kutoa kodi stahiki kupitia kampuni zake tanzu mbalimbali.

''SUMAJKT limesaidia kutoa ajira kwa vijana wa kitanzania kupitia kampuni na miradi yake ikiwemo Kampuni ya Ulinzi SUMAJKT Guard hadi sasa imetoa ajira kwa vijana zaidi ya 16000,''amesema na kuongeza,

''Shirika limekuwa likisaidia vijana wa Jeshi la Kujenga Taifa kujifunza stadi za kazi kupitia shughuli zake mbalimbali za uzalishaji mali ikiwemo kilimo,ufugaji ,ujenzi,utengenezaji wa Samani na bidhaa za ngozi,''amesema.

Post a Comment

0 Comments