UNICEF kuwarudisha shuleni watoto kutoka Tabora, Songwe na Kigoma

NA RESPICE SWETU

ZAIDI ya watoto laki moja wa mikoa ya Tabora, Songwe na Kigoma wenye umri wa miaka 7-14 walio nje ya mfumo rasmi wa elimu, wanatarajia kunufaika na mpango wa elimisha mtoto utakaotekelezwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) kwa ufadhili wa nchi ya Qatar.
Kaimu Ofisa Elimu wa Mkoa wa Songwe, Mtinga Maleya (kushoto) na Kaimu Ofisa Elimu wa Mkoa wa Kigoma, David Mwamalasi (kulia) wakiwa na mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Batilda Buriani (katikati) wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi huo iliyofanyika katika Manispaa ya Tabora.

Hayo yamebainika wakati wa hafla ya uzinduzi wa mpango huo iliyofanyika kwenye viwanja vya Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Askofu Marko Mihayo kilichopo Manispaa ya Tabora.

Akisoma hotuba kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) aliyetarajiwa kuhudhuria hafla hiyo, mkuu wa mkoa wa Tabora, Balozi Batilda Buriani alisema, hakuna taifa linaloweza kupata mafanikio iwapo kuna watu wasiojua kusoma na kuandika.

Amesema kuwa, mpango huo utakaotekelezwa kwa miaka mitano, unatokana na utafiti ulioibaini mikoa hiyo kuwa na idadi kubwa ya watoto wenye umri wa kwenda shule ambao hawapo shuleni.

Uzinduzi wa mpango huo wenye kauli mbiu isemayo tushirikiane kuwaandikisha na kuwarudisha shuleni watoto walio nje ya mfumo rasmi wa elimu, ulitanguliwa na kikao kazi cha maofisa elimu msingi na kitengo cha elimu ya watu wazima wa halmashauri 21 za mikoa ya Tabora, Songwe na Kigoma pamoja na maofisaelimu wa mikoa hiyo.

Katika kuupokea mpango huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, amewaagiza watendaji wa kata, waratibu elimu wa kata, walimu wakuu na watendaji wa vijiji kwenye maeneo yenye shule zitakazohusika na mpango huo, kuanza kuwabaini na kuwasajili watoto wote wanaostahili kunufaika na mpango huo.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana kutoka ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, vituo vitakavyohusika na mpango huo vitakuwa katika shule za msingi za Kitanga, Kigadye, HeruUshingo, Nyarugusu, Makere, Mwali, Mvinza, Kagera, Titye na Kabulanzwili.

Post a Comment

0 Comments