Wasafirishaji wampongeza Rais Samia, Serikali

NA GODFREY NNKO

CHAMA cha Wasafirishaji Tanzania (TAT) kimempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Serikali kwa ujumla kwa kusikiliza na kufanyia kazi maoni ya wasafirishaji nchini kwenye bajeti ya Mwaka 2022/2023.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Juni 26, 2022 na Ofisi ya Rais wa Chama cha Wasafirishaji Tanzania (TAT), Mohammed Abdullah.

“Kwa niaba ya Chama cha Wasafirishaji Tanzania (TAT), Bodi, Wanachama na Wasafirishaji wote nchini, tunapenda kukupongeza Mh.Samia Suluhu Hassan,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na wasaidizi wako kwa
kuwasikiliza Wasafirishaji wa mizigo katika Bajeti ya Mwaka 2022/23. 

"Tunayo furaha kubwa kukupa pongezi za dhati kabisa pamoja na wataalamu wako ambao wamekuwa wakifanya kazi nzuri kuishirikisha Sekta Binafsi katika masuala mbalimbali ya Bajeti na Kodi.

“Tunashukuru sana kwa punguzo katika Kodi ya Matrela na Vichwa vya Magari ya kusafirishia mizigo hadi asilimia sufuri, na Punguzo katika Tozo ya matumizi ya barabara kutoka dola za Marekani 16 kwa kilomita 100 hadi dola 10 kwa kilomita 100. Tunakupongeza Rais Mama Samia Suluhu Hassan na Serikali yako kwa kuwa sikivu kwa maombi ya Wasafirishaji nchini na tuna imani kubwa kuwa changamoto ambazo hazijatatuliwa, zitafanyiwa marekebisho ili zilete tija katika Sekta ya Usafirishaji na nchi kwa ujumla,”imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

TAT ni chama chenye wanachama wasafirishaji wa mizigo na mafuta zaidi ya 200 nchini. Changamoto katika Sekta ya Usafirishaji zinawagusa moja kwa wanachama wake na wasafirishaji wote nchini.

Post a Comment

0 Comments