Watatu wauawa wakijaribu kuiba fedha Dar, askari ajeruhiwa begani katika majibizano ya risasi

NA DIRAMAKINI

WATU watatu ambao wanatuhumiwa kuwa ni majambazi wameuawa jijini Dar es Salaam wakiwa katika harakati za kutaka kuiba dukani huko Goba Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo jijini Dar es Salaam.

Watu hao wameuawa baada ya kupambana na maafisa wa Jeshi la Polisi.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Jumanne Murilo amesema kuwa, tukio hilo limetokea leo Juni 24, 2022 majira ya saa 6:45 mchana eneo la Goba Tegeta A, Wilaya ya Ubungo kwenye duka la miamala ya kifedha lililopo eneo lililofahamika kama Skymart Mini Supermarket.

Amesema, kundi la watu wanne wakiwa na pikipiki namba MC 469 CMT aina ya TVS huku wamejihami kwa silaha za moto, walifika eneo hilo kwa lengo la kuvamia na kupora fedha katika duka hilo.

Kamanda Muliro amesema, taarifa zilitolewa haraka na askari Polisi walipofika eneo hilo walianza kushambuliwa kwa risasi na katika mazingira hayo askari namba F3625 SGT Eliamini alijeruhiwa kwa risasi chini ya bega karibu na kifua.

Amesema,majambazi nao walishambuliwa na kujeruhiwa vibaya, ambapo walipelekwa haraka hospitali lakini kwa bahati mbaya watatu wamepoteza maisha na mmoja alitoroka. Hali ya askari aliyejeruhiwa inaendelea vizuri.

Kamanda amesema, uchunguzi wa awali umeonesha kuwa kati ya majambazi hao, wawili wametambuliwa kuwa ni Ridhiwani Sunna Mgeni (Babu Ally) aliyewahi kushtakiwa kwa kesi ya mauaji PI 148/2006 na Rajabu Ramadhani (Rogers) aliyewahi kushtakiwa kwa mauaji PI 28/2014.

Majambazi hao wamekutwa na silaha mbili aina ya Long rifle 22 iliyotengenezwa Ubelgiji yenye risasi 11 pamoja na Pistol aina ya Star yenye risasi sita.

Amesema, jeshi hilo linaendelea na ufuatiliaji wa makundi yote yanayojihusisha na kupanga njama na kujaribu kutelekeza vitendo vya kihalifu.

Pia amesema kuwa,jeshi halitavumilia na halitasita kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria kwa yeyote atakayejihusisha na uhalifu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news