Wazee wa mila, wachimbaji waelimishwa fursa, sheria na ushiriki Sekta ya Madini

NA STEVEN NYAMITI-WM

IMEEELEZWA kuwa, mafunzo kwa wachimbaji na wazee wa mila yamelenga kutoa elimu katika masuala mbalimbali yatakayohusu Sheria ya Madini, uchimbaji na usimamizi wa mazingira katika maeneo ya uchimbaji ili kutambua taratibu za uwekezaji katika madini ikiwemo jinsi ya kupata leseni, uchimbaji bora na utunzaji wa mazingira.
Hayo yamebainishwa leo Juni 3, 2022 na Mkuu wa Wilaya ya Longido Nurdin Babu wakati akifungua mafunzo ya siku mbili yanatolewa na wataalamu wa Wizara ya Madini mkoani Arusha.

"Mafunzo hayo yatawasaidia kupata uelewa mpana wa shughuli zinazofanyika katika Sekta ya Madini na kupata elimu itakayowawezesha kupata maeneo kwa ajili ya uchimbaji," amesisitiza.

Mkuu wa Wilaya Babu, amewataka watumie mafunzo hayo kujifunza masuala mbalimbali yanayohusu Sekta ya Madini kwa kupata elimu inayotolewa na wataalam kutoka Wizara ya Madini ili wapate elimu kwa manufaa ya wachimbaji wadogo wote nchini.

"Ninawataka mtumie mafunzo haya vizuri, waelewe, waulize maswali waliyonayo pale ambapo hawapaelewi ili wakitoka hapa watakuwa na elimu itakayowasaidia katika uchimbaji," amesema.

Pia ameongeza kuwa, mafunzo hayo yatasaidia kupunguza changamoto walizonazo wachimbaji katika masuala ya Sheria, Leseni, Utafiti, Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini na Wajibu wa Makampuni kwa jamii zinazozunguka migodi.

Naye, Kamishna Msaidizi wa Uendelezaji Migodi, Theresia Ntuke amesema, mafunzo hayo yamelenga kuwasaidia wachimbaji na kufahamu namna ya kuwekeza ili waweze kunufaika na rasilimali madini iliyopo katika maeneo yao baada ya kupata elimu sahihi.

"Matarajio yetu ni kuwaona wawekezaji wananufaika na rasilimali madini tuliyonayo hususan kwa wenyeji wa hapa na kuepusha migogoro inayoweza kutokea," amesisitiza.

Akizungumzia masuala ya Sheria, Afisa Sheria Mwandamizi wa Wizara ya Madini, Damian Kaseko amesema, mada aliyoitoa inalenga kuwaelimisha wazee wa mila ili kupata uelewa wa Sheria ya Madini katika uombaji wa leseni, usimamizi wa leseni na mambo mengine yanayosimamiwa na Sheria ya Madini.
Naye, Kamishna Msaidizi wa Usimamizi wa Mazingira, Gilay Shamika, akieleza Mpango wa Usimamizi wa Mazingira amesema, mmiliki wa leseni ya uchimbaji inamtaka mmiliki wa leseni ndogo ya uchimbaji kuandaa taarifa ya mambo ya msingi kwa kutumia mtaalam wa mazingira.

Pia amesema, mambo ya msingi yanayopaswa kufanyika wakati wa kuandaa mpango wa usimamizi wa mazingira ni kuonesha kama kuna makazi ya watu katika eneo hilo, historia ya urithi wa eneo na kuonesha aina ya uoto wa asili katika eneo hilo na aina ya udongo.

Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi wa Arusha, Mhandisi Alphonce Bikulamchi amesema, mafunzo hayo yatasaidia katika kuelimisha jamii kwa masuala mbalimbali katika Sekta ya Madini kuhusu taratibu za utoaji wa leseni, taratibu za uchimbaji madini na masuala ya mazingira ili iweze kufuata taratibu zilizopo kwa mujibu wa Sheria ya Madini Sura Namba 123 na Kanuni zake.
"Kumekuwa na umuhimu mkubwa sana wa kuleta elimu hii ya sheria ya madini katika maeneo haya ili kutoa uelewa kwa jamii ili iweze kuona manufaa yatokanayo na Sekta ya Madini katika maeneo yao," ameongeza.

Mafunzo hayo ya siku mbili yamewakutanisha wachimbaji, wadau, wafanyabiashara wa madini na viongozi wa chama na Serikali ili kujadili kwa pamoja masuala mbalimbali katika Sekta ya Madini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news