Waziri Makamba ateua nane TPDC

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Nishati, Mheshimiwa January Makamba (Mb) amewateua wajumbe nane wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

Uteuzi huo ameufanya Juni 10, 2022 kufuatia uamuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kumteua Balozi Ombeni Sefue kuwa Mwenyekiti wa bodi hiyo. Mheshimiwa January Makamba amesema kuwa, uteuzi huu unaanza mara moja.
Waziri wa Nishati, Mheshimiwa January Makamba. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mheshimiwa Waziri January Makamba wajumbe walioteuliwa ni Ruth Zaipuna ambaye ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB.

Zaipuna aliwahi kuwa, Mkaguzi wa Mahesabu ya Price WaterHouseCoopers na Afisa Mkuu wa Fedha Standard Chartered.

Pia Mheshimiwa Waziri amemteua, Dkt.Natu Mwamba ambaye ni Mhadhiri Mwandamizi katika Shule ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Dkt.Mwamba amewahi kuwa Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania.

Tatu, Mheshimiwa Waziri amemteua Musa Makame ambaye ni Mshauri Mwelekezi katika sekta ya mafuta na gesi. Makame amewahi kuwa Afisa Mwandamizi wa Biashara katika Kampuni ya Equinor (zamani Statoil) na kabla ya hapo Makamu wa Rais (Fedha na Utawala) katika Kampuni ya Wentworth (zamani Artumas).

Nne, Mheshimiwa Waziri amemteua Mpambika William Chiume ambaye ni Mshauri Mwelekezi kwenye Sekta ya Mafuta na Gesi. Chiume aliwahi kuwa Naibu Mkurugeni Mkuu wa Kampuni ya PanAfrican Energy na Mkuu wa Masuala ya Biashara wa Kampuni ya Ophir Energy na pia kama Msimamizi wa Miradi Kenya na Seychelles.

Tano, Mheshimiwa Waziri amemteua Protas Ishengoma ambaye ni Mwanasheria Mbobezi wa Sekta ya Mafuta na Gesi. 

Sita, Mheshimiwa Waziri amemteua Paul Makanza ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC),Mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI) na Makamu Mwenyekiti wa Tanzania Private Sector Foundation (TPSF).

Saba, Mheshimiwa Waziri amemteua Dismas Fuko ambaye ni Mshauri Mwelekezi wa Miradi ya Nishati hasa kwenye uchambuzi wa kifedha (Project Financial Modelling). Aliyekuwa Mkurugenzi wa Masoko na Uwekezaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

Uteuzi wa nane, Mheshimiwa Waziri amemteua, Balozi Peter Kallaghe ambaye ni Mkufunzi wa Chuo cha Ulinzi cha Taifa (National Defence College). Balozi Kallaghe aliwahi kuwa Msaidizi wa Rais Ikulu na kwa nyakati tofauti alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Canada na Cuba.

Post a Comment

0 Comments