Bosi mpya TPA apewa wiki mbili kuhusu Bandari ya Bagamoyo

NA MWANDISHI WETU 

NAIBU Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete, ametoa siku Kumi na Nne (14), kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuwasilisha ripoti ya vitu vyote muhimu vinavyohitajika kwa maboresho ya miundombinu katika Bandari ya Bagamoyo. 
Meneja Miliki wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Alexander Ndibalema, akimuonesha Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupeleke Mwakibete (mwenye koti la Buluu), eneo lililotengwa kwa ajili ya Ujenzi wa Bandari ya Mbegani, wakati Naibu Waziri alipotembelea eneo hilo, wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.

Akizungumza mara baada ya kukagua Bandari hiyo mkoani Pwani, Naibu Waziri Mwakibete, amesema kuboreshwa kwa Bandari hiyo kutarahisha shughuli za utalii nchini na hivyo kukuza pato la wananchi wa mkoa huo na Taifa kwa ujumla. 

“Kwa kuwa eneo hili la Bagamoyo ni muhimu sana kwa utalii nampa Mkurugenzi Mkuu wa TPA wiki mbili alete watalaam hapa waangalie vitu muhimu vya kuboresha”, amesisitiza Naibu Waziri Mwakibete. 

Naibu Waziri Mwakibete amesema pamoja na maboresho ambayo Serikali imejipanga kuyafanya kwa Bandari bado inaendelea na mkakati wake wa kurasimisha Bandari bubu zinazozunguka eneo la Bahari ya Hindi ili kuweza kupunguza biashara za magendo ambazo zimekuwa zikiendelea kufanyika bila usimamizi mzuri. 

Naye, Meneja Miliki wa TPA, Ndibalema Alexander, amemuhakikishia Naibu Waziri Mwakibete kuwa TPA iko tayari na itatuma watalaam wa kufanya tathmini ya mahitaji halisi ya maboresho ya miundombinu ya Bandari hiyo lengo likiwa ni kuongeza wigo wa mapato kwa Mamlaka na kuhakikisha wananchi wanapata huduma katika miundombinu bora. 
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupeleke Mwakibete, akizungumza na wazee wa Wilaya ya Chalinze wakati alipotembelea Wilaya hiyo, mkoani Pwani. Kulia kwa Naibu Waziri Mwakibete ni Naibu Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi ambaye pia ni Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze, Hassani Rajabu, ameishukuru Serikali kwa kutupia jicho Bandari ya Bagamoyo na kusema maboresho ya miundombinu yatakayofanywa na Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, itaongeza pato kwa kuwa itaongeza idadi ya watalii wanaotembelea vivutio mbalimbali vilivyopo mkoani Pwani. 

Naibu Waziri Mwakibete yuko mkoani Pwani kwa ziara ya kikazi ya siku mbili ya kukagua miradi mbalimbali inayosimamiwa na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news