Chunga kinywa chako kisiwe chanzo cha maumivu, mauti kwa wengine

NA DIRAMAKINI

IJUMAA iliyopita, nilikuwa darasani nikiwafundisha wanafunzi wangu ndipo mwanafunzi mmoja wa kike akainua mkono kuuliza swali.

Nilimruhusu na akauliza swali rahisi sana ambalo nilidhani anapaswa kujua jibu lake maana tayari nilikuwa nimezungumzia mada hiyo wiki iliyopita.

"Kaa chini, tafadhali! Na sura yako mbaya! muone!" ndilo jibu pekee nililompa. Darasa zima liliangua kicheko na alionekana kufedheheka sana.

Niliendelea na somo langu, lakini nilihisi kuwa na hatia kwa sababu ya kile nilichokuwa nimesema. Nilimaliza kipindi changu na kuondoka. Siku ya Jumapili, nilienda Kanisani. Mhubiri alikuwa akiongea juu ya nguvu ya ulimi.

Alizungumza juu ya jinsi unavyoweza kuwavunja moyo, kuwakatisha tamaa na kuwaangusha kabisa wengine kwa kile unachosema.

Nilikumbuka kile kilichotokea Ijumaa na nikajiona ni mwenye hatia zaidi. Niliapa kuwa nitaenda kumuomba msamaha Jumatatu nikifika darasani.

Jumatatu alasiri, nilienda darasani lakini sikumuona yule mwanafunzi. Nilimuulizia kwa wenzake, lakini hawakuonekana kujua ni nani hasa niliyekuwa nikimzungumzia. Ndipo nikasema "ninamtafuta mtu niliyemtukana Ijumaa".

"Aah, huyo ni Furaha, mwalimu! Hayuko darasani leo" walijibu. Rafiki yake ni nani? Niliuliza. "Aisha", walijibu. Lakini Aisha pia hayupo darasani.

Ghafla, msichana aliye na Hijab aliingia. "Mwalimu, huyo ni Aisha" wanafunzi wangu walinijulisha. Yuko wapi rafiki yako? Nikamuuliza. "Yupi?" Alijibu bila kunitazama usoni. Furaha! Nilisema.


Yuko chumba cha kuhifadhia maiti.Alijibu. Jibu hilo lilinishtua! Chumba cha kuhifadhia maiti ??? Kufanya nini hapo ? Niliuliza. "Alifariki Ijumaa" Aisha alijibu. Imekuaje ??? Niliuliza.

Baadaye niligundua kuwa baada ya kipindi changu Ijumaa, Furaha aligongwa na gari lililokuwa likienda kwa kasi. Alikuwa akivuka barabara bila tahadhari, labda kwa sababu ya kile nilichosema. "Mazishi yake ni Jumamosi na umealikwa pia, mwalimu" Aisha aliendelea.

Wakati nilikuwa nimesimama nilijaribu kuudhibiti mshtuko niliokuwa nao, Aisha alisema huku akilia, "Mwalimu, umemuua rafiki yangu".

Alikuwa sahihi! Ninapaswa kuwa muuaji! Wasichana wengine darasani walikuwa tayari wanalia! Sikujua niseme nini, ikiwa ni kuomba msamaha kwa rafiki wa Furaha au kwa roho ya Furaha.

Niliwasilisha barua yangu ya kujiuzulu siku iliyofuata ikiwa na maneno haya: "Wapendwa Wahadhiri na Walimu, tafadhali acheni kutukana wanafunzi wenu. Wako shuleni ili kujifunza kutoka kwenu. Ingekuwa tayari wanajua, wasingekuwa shuleni".

Tafadhali fikiria kile unachosema kwa watu wengine. Je? Maneno yako yanaleta uhai au kifo kwa wasikilizaji?

ZINGATIO: HADITHI HII NI LAZIMA ISOMWE NA HAIWAHUSU WALIMU TU BALI SISI WOTE TUNAPOKUWA TUNAWASILIANA NA BINADAMU WENZETU: WATEJA, WANAFUNZI, WAZAZI, WENZIO, MARAFIKI NA KADHAlIKA.

Yatupasa tuwe waangalifu sana juu ya jinsi tunavyosemezana.

Asante.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news