DCB yazindua kampeni kusherehekea miaka 20 ya mafanikio

NA DIRAMAKINI

BENKI ya Biashara ya DCB imezindua kampeni kusherehekea miaka 20 ya mafanikio tokea ilipoanzaishwa huku Mkurugenzi Mtendaji wake, Godfrey Ndalahwa akianisha mambo kadhaa yakiwemo mafanikio na mipango ya baadae.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara ya DCB, Godfrey Ndalahwa (katikati) akizingumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kusherehekea miaka 20 ya mafanikio ya benki hiyo jijini Dar es Salaam hivi karibuni. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Uendeshaji, Nelson Swai, Mkurugenzi wa Mikopo, Isidori Msaki, Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano, Rahma Ngassa na Mkurugenzi wa Wateja Binafsi, Ester Bgoya.

"Kama mnavyofahamu benki yetu inasherehekea miaka 20 tokea kuanzishwa kwake kipindi hicho ilipoanzishwa mwaka 2002 ikijulikana kama benki ya Kijamii ya Dar es Salaam (Dar es Salaam Community Bank), kutimiza maono ya Rais wa Awamu ya tatu, Hayati Benjamin William Mkapa kufuatia kilio cha wajasiriamali wakazi wa Dar es Salaam kukosa huduma za kifedha hususani mikopo baada ya kukosa vigezo katika taasisi nyingi za fedha, kwa kipindi hicho benki ilianza na mtaji wa shs bilioni 1.7. 

"Mafanikio tunayojivunia ni makubwa na ninapenda kuchukua fursa hii kuainisha baadhi ya mafanikio hayo: Ikumbukwe kuwa DCB ilikuwa benki ya kwanza kuorodheshwa katika soko la hisa la Dar es Salaam (DSE) baada ya kutimiza vigezo na masharti ya mamlaka mbalimbali za udhibiti hapa nchini. Kuorodheshwa katika soko la hisa haikuwa tu fursa kwa umma kumiliki benki na kutengeneza faida iliyotokana na gawio pamoja na kuuza na kununua hisa, bali imekuwa fursa kubwa zaidi kwa benki kuongeza mtaji pindi unapohitajika. 

"Niwashukuru sana wanahisa wetu kwa kuendelea kushiriki katika mazoezi ya uuzwaji wa hisa jambo ambalo limesaidia kukuza mtaji wa benki yetu kutoka shilingi bilioni 1.7 hadi kufikia shilingi bilioni 30 hivi sasa. Mtaji huu umeiwezesha benki kukidhi masharti ya benki kuu ya kujiendesha kama benki ya biashara na kuiongezea benki yetu uwezo mkubwa wa kushindana katika soko.

Mwaka 2012 benki yetu ilifanikiwa kuhuisha leseni kutoka kwenye benki ya jamii na kuwa benki kamili ya biashara ambayo imepanua wigo kwa benki yetu kuweza kushindana katika soko ikihudumia wateja wadogo, wa kati na wakubwa. Katika kufanikisha hayo, benki iliweza kufungua matawi 9, na mawakala zaidi ya 700 maeneo tofauti nchini. 

Benki yetu pia haikuwa nyuma katika kuanzisha mifumo ya kidijitali ambayo kwa sasa ndio ushindani wa soko ulipo, hivyo mnamo mwaka 2016, benki ilianza kutoa huduma za kibenki kwa njia ya simu na mtandao na imeendelea kuboresha huduma hizo kadri teknolojia inavyozidi kubadilika. Huduma hizi za Kidijitali zimewezesha kufikia wateja wengi zaidi kwa muda mfupi hivyo kurahisisha shughuli za utoaji huduma. 
Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Biashara ya DCB, Rahma Ngassa (wa pili kulia) akizungumza katika mkutano ambao Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Godfrey Ndalahwa (wa tatu kushoto) alipokutana na waandishi wa habari kuzungumzia uzinduzi wa kampeni ya kusherehekea miaka 20 ya mafanikio ya benki hiyo jijini Dar es Salaam. Wengine kutoka kushoto ni; Mkurugenzi wa Uendeshaji, Nelson Swai, Mkurugenzi wa Mikopo, Isidori Msaki na Mkurugenzi wa Wateja Binafsi, Ester Bgoya.

Wakati benki inaanzishwa ilijikita kwenye kuhudumia wafanyabiashara wadogo na wateja binafsi wa jiji la Dar es salaam ambapo kiwango cha utoaji mikopo kwa mteja mmoja kilianzia shilingi 200,000 hadi shilingi milioni 5. Kwa kipindi cha miaka 20, benki yetu inajivunia kutoa jumla ya mikopo yenye thamani isiyo pungua trilioni 1 ambayo imenufaisha watanzania wasiopungua 400,000. Aidha baada ya kuboresha leseni yake kiwango cha utoaji mikopo kiliongezeka hadi kufika uwezo wa kukopesha bilioni 5 kwa mteja mmoja. Kadhalika, mikopo hiyo sasa hunufaisha wafanyabiashara wote yaani wadogo, kati na wakubwa bila kusahau wateja binafsi popote nchini.

"Leo ninayo furaha kutamka kwamba, wateja hao waliokuwa wakikopa shilingi 200,000 wameweza kupanua mitaji yao na hivyo kuwawezesha kumudu majukumu yao ikiwemo ada za watoto, ujenzi wa nyumba na mengineyo. Baadhi yao wameweza kuongeza uwezo wa kukopesheka kutoka shilingi 200,000 hadi kufikia shilingi milioni 100 na zaidi. 

Haya ni mafanikio makubwa kwa benki na kwa wateja wetu kwani tunaamini lengo la waasisi la kuhakikisha watanzania wanapata huduma wanayostahili na kwa wakati limefanikiwa. Benki inaendelea kuboresha huduma ikihakikisha wananchi wengi zaidi wananufaika. Wakati tunaanza wateja walikuwa takribani 6,530 ambao wameongezeka hadi kufikia zaidi ya wateja 200,000. 

Sambamba na ongezeko hilo la wateja, imani ya wateja na benki yetu imeendelea kukua na kupelekea amana nazo kukua. Katika kipindi cha miaka hiyo benki yetu imefanikiwa kukuza amana za wateja mwaka hadi mwaka na kufikia bilioni 125 Desemba mwaka jana, huku tukijiwekea malengo ya kufika bilioni 162 mwisho wa mwaka huu.

Zaidi ya mafanikio katika namba, benki yetu imeendelea kuwa kinara katika maswala ya utawala bora. Benki imekuwa ikishinda tuzo mbalimbali ikiwemo tuzo zitolewazo na Bodi ya taifa ya wahasibu na wakaguzi (NBAA) kama mtoa taarifa bora za kifedha katika kipengele cha benki ndogo na za kati miaka 8 mfululizo. 

Mwaka 2018 benki yetu ilipokea tuzo kutoka soko la hisa la Dar-es-Salaam (DSE) katika sekta ya benki na uwekezaji chini ya kipengele cha utawala bora ulinzi sahihi wa wawekezaji, utekelezaji bora wa sera za mazingira. Mwaka 2021 benki yetu ilipata tuzo ya Consumer Choice Awards, ikiwa ni tuzo ya kwanza kushinda ambapo wateja wetu walitupigia kura kuonesha kufurahishwa kwao na huduma zetu.

Wakati benki inatimiza miaka 20 kwa mafanikio makubwa, ni vyema kuwakumbusha kwamba tumetimiza miaka minne toka tuanze safari yetu ya mabadiliko. Tulianza safari yetu ya mabadiliko mwaka 2018 tukikabiliana na mahitaji ya kuboresha mtaji ili kuweza kushindana katika soko, mikopo chechefu kuwa katika kiwango cha juu sana, ukwasi usio ridhisha kwa maendeleo ya benki pamoja na benki kujiendesha kwa hasara. 

Katika safari hii, Benki ilijiwekea malengo makuu matatu:
 

Lengo la kwanza lilikuwa ni kurejesha benki katika hali yake ya kupata faida mwaka hadi mwaka, lengo ambalo ndani ya miaka minne tumeweza kulifanikisha kwa kiwango kikubwa.

Lengo la pili, lilikuwa ni kuhakikisha benki inakuwa imara na kuendelea kushindana. Ndugu waandishi wa habari, katika eneo hili benki ilijikita katika kukuza mtaji, kuongeza ukwasi na kupunguza mikopo chechefu.

Lengo la tatu, lilikuwa ni ukuaji na upanuzi wa Benki ambapo kwa Pamoja tulijadili na kukubalina taswira mpya ya mafanikio.Kwa ushirikiano wa wanahisa wetu na maelekezo thabiti ya Bodi ya wakurugenzi na juhudi za wafanyakazi wenzangu pamoja na imani ya wateja wetu, tumeweza kukabiliana na changamoto hizi na kwa sasa benki yetu imeweza kujiendesha ikiwa imekidhi kiwango cha mtaji kinachotakiwa kisheria, benki ina ukwasi unaoridhisha,kiwango kidogo cha mikopo chechefu na benki imeendelea kupata faida kwa miaka yote minne mfululizo.

Ndugu waandishi wa habari, Mwaka 2020 Bodi ya Wakurugenzi na Uongozi wa benki uliweza kuainisha taswira mpya ya mafanikio ya benki kuelekea mwaka 2025 kama ifuatavyo: 

Kuongeza kiwango cha faida kinachopatikana kila mwaka hadi kufikia kiasi cha shilingi bilioni 11 mwaka 2025.  

Kutoa huduma bora zaidi kwa wateja na hivyo kuongeza idadi ya wateja hadi kufikia wateja 400,000 ifikapo mwaka 2025. 

Kuongeza ufanisi na udhibiti wa mali za benki

Kuhakikisha benki yetu inakua mwajiri bora mwenye kuvutia wafanyakazi wenye uwezo na ari kubwa ya kufanya kazi.Vipaumbele vitano vitakavyofanikisha taswira mpya ya mafanikio: 

1. Kukuza kiwango cha mikopo kwa wateja kutoka kiasi cha shilingi bilioni 104 mwaka 2020 hadi kufikia shilingi bilioni 290 mwaka 2025. Sambamba na hiyo kupunguza mikopo chechefu hadi kufikia chini ya asilimia 5. 

Mwaka 2021 benki imefanikiwa kukuza mikopo yake hadi kufikia shilingi bilioni 121 ambayo ni sawa sawa na ongezeko la asilimia 16 kwa mwaka. Na pia benki imeweza kupunguza mikopo chechefu kutoka asilimia 11.6 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 7.3 mwaka 2021. 

2. Kuongeza mapato yasiyotokana na riba (non funded income) katika mchango mzima wa mapato ya benki kutoka kiwango cha asilimia 26.4 mwaka 2020 hadi kufikia kiwango cha asilimia 35 mwaka 2025. Lengo hili linalenga kupunguza utegemezi mkubwa wa mapato yanayotokana na mikopo ili kuiwezesha benki kuwa imara zaidi na kuhimili changamoto zinazotokana na mabadiliko ya kiuchumi. 

Ili kufanikisha lengo hili benki imejikita zaidi kuboresha biashara za bima (bancassurance), huduma za malipo ya kidijitali (GePG, Internet Banking, Mobile Banking, International Money Transfer etc). Benki imefanikiwa kuongeza mapato yasiyotokana na riba kutoka asilimia 26.4 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 30.8 mwaka 2021.

3. Benki inalenga kuongeza mchango wa amana za gharama nafuu katika amana zote za benki kutoka asilimia 34 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 60 ifikapo mwaka 2025. 

Nia ya lengo hili ni kupunguza gharama zitokanazo na amana za muda maalumu (Fixed Deposits), ambapo kupungua kwa gharama hizi kutachangia kuongezeka kwa faida na kuleta ongezeko la thamani kwa wanahisa. 

Benki imeweka mikakati mbalimbali ya kuongeza amana zake ikiwemo kujikita zaidi katika kuboresha na kuleta bidhaa na huduma zenye tija na ubunifu,tutaendelea kuongeza wateja mbalimbali ikiwemo VICOBA, SACCOS, wajasiriamali, wafanyakazi na makundi mbalimbali, kufanya kazi na Mashirika ya simu pamoja na taasisi za serikali. Benki imeunganishwa na mfumo wa malipo ya serikali (GePG) na imeaanza mahusiano na taasisi mbalimbali za serikali zikiwemo manispaa za mkoa wa Dar Es Salaam, Mamlaka ya bandari Tanzania (TPA) na taasisi nyingine za serikali. Mahusiano haya yanatarajia kukuza amana za benki zitokanazo na makusanyo ya mapato ya serikali. 

4. Kukuza mtandao wa benki kwa ufanisi – Benki ya DCB imeshaweka lengo lenye shauku la kutoa huduma nchi nzima ifikapo mwaka 2025. Hii itawezekana kupitia muundo wetu wa kibiashara wa kufungua matawi na kusambaza huduma katika maeneo ya karibu kupitia vituo vidogo vidogo na tekinolojia ya kimtandao (hub and spoke). 

Benki inatarajia kufungua matawi mapya 5 na vituo vidogo (DCB Jirani) vipatavyo 28. Kwa sasa benki ina matawi 9 likiwemo tawi letu la Dodoma na tawi jipya la Victoria, vituo vidogo 5 vinavyotumika kutoa huduma mbalimbali za kibenki. Vituo hivyo vipo Dar Es Salaam, Mbeya, Mwanza, Morogoro, na Singida. 

5. Benki ya DCB inalenga kuongeza wigo wa mikopo itolewayo kidijitali hadi kufikia asilimia 50 ya mikopo yote ifikapo mwaka 2025. Benki ipo kwenye hatua za mwisho za makubaliano na taasisi mbalimbali zenye mifumo ya teknolojia na makampuni ya simu yenye idadi kubwa ya wateja waliohakikiwa. 

Lakini pia DCB itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita ya Mama Samia Suluhu Hassan katika azma yake ya kuwainua watanzania kiuchumi na kuchangamkia pia fursa za kifedha zitokanazo katika miradi mbalimbali ya kimaendeleo inayoendelea hapa nchini.

Natoa wito kwa watanzania kujiunga na benki yetu na kufaidika na fursa mbalimbali za huduma bora za kibenki zitolewazo na benki yetu, DCB ni Mkombozi wa Kweli kwa watanzania wote, wajasiriamali wadogo, wa kati, wanawake na vijana DCB ni Mkombozi wa Kweli kwa wafanyabiashara wa kada zote,"alifafanua kwa kina Mkurugenzi huyo mbele ya waandishi wa habari.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news